Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia pumzi na kauli, na mimi kusimama katika Bunge hili tena kwa kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Michezo, Vijana na Utamaduni. Namshukuru sana Mungu kwa kuzidi kunipa pumzi na leo nitamtanguliza Mungu, nipo kwenye swaumu, nitakayoyasema, basi yawe mustakabali katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Michezo, naomba kwa dhati ya moyo wangu kabisa, yale mazuri yaliyozungumzwa na Kambi ya Upinzani kupitia Waziri Kivuli uyachukue uyafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika sana ndani ya moyo wangu na ndani ya nafsi yangu na moyo ukanisuta na nafsi ikanisuta kama mwanamke; na katika mwanamke ambaye nimelelewa katika maadili ya kiislamu, nikalelewa na wamama ambao walinitangulia katika siasa, wamama wa Kizanzibar; akiwemo sasa hivi ni Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu na Mama Amina Salum Ally na wakifuatia wengine, hata dada yangu Saada ambaye nilifanya naye kazi katika Wizara ya Fedha kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitika kwa nini? Leo hii dada yangu Mheshimiwa Malembeka, huwezi kumdhalilisha mwanamke mwenzako kiasi kama hicho na wewe ni mwanamke. Tumekaa ndani ya Bunge hili, wanawake katika Bunge la Mama Anna Makinda tulipata maadili kutoka kwa Mheshimiwa Mama Anna Abdallah, kwa Mheshimiwa Jenista Muhagama; walitupokea kama model katika Bunge hili na tukafuata nyayo zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina wasiwasi kabisa dada yangu, huna maadili ya Kizanzibari. Angalia Mawaziri wote waliotoka Zanzibar, mfano kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, angalia maadili aliyonayo ya Kizanzibari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kwa kaka yangu Waziri wa Ujenzi, angalia maadili aliyokuwa nayo, angalia maadili ya Wizara mbalimbali zilizoongozwa na Wazanzibar katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na hata wengine sasa hivi wamefika nyadhifa za juu, ni Makamu wa Rais hawajahi kutukana matusi kama unayoyatoa ya kumdhalilisha mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba kwa dhati kabisa Mheshimiwa Mama Sitta na akina Mheshimiwa Jenista na Mheshimiwa Ummy Mwalimu umekaa kwenye mambo ya jinsia, uangalie namna gani angalau sauti zile ziwe za upole, tusidhalilishane wanawake kwa wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, narudi kwenye hoja. Tatizo langu…
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, natambua weledi wako, wewe ni mwanasheria makini, wala hubabaishwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika TBC na vyombo vya habari kwa ujumla na waandishi wa habari. Waandishi wa habari ni kioo cha jamii, waandishi wa habari na televisheni zote tumeona wakiibua mambo mbalimbali katika jamii, wakiibua watu ambao wapo vijijini; siyo TBC, siyo ITV, siyo Channel Ten; na hata Watanzania hawa wakapelekwa nje ya nchi wakapona maradhi yao yaliyokuwa yanawasumbua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeona ndani ya Serikali wakiwemo Mawaziri na Mheshimiwa Waziri ambaye nilikuwa naye kwenye Kamati moja, namna gani vyombo vya habari vilikuwa vinambeba mpaka leo hii weledi wake na kazi yake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana na ninaishauri Serikali, msijenge chuki zisizokuwa na sababu kwa Watanzania na kwa wapiga kura wenu. Jambo hili ninyi mtaliona ni jepesi sana, mkalichukulia kimzaha lakini litawa-cost mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, angalia kwa makini sana namna gani Watanzania wapate habari kwa wakati muafaka na watazame Bunge linavyoendelea. Msiogope, mnaogopa kitu gani? Kwa sababu hata ninyi Mawaziri mkienda kufanya kazi katika sekta zenu, lazima muatumie waandishi wa habari. Kama mwandishi wa habari hajakutangaza, hajakuandika kwenye gazeti, kazi yako haiwezi kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna wapiga kura wenu wanatamani waone Mbunge wao kaongea nini? Waone Bunge la Bajeti linafanya kazi gani Dodoma; lakini mmeziba pamba masikioni na hii TBC mkasema sasa tena basi; lakini nakumbuka TBC ni ya walipa kodi na ndio wanaoichangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kingine zaidi nilikuwa naomba, kama hii TBC labda imekosa pesa, kwa nini hii channel ya Bunge isiangaliwe ni namna gani iboreshwe vyombo vyote vya habari virushe kupitia channel ya Bunge? Pia itaondoa sintofahamu ya TBC. Kwa hiyo, naomba mwandishi wa habari katika Tanzania hii athaminiwe na apewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa mdau sana wa waandishi wa habari. Mara yangu ya kwanza kuingia katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano nilikuwa kwenye Kamati ya Maendeleo ya Jamii na niliweza sana kuwatetea waandishi wa habari. Mwandishi wa habari anafanya kazi katika mazingira magumu. Leo hii waandishi wa habari wengine hawana hata bima ya afya. Kuna wengine wanakufa kwa ajili ya kuchukua habari, wanapata matukio mbalimbali, maisha yao yako hatarini kwa ajili ya kutafuta habari. Ni kwa nini mwandishi wa habari wa Tanzania anaminywa kiasi hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie ni namna gani ya kumboresha huyu mwandishi wa habari, pia wapewe maslahi yao ya kikazi. Yule mwandishi wa habari anayefanya kazi vizuri, pia muwe mnaandaa tuzo ya kuwatunza ili wawe na morali ya kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kupitia hao hao waandishi wa habari wameokoa maisha ya Watanzania, watoto wadogo na leo hii wamepona kabisa. Ni kwa nini tusiwaenzi waandishi wa habari na mkawapa habari kwa wakati muafaka bila kuminyaminya sekta hii ya habari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika lugha ya Taifa, lugha ya Kiswahili. Kiswahili ni lugha ya Taifa, tuangalie sasa hivi ni namna gani sisi Tanzania Kiswahili kinavyoporwa hapa kwetu. Sasa hivi unasikia Kenya wanatafuta ajira sehemu za Afrika ya Mashariki za walimu wa Kiswahili, lakini sasa Serikali imejipanga vipi kuhakikisha Kiswahili kinatangazwa na hata walimu wetu wa Kiswahili wanapata ajira katika Afrika Mashariki? Kwa sababu leo tunajivunia kwamba Kiswahili ni lugha ya Taifa, lakini tumekuta Kiswahili hatukitumii ipasavyo. Unakuta leo mtu anaongea Kiswahili anachanganya na Kiingereza, tunashindwa kuelewa huyu ni mswahili au ni muingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote iliyoendelea, haikuendelea kwa kuiga lugha, waliendelea kwa kusimama kwenye lugha yao. Leo ukienda China wanaongea Kichina, ukienda Korea, wanaongea Kikorea, ni kwa nini sisi tusienzi lugha yetu ya Taifa ambayo tuliachiwa na waasisi wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.