Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika Bajeti ya Wizara ya Madini. Kabla sijaanza mchango wangu nataka nimsaidie tu kaka yangu Iddi, Mbunge wa Msalala kwamba kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2019 kinaelekeza CSR utekelezaji wake ni lazima mipango yote ipangwe na halmashauri ikishirikiana na mgodi na halmashauri ni lazima itengeneze guideline ya namna ya kutekeleza CSR na imeweka haki zote za Baraza la Madiwani na Halmashauri kutekeleza. Kwa hiyo kama hawafanyi hivyo ina maana wametoa hisani kama watu wengine na hisani hiyo ni lazima itozwe kodi kwa sababu hawajafuata utaratibu wa kisheria.

Mheshimiwa Spika, tarehe 22/04/2020 nilisimama ndani ya Bunge hili Tukufu, pamoja na kashikashi zote nilisimama kwa ajili ya kuwatetea wachimbaji wadogo wadogo ambao wakiwa wanachimba sehemu kubwa ya mapato yao ilikuwa inachukuliwa na mtu anayeitwa mwenye shamba na fedha nyingine anachukua mtu ambaye anaitwa msimamizi. Leo kwa kweli kwa mara kwanza niseme tu nimpongeze Mheshimiwa Waziri alisilikiza kilio change, ametekeleza na sasa hivi kwa mara ya kwanza mchimbaji mdogo anapochimba na kupata dhahabu asilimia 70 ya mapato inakuwa ya kwake, huyo anayeitwa mwenye shamba anapata asilimia 15 na huyo anayeitwa msimamizi anapata asilimia 15. Mimi najivunia kwa sababu hoja niliyoisimamia imetekelezwa kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchukua maombi yangu ambayo niliyasema ndani ya Bunge hili mimi nina mambo mawili ambayo nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri ayasimamie. La kwanza, inaonekana kwamba asilimia kubwa ya watu ambao wana leseni za uchimbaji hawachimbi, wamezikalia leseni hizo. Hayo siyo maneno yangu, ripoti ya CAG inasema asilimia 58.3 ya watu wenye leseni za uchimbaji hawafanyi shughuli za uchimbaji, yaani ni leseni mfu.

Mheshimiwa Spika, vile vile ripoti hiyo inasema katika hiyo asilimia chache ambayo ya watu wanaochimba, asilimia 97 zaidi ya robotatu ya watu wanaochimba ni wachimbaji wadogo wadogo. Mheshimiwa Waziri naomba awanyang’anye leseni watu ambao wamezikalia leseni hizo na maeneo ya uchimbaji, hawafanyi shughuli za uchimbaji, badala yake wanawanyima fursa wachimbaji wadogo ambao wapo tayari kufanya shughuli za uchimbaji na wanajikuta wachimbaji wale wanachimba kwenye maeneo ambayo hayana potential ya kupata mali. Hilo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu la pili kwa Wizara hii; TRA wanakwenda kwenye masoko ambayo wachimbaji hawa wanakwenda kuuza dhahabu, masoko ambayo yameanzishwa hivi karibuni. Wakifika pale wanamkuta mchimbaji anauza dhahabu yake, tuseme milioni 200 au milioni 300, Waheshimiwa msishangae milioni 200 au 300 kwa mchimbaji ni hela ndogo sana akiipata. Anakwenda mtu wa TRA pale anamtoza ushuru kwa ile milioni 300 pato ghafi ambalo mchimbaji yule amelipata bila kujali kwamba kuna gharama za uchimbaji, bila kujali mtu yule amepata hasara kiasi gani, bila kujali kwamba mtu yule amewekeza kiasi gani? Sasa hawa wachimbaji wadogo mtu anaweza akachimba hata miaka 10 hajakutana na mali, anazika mtaji ardhini zaidi ya mamilioni ya fedha. Anapopata bahati anakwenda kuuza dhahabu yake anategemea angalau aweze, kuna watu wapo kwenye machimbo kule wana miaka zaidi ya 10 hawajawahi kuonana na familia zao.

Mheshimiwa Spika, naomba nimwombe Mheshimiwa Waziri akae pamoja na watu wa madini, wasitafute cheap income, hawa watu wana struggle kwenye machimbo na wenyewe waende kule wanakochimba wale watu. Wizara pia iliahidi kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo, nafahamu kwamba hii ni private sector, kuwapa mitaji mmoja mmoja ni vigumu, lakini ng’ombe anayekupa maziwa lazima umlishe, wenyewe wanakiri kwamba sekta ya madini ndiyo sekta inayolipa kuliko sekta nyingine yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde thelathini.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa faini aliyoitoza NEMC na Mheshimiwa Waziri kwenye Bonde la Mto Tigiti. Wametoza faini ya bilioni moja inaonekana ni kubwa, lakini kiuhalisia madhara makubwa yaliyopatikana kwa watu wale bado wanahitaji kulipwa fidia. Hatukubaliani kanda ya ziwa ndiyo inayoongoza… (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)