Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana. Pia kwa moyo wa dhati kabisa, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Ndejembi. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Rais ambaye amekuwa na imani na huyu kijana mchapakazi, mahiri kabisa na naomba tu niseme, kwa kweli nimeridhika sana kufanya kazi na huyu kijana, ni msaada mkubwa kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru pia watendaji wote kama nilivyosema mwanzo ndani ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa kazi kubwa ambayo tumekuwa tukiifanya kwa ushirikiano, taasisi zote na Watendaji Wakuu wa Taasisi zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa leo wala hatutaki kupiga maneno wala porojo, tunachotakiwa sasa ni kutoa maelezo ya Serikali na hasa kuhusiana na hoja ambazo zilijikita katika mjadala kwenye siku hii ya leo. Nianze kwanza kwa kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote, katika kuchangia kwako wamedhihirisha kabisa wapo hapa kwa niaba ya ustawi wa wananchi. Ustawi wa wananchi ni pamoja na huduma bora kwa wananchi zinazotolewa na watumishi wa umma nchini, lakini hatuwezi kupata huduma bora zinazotolewa na sekta hii ya watumishi wa umma nchini kama vile pia hatutakuwa na watumishi wa umma wa kutosheleza mahitaji yanayohitajika katika sekta mbalimbali nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, sisi kwa mwaka huu wa fedha tumejipanga kuyashughulikia yote, tunaongozwa na dira ya maendeleo, mpango wa maendeleo, Ilani ya Uchaguzi lakini vile vile maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yeye katika utumishi wa umma amesimama katika kuhakikisha haki na stahiki za watumishi wa umma zinalipwa kwa kuzingatia taratibu na sheria. Sasa jambo hilo hata sisi watendaji lazima tulifuate. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Rais ametuhimiza tusimamie utumishi wa umma ili kuhakikisha pamoja na Serikali kutekeleza wajibu wake wa kuzingatia haki na stahiki za watumishi wa umma ni lazima tujipange kuwa na mifumo itakayowasaidia watumishi wa umma hawa pia na wao wawajibike kwa Serikali yao, lakini wawajibike kwa hiyari bila kulazimishwa na waweze kuwahudumia Watanzania wote vizuri kwa viwango vinavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumekubaliana sasa ni win win situation watumishi wa umma waje hapa, Serikali ije hapa, tuzungumze, lakini mwisho wa siku ni ustawi wa Taifa hili kwa ujumla wake. Kwa hiyo naomba niwahakikishie watumishi wa umma nchini, tutapata muda wa kujibu hoja chache kwenye siku hii ya leo, lakini Waheshimiwa Wabunge tumechukua hoja zote tutazijibu kwa maandishi na naomba niwahakikishie wale Wabunge wanaowawakilisha wafanyakazi, lakini Wabunge wote mnaoiwakilisha sekta hii ya utumishi wa umma tutapata pia fursa ya kukutana na vyama vya wafanyakazi, tutaeleza haya yote yaliyoibuka kwenye mkutano huu na kuyatolea majibu kwa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipite kwenye maeneo machache sana kwa kuzingatia muda ulionipa. Naona katika mjadala wa leo kulikuwa na mambo kadhaa ambayo ukiyachukua kiujumla ndio kilikuwa ni kilio kikubwa cha Waheshimiwa Wabunge kwenye mjadala wetu kwenye Wizara yetu, jambo la kwanza lilikuwa ni suala hili la kupanda vyeo na madaraja kwa watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme, pamoja na ushauri na nini tulioupokea lakini tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, tunakumbuka Serikali ya Awamu ya Tano ilifanya kazi yake ya clean data za watumishi hewa, watumishi waliodanganya na vitu vya namna hiyo kwa muda mrefu madaraja hayakupanda lakini Mheshimiwa Rais alipoingia tu madarakani na kwa bajeti hii iliyopita, akaamua kufanya maamuzi ya kuhakikisha fedha zinatolewa na tukawa tumekwisha kupandisha madaraja na vyeo watumishi 190,781 na juzi nimesema kabla ya tarehe 30 Juni watumishi wengine 92,000 lazima wapande madaraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimewasikiliza sana Wabunge na hasa nimewasikiliza pia wale ambao wanawawakilisha wafanyakazi, lakini na wote waliokuwa wanawawakilisha watumishi wa umma wakasema hoja yetu hapa tunalo lile kundi lililoachwa nyuma mwaka 2015, 2016 na 2017. Hawa watumishi tunafanya nao nini, kwa sababu na wao katika kipindi kile ambacho tumeamua Serikali sasa tusafishe data za watumishi wa umma tulikuwa na watumishi takribani 67,244 ambao kuna wengine walikuwa wameshapata barua mkononi za kupanda vyeo, zile barua zikafutwa na upandaji wao wa vyeo ukasimamishwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hao ndio watumishi ambao wengine wanakaribia kustaafu lakini haki yao ya kupanda vyeo haijatekelezwa kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa kada zao na kwa mujibu wa bajeti zilizopangwa. Hapa kwenye jambo hili hatuna mjadala wa kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini hoja inabaki kwa hao watumishi ambao walikuwa stranded baada ya hayo mambo kuwa yametokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge mwaka 2020/2021, tulifanikiwa kuwapandisha watumishi 16,025 tu kati ya hao 67,244. Kwa hiyo tuna watumishi 51,219 ambao hawajui hatma yao, watumishi hawa pia kuna wenzao waliopanda madaraja kwa utaratibu wa kawaida sasa wametofautiana nao madaraja, wenzao wameshaondoka wao wamebaki wana- hang hawajui hatma yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme hivi, tumekubaliana ndani ya Serikali na tunamshukuru sana Kiongozi Mkuu wa Nchi, Mheshimiwa Rais wetu tulichoamua sasa ni lazima tuondoe hayo manung’uniko watumishi hawa tunasema wafanye kazi kwa hiyari, lakini watafanyaje kazi kwa hiyari kama hawajatekelezewa hiyo stahili yao. Mtu anayetaka kula ni lazima afanye nini?

MHE. CECILIA D. PARESSO: Ni lazima aliwe.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Hapana, ni lazima anawe mikono, Mheshimiwa Paresso ni lazima anawe mikono. Kunawa mikono kunathibitisha utayari wake wa kula.

Mheshimiwa Naib Spika, utayari wa kula inaonesha kwamba kuna umakini na sisi Serikali tumesema tutakuwa makini kwenye jambo hili. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tulichokipanga sasa tutafanya nini? Tumeamua kwenye hawa watumishi 92,000 wale ambao wanakaribia kustaafu katika kipindi hiki kifupi ni lazima tutawa-consider kwenye hawa watumishi 92,000 tuweze kuwasawazisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hiyo namba ambayo nimeisema wa watumishi 51,219, tutakwenda kuwatambua wale wanaokaribia kustaafu kabla ya tarehe 30 Juni tuanze na hao kusudi wasije kuumia kwenye mafao yao huko baadaye. Hata hivyo, kwa mwaka ujao wa fedha mmenisikia hapa Mheshimiwa Rais ameidhinisha mafungu ya fedha kwa ajili ya kazi hiyo, naomba niwahakikishie tunajipanga kuwapandisha kwa mseleleko ili tuondoe adha na kadhia hii kubwa ambayo watumishi hawa wameipata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba niwaambie hatutaki matabaka ndani ya Serikali tumeamua sasa hatutaki matabaka tunataka kila mtumishi anapofikia wakati wa kupandishwa daraja, basi iwe inafanyika hivyo, kwa hiyo tunataka tuondoe hizi kadhia ya nyuma hizi Waheshimiwa Wabunge na naomba mumpigie sana Makofi Mheshimiwa Rais na Serikali yake jambo hili tumeamua kulichukua kwa uzito mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wameeleza sana hapa ndani upungufu wa watumishi, ndugu zangu tunakubali tuna upungufu wa watumishi, lakini hatuishi katika kisiwa, upungufu huu wa watumishi umeendelea katika mataifa mengine mbalimbali, lakini sio sababu kwa Serikali yetu, kutokuhakikisha kwamba tunajitahidi kuondokana na tatizo hilo la watumishi. Waheshimiwa Wabunge naomba kwa dhati ya moyo wangu, kwa kweli tumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Hapa wote tumekuwa mashahidi na mmeona tulipanga bajeti ya watumishi 44,096 na tulipofika mwaka 2020/2021, tukawa tumeajiri wachache na ndio maana tumetangaza hizo ajira 32,000 plus ili tuhakikishe kwamba tunakamilisha ahadi ya Serikali ya Watumishi 44,096, tukaanze kupunguza huo upungufu katika maeneo yetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewaambia hapa kipaumbele imebidi twende na hicho ambacho Wabunge wanaowawakilisha wananchi wao, tumejenga madarasa ya UVIKO, tumejenga vituo vya Afya na Zahanati, twende tukaanze kuhakikisha vituo hivyo vyote vinatoa huduma na visikae bila kutoa huduma. Tutakwenda pia kwenye sekta nyingine, kwa mfano sekta ya kilimo, mmeona tumezindua mkakati wa kilimo na Waheshimiwa Wabunge wamesema Bunge hili ni la mkakati wa kilimo, huko pia tutakwenda kuzingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie kwamba, tumejipanga, lakini tunafanyaje, suala la ajira sasa litaendana na kufanya HRO audit ama main power audit, main power survey, tujue humu ndani ya nchi tumejipangaje hawa watumishi ndani ya Taifa letu. Niwape mfano mmoja tulifanya tu utafiti kidogo wakati tunafanya hii main power audit kwenye eneo la majiji makuu na hasa sekta ya uhasibu, tukawauliza haya majini hivi mahitaji yetu ya Wahasibu mnaowahitaji ni wangapi? Wakatuambia wanataka Wahasibu 526. Tukawauliza mnao wangapi wakatuambia waliopo katika kipindi hicho walikuwa 351. Sasa sisi tukaenda kuwasiliana na Wizara ya Fedha, tukawauliza hivi kwa utaratibu wa haya majiji wanahitaji Wahasibu wangapi wakatuambia wanahitaji wahasibu 317 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukagundua kwamba tungewapa hawa 500 na kitu wangekuwa na extra 209 katika maeneo yao ya kazi. Wakishakuwa na extra 209 ndio tutabaki tunalaumu kwamba Wahasibu hawatoshi kumbe kuna kada fulani watumishi wapo wengi hawazingatii ikama iliyokuwa inatakiwa, kama walitakiwa wawili hapa tungeweza kujikuta kwamba wapo watano ama sita, kwa hiyo basi mtawanyiko na msambazo wa watumishi hauendani na mahitaji katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, wametuambia, huko vijijini walimu wachache, lakini nendeni kwenye shule za mjini, walimu wapo wengi. Hata kwenye kada nyingine tofauti tofauti, naomba mtuunge mkono tunafanya hii HR Audit vizuri, survey inafanyika vizuri, mwisho wa siku tunataka sasa kuwa na majibu halisi ya kuona nini kifanyike kusudi hiki kidogo tulichonacho kiweze kumhudumia kila Mtanzania katika eneo alilopo na kwa ufanisi wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda eneo lingine ni recategorization limesemwa sana hapa. Recategorization tunaitazama katika sura tatu zifuatazo: ya kwanza, mtu anaweza kufanyiwa recategorization kama mwajiri anaona katika sekta yake kuna uhitaji wa mtumishi; labda kwenye Halmashauri wanahitaji Afisa Manunuzi na hayupo, lakini kuna Mwalimu anayeweza kwenda kusomea Uafisa Manunuzi na akaja kusaidia. Mwajiri atamwandikia kumwomba, naye akikukubali na akaenda shule, akirudi, mshahara wake itabidi aendelee nao kwa sababu mwajiri alikuwa na hilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba waajiri wote kama watumishi hao wameangukia kwenye kifungu hiki cha kwanza, ni lazima wafanyiwe recategorization na wawekwe kwenye ikama na ni lazima haki itendeke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni mtumishi kuomba kujiendeleza kwa kuruhusiwa kwa maandishi na mwajiri wake, naye mwenyewe kuomba kwa maandishi, lakini kwenye kada ile ile ya kwake. Kama ni Mwalimu ana Degree, anaenda kufanya Masters, kama ana Diploma anaenda kufanya Degree, kama ana Masters, anaenda kufanya Ph.D katika kada yake ile ile, huyo naye akirudi ni lazima afanyiwe recategorization na mshahara wake uendane na madaraja yatakoendana na kisomo chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watumishi waendeshaji kama ma-PS, madereva na watu wa namna hiyo; hawa sasa wakienda kusoma na kurudi, wana kibali cha kufanyiwa recategorization ili mradi tu walipata kibali cha kwenda kufanya hivyo. Sasa shida inakuja, kwa watumishi ambao wamesoma fani tofauti, wanaenda kusomea kada na fani nyingine tofauti halafu wanatakiwa wafanyiwe recategorization, sasa hapo ndipo pana shida ndugu zangu…

NAIBU SPIKA: Dakika moja, malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba waajiri wote hawahakikishe kwamba wanaposhughulikia masuala ya recategorization, wazingatie miongozo na taratibu tulizozitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna suala la watumishi wa Darasa la Saba, kama utanipa muda wa dakika mbili tu nadhani hili lilikuwa limezungumzwa sana.

NAIBU SPIKA: Dakika moja na nusu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Haya, dakika moja na nusu naipokea kwa unyenyekevu mkubwa. Hadi sasa Watumishi wa Darasa la Saba walioondolewa kimakosa 4,380 wamesharejeshwa kwenye utumishi. Kwa nini wamerejeshwa? Hawa ni wale ambao waliajiriwa kabla ya tarehe 20 Mei, 2004. Kwa hiyo, sifa yao ya ajira ilikuwa ni darasa la saba.

Kwa hiyo, kama waliondolewa kimakosa na pia kama hawakughushi, kwa sababu wengine waligushi vyeti hapo katikati na wakajiona kwamba ni form four. Sasa kama walighushi, hao hatuwahitaji, lakini kama hawakughushi, wanatakiwa warudishwe. Huo ndiyo utaratibu na mpaka sasa hawa 4,380 wamesharudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watumishi wengine ambao waliajiriwa baada ya tarehe 20 Mei, 2004, baadhi ya waajiri hawakuzingatia utaratibu, wakawaajiri tena darasa la saba badala ya kigezo cha form four; na hao nao waliondolewa. Sasa tulisema hivi, hao walioondolewa wanatakiwa kurudi kazini, lakini kama wametekeleza kile kigezo cha kujiendeleza. Kwa hiyo, tuliwaagiza wajiendeleze na watumishi 954 wamejiendeleza na wamesharudi kazini na wapo kazini mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba wale ambao wanataka kurudi na wamejiendeleza, waendelee kuwasiliana na Ofisi zetu. Kama hawakujiendeleza, kwa sababu hicho ndiyo kilikuwa kigezo, waajiri tunawaagiza waendelee kufuata maelekezo na nyaraka tulizowapelekea wazisome ili waweze kutenda haki kwa hao watumishi. Hata hivyo, hawa nao tutawarudisha kazini na watapata haki zao kama nao hawakughushi vyeti. Kuna wengine walighushi vyeti pamoja na kwamba waliajiriwa kwa sifa hiyo, lakini wakaghushi vyeti. Sasa kama walikuwa wameghushi vyeti, hilo nalo hatutaweza kulizingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maelezo zaidi tutaendelea kuyatoa na ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ya muda, itatupasa tufanye Press maalum ya kuyaeleza haya mambo yote kwa ukubwa na upana wake kadri inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri toa hoja.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa huu muda, tulikuwa na mambo mengi ya kueleza, lakini kwa sababu ya muda, basi niishie hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.