Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya, pili ninakushukuru sana kwa namna ambavyo unaendesha vikao nakupongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na mdogo wangu Mheshimiwa Deo Ndejembi, kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kuongoza Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuliongoza Taifa letu, pia nitumie nafasi hii kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kutuwezesha kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, bajeti ambayo tunaenda kuitekeleza kwa nguvu na jitihada kubwa tukishirikiana na nyinyi. Bajeti ya Utumishi ni bajeti ambayo inasomana kwa karibu sana na bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa hiyo nashukuru kupata fursa hii ili niweze ku-clarify baadhi ya mambo ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeyajadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la ajira. Katika hili ninamshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutupa kibali cha kuajiri Walimu 9,800, kwenye upande wa afya kuajiri Wauguzi 7,612. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutupa kibali hiki, tunaenda sasa kuajiri vijana wetu ambao wamekuwa wakisubiri ajira kwa muda mrefu. Kwa hiyo, watapata fursa lakini pia tunaenda kupunguza uhitaji wa mahitaji ya Walimu na Wauguzi katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili Waheshimiwa Wabunge ningependa niwaondoe wasiwasi, mfumo wa kuomba ajira wa online kwa siku ya mwanzo kwa sababu wanaoomba ni wengi, kumekuwa kuna changamoto ya mambo ya mtandao lakini timu yangu inafanyakazi kwa jitihada kubwa kuhakikisha wanoomba huduma ya kuomba kupitia mtandao inaenda vizuri, nami baada ya kutoka hapa naenda kwenye eneo ambalo wanafanyia kazi kujiridhisha marekebisho haya yafanyike ili wale wanaoomba hizi ajira waweze kuomba kwa urahisi sana kupitia mtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa ajira Waheshimiwa Wabunge utaratibu uliopo na application ya mtandaoni imezingatia uhitaji wa ajira kwenye maeneo. Kama ni upande wa Wauguzi, kama ni upande wa Walimu imeangalia mahitaji ya nchi nzima, kwa hiyo wanapoomba inapeleka pale ambapo pana uhitaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ningependa mtuamini kwamba utaratibu uliopo unaenda kukidhi maeneo ambayo yana mahitaji critical, lakini hoja ambayo tumeipata hapa ya kwamba ajira izingatie maeneo kwa maana ya Wilaya, Majimbo ni wazo lakini naomba mtupe nafasi upande wa Serikali tulichukue tukaliangalie, tuangalie namna ambavyo linaweza likatekelezeka au kama utaratibu uliopo unaweza ukaboreshwa ili kuweza kuzingatia hilo, hilo pia tutaliangalia Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa machinga ningependa nitumie nafasi hii kutoa maelezo kwa ufupi sana, nimpongeze Mheshimiwa Kaka yangu Mheshimiwa Gwajima amelielezea vizuri, Mheshimiwa Rais wetu maelekezo aliyoyatoa kwa wamachinga ni kuwawekea mazingira rafiki ya kufanyia kazi na kuwapanga kwa utaratibu ambao hatutumii msuli, kwa utaratibu ambao hatuchukui mali zao na kuzihodhi, kwa utaratibu ambao unajenga ustawi wa machinga huyu kuweza kufanya kazi kujipatia riziki, ku-support familia zao na kwa pamoja kama machinga waweze kusaidia katika kujenga uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni kundi ambalo tunalitambua na kulithamini kama Serikali. Serikali ya Awamu ya Sita kama nilivyoeleza kwenye bajeti yangu, pamoja na Bilioni Tano ambazo Mheshimiwa Rais ametupatia kwenda kujenga miundombinu hii rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Dodoma kama nilivyoeleza tunajenga Machinga Open Complex, Waheshimiwa Wabunge baadhi yenu mmetembelea eneo hili, kwa dhamira njema ya Mheshimiwa Rais wetu bilioni tano ambazo alizitoa tumekuja kujenga soko hili kama mfano lakini tunataka tuende kwenye Majiji, Manispaa na baadae hata kwenye Halmashauri za Mji ambazo zina Machinga wengi ili tuweze kujenga masoko ambayo ni rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningependa kutumia nafasi hii kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa, maelekezo haya yazingatiwe na nimeshaelekeza Wakuu wa Mikoa kwenye masuala ambayo yanahisia kama machinga, bodaboda, mama lishe, tufanye consultations kati ya Mikoa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili operation ambazo zitakuwa zinafanyika tuwe tunauelewa wa pamoja ili kuhakikisha usimamizi wake wa operation hizi uweze kuwa ni rafiki na kwa matarajio ambayo Serikali inataka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali dhamira yake ni kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya vijana wetu machinga akina Mama na Vijana ambao wanategemea sekta hii na tutaendelea kufanya sekta hii izidi kuwa Rafiki, izidi kuwa na matumaini kwa watu ambao wanaitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunaendelea kufanya kila aina ya jitihada kujenga nyumba za watumishi, kwenye bajeti mmeona kwa mara ya kwanza bajeti ambayo tumeitenga kwa ajili ya kujenga nyumba za Walimu hasa hasa Walimu ambao wanaishi maeneo ya mbali. Jambo hili tumelizingatia kwenye bajeti na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kila mwaka wa fedha tutakuwa tunatenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za watumishi ili kupunguza uhitaji mkubwa wa nyumba za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kengele ya kwanza muda bado ninao basi. Kuhusu upungufu wa watumishi nimeshasema Mheshimiwa Rais tunamshukuru ametupatia kibali kwa ajili ya kuajiri Walimu na Wauguzi

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upandishaji madaraja, katika hoja ambazo zimetoka kwa Waheshimiwa Wabunge tutaleta majibu kwa kila hoja, kwa kila Mbunge aliyechangia ikiwemo takwimu, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, kwa kipindi ambacho amekaa madarakani mwaka mmoja amepandisha madaraja kwenye Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa, pia kwenye arrears tumekuwa tukishirikiana vizuri na Ofisi ya Rais, Utumishi kukusanya arrears na kuwapelekea Hazina ili kuhakikisha malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wetu yanalipwa. Kwa hiyo, jambo hili tutaendelea kushirikiana ili tuweze kuhakikisha wenye haki ya kupandishwa madaraja lakini pia wenye haki ya kulipwa malimbikizo wanapata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeshakubaliana na Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, baada ya kuhitimisha hotuba yake na nitumie nafasi hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge tumpitishie bajeti ili akaweze kutekeleza haya mengi mazuri ambayo yamesheheni katika bajeti yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubaliana baada ya leo Wizara mbili zitakaa, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utumishi tujipange vizuri kwa mambo ambayo mmetuelekeza humu.

Tujipange vizuri katika kutekeleza bajeti zetu mbili kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge pamoja na kuchangia maeneo ambayo yamehusu Ofisi ya Rais, TAMISEMI niwahakikishie Mheshimiwa Dada Jenista ni role model wa Wabunge wengi sana humu na tunajivunia yuko hapo. Kwa hiyo, kwenye mambo ambayo mmezungumza hapa nasi kwa vile mlituunga mkono, mkapitisha bajeti yetu kwa kishindo, muamini Wizara hizi mbili kwa kweli tuna ushirikiano wa karibu, changamoto ambazo mmezitaja tutashirikiana katika kuhakikisha zinatekelezwa kwa manufaa ya wananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala la posho za Watendaji wa Kata. Nitumie nafasi hii kuwaelekeza Wakurugenzi wote nchini

MWENYEKITI: Hilo nakuongezea dakika moja liongee vizuri hilo la Watendaji wa Kata.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Serikali ilitoa posho ya madaraka kwa Watendaji wa Kata 100,000 kwa mwezi na tukaelekeza Wakurugenzi kuhakikisha kila mwezi Mtendaji wa Kata anapata hii 100,000 iweze kumsaidia katika majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Halmashauri, Watendaji wa Kata wamekuwa wakifuatilia kana kwamba hii ni hisani. Kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwaelekeza Wakurugenzi kote nchini kuhakikisha kila mwisho wa mwezi Mtendaji wa Kata anapata hii 100,000 akiwa kwenye Kata yake, kuondokana na adha ya kutoka kwenye Kata kwenda kwenye Halmashauri kudai hii posho kana kwamba ni hisani. Hii siyo hisani ni haki ya Watendaji wetu kwa hiyo, Wakurugenzi zingatieni hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili kwenye bajeti ijayo tunatambua kazi nzuri ambayo Watendaji wa Kata wanafanya, tutatenga bajeti kwa ajili ya kuwapa usafiri, katika hili nitumie nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan tunaona hata Wizara za kisekta Mheshimiwa Rais ametoa vibali kwa ajili ya kuhakikisha Maafisa Kilimo kwa upande wa kilimo wanapata usafiri, Maafisa Ugani na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye bajeti itakayokuja ya 2023/2024 tutahakikisha Watendaji wa Kata na wenyewe tunawapa kipaumbele katika kuhakikisha wanapata usafiri ili waendelee kufanya kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kuisimamia Serikali ngazi za Kata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)