Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kumpongeza sana Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya kwa kuongeza ajira, kupandisha vyeo kwa watumishi nchini. Jambo hili linakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa cha upungufu wa ajira na kuongeza ufanisi katika kada mbalimbali. Ninapo kwenda kumpongeza Mheshimiwa Rais pia niwapongeze sana watendaji walioko kwenye Wizara hii wakiongozwa na Waziri Mheshimiwa Jenista Mhagama, nawapongeza kwa kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa napenda kutoa ushauri wangu katika mambo yafuatayo; kwanza tunapo kwenda kuajiri watumishi hasa kada ya elimu na afya ni lazima kuzingatia uhitaji, jiografia na taaluma ya wahitimu kwani yapo maeneo watumishi wapya huenda kwenye ajira mpya kwa lengo la kuchukua check number tu na baadaye kuhamia maeneo ya mjini. Mfano Halmashauri ya Liwale tumekuwa tukipokea watumishi wengi sana lakini baada ya muda mfupi uhaba unajirudia kutokana na watumishi wengi kuhama. Lakini tunao vijana wanaojitolea kwenye shule na zahanati zetu kwa muda mrefu na wanapoomba ajira hawapati pamoja na kupata barua kutoka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri juu ya miradi ya uwekezaji inaofanywa na Mifuko ya Jamii. Ni lazima miradi hii ifanyiwe stadi za muda mrefu na makini kuepusha kupoteza fedha nyingi kwenye miradi isiyokuwa na tija. Vilevile miradi hiyo isimamiwe kwa karibu ili kupata thamani ya fedha zilizotumika. Mfano miradi ya NSSF iliyoko kule Kigamboni Dar es Salaam, miradi ambayo imetekelezwa si tu chini ya kiwango bali pia ni miradi isiyokuwa na tija, hivyo kupoteza fedha za taasisi husika.

Kuhusu Taasisi ya TAKUKURU kwa ujumla wake inafanya kazi vizuri pamoja na kuwa wapo watumishi wasio waaminifu bado wapo kwenye taasisi hiyo. Naiomba Serikali kufanya vetting ya kutosha juu ya uzalendo na uaminifu wao. Kuwepo kwa vitendo au viashiria vya rushwa kwenye taasisi yenye dhamana ya kupiga vita rushwa ni jambo baya zaidi, hivyo naomba umakini uongezeke ili kupunguza malalamiko katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TASAF; taasisi hii lengo lake ni kuboresha au kusaidia kuinua vipato vya kaya au jamii. Je, hadi sasa Serikali imeshafanya utafiti wa kiwango gani kujua hadi sasa ni kaya ngapi zilizonufaika na mpango huu na tayari zimeshatoka kwenye kaya maskini na kuingia kwenye kaya zenye kipato cha kati. Lakini pia hapa ningeshauri wanufaika hawa wangepatiwa vifaa au vitendea kazi badala ya fedha cash. Lakini ikibidi kupewa fedha cash basi zitoke kwa wakati na kwa usimamizi wenye weledi na umakini mkubwa, kwani yako malalamiko ya fedha hizi kuingia kwenye mikono haramu.