Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hii muhimu ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Wizara hii lakini pia kwa Mheshimiwa Rais kwamba baadhi ya mambo tuliyoyaomba mwaka jana kwa upande wa Jimbo langu yameanza kutekelezwa, hasa ujenzi wa Ofisi ya TAKUKURU ambao walikuwa wanakaa kwenye godauni, sasa umeanza tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kushukuru, ni kwamba tumeshawasilisha sasa ombi letu la ukarabati wa zahanati kupitia Mfuko wa TASAF. Zahanati ya Kijiji cha Mkalanga na Zahanati ya Kijiji cha Winome ambazo wananchi ndio wameibua miradi hii ili zile ziweze kukarabatiwa na kukamilika kupitia Mfuko wa TASAF. Naomba kupitia kiti chako basi Wizara hii iweze kuzifanyia kazi angalau kwenye bajeti hii ili zahanati hizi mbili ziweze kukarabatiwa na kwa umahiri wa Mawaziri pamoja na Watendaji wa Wizara hii, nina hakika ombi hili litapokelewa kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumzia mambo machache, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, kwa hiyo, mambo mengi kwa kweli tumekuwa tukishauri kwenye Kamati. Jambo la kwanza ambalo tumekuwa tukiendelea kushauri, nami ningependa kulisisitiza hapa ni kuhusu watumishi wanaojitolea kwenye sehemu mbalimbali. Watumishi hawa wanajitolea kwa muda mrefu, wengine miaka sita wengine nane wengine saba, hasa walimu na wale wa kwenye sekta ya afya, na wengine wanajitolea kwenye mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hakuna mfumo maalum wa kujitolea, japo mahitaji ya kujitolea yapo, tulitoa ushauri utengenezwe mfumo maalum unaowatambua watu wanaojitolea ili inapofika wakati wa kuajiri tuwe na hiyo database. Kwa sababu, siku hizi mtu anakwenda tu anaongea na Mkuu wa Shule na anaanza kujitolea, au anaenda Zahanati, anaanza kujitolea. Hii haitoi fursa sawa. Kwa sababu, mtoto wa masikini anaweza akaenda pale akakataliwa, lakini mtoto wa Mtendaji wa Kata au Mwenyekiti wa Kijiji, akapata fursa kwa mamlaka au mtoto wa mtu mwingine mwenye mamlaka. Kukiwa na mfumo mzuri wa kujitolea ambapo tunajua mahitaji yapo, utasaidia kufanya acceleration wakati wa kuajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hii haipo, naomba iangaliwe namna itakayokuwa fair, ya kuwafanya wale waliojitolea muda mrefu kwenye hizi ajira waweze kupata kipaumbele. Jambo la pili ambalo ningependa kulisema na tumelizungumza pia hata kwenye Kamati, ni suala zima la mafunzo. Utakuta kwenye maeneo mengi wanaohudhuria mafunzo ni viongozi katika ngazi za Wilaya, labda wakuu wa Idara na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Watendaji wa Kata, na kwa mujibu wa taratibu na Kanuni za muundo, wao ndio kama viongozi katika Kata; na wale watendaji wengine awe Afisa Kilimo au Afisa Mifugo, wanaripoti kwao. Jambo la kwanza, pamoja na kwamba vitendea kazi hawapewi, unakuta wa Mifugo wamewapa, labda wa elimu wamepewa pikipiki, yeye bosi wao hana hata baiskeli. Hilo linaweza likawa linaangukia TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mafunzo sasa. Tulishauri na ninaendelea kushauri kwamba mtu hawezi kutoka Chuoni au huko aliko akaanza kufanya kazi zile bila kupata mafunzo maalum. Tulishauri Chuo cha Utumishi wa Umma kiweze kutoa hayo mafunzo ili watumishi hawa wa ngazi ya Kata na hatimaye wa ngazi za Vijiji waweze kuwa na umahiri wa kutenda kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Watendaji wa Kata kwa kuwa tumesema ni Wakurugenzi katika ngazi ya Kata, waweze kujua wajibu wao wa Ukurugenzi katika ngazi ya Kata; wanawajibika kufanya nini? Kwa sababu, wakati huo utakuta kwenye Halmashauri kuna Masijala na nini; nenda kwenye ngazi ya Kata, hata Folio kwenye file, huyu mtu hajawahi kufundisha na haelewi. Kwa hiyo, haya ni mambo ya muhimu sana ambayo tungependa yatiliwe mkazo kwenye bajeti, hasa kwa ajili ya Chuo cha Utumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba, hili ni wasilisho la ombi langu ni kuhusu Watumishi Housing. Sasa hivi ujenzi wa nyumba nyingi unaendelea mijini. Nitaje mfano kama Kilolo; Mji wa Kilolo ni Mji unaokua. Watumishi wengi pale kila siku tunafukuzana nao kwa sababu wanataka kuishi Iringa Mjini na ukiangalia ni kwa sababu pale Kilolo hakuna nyumba hata za kuweza wao kupanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza, hizi Wilaya ambazo zimejengwa kwenye maeneo ambayo hayakuwa Miji, zipewe kipaumbele kwa kujengewa nyumba na Watumishi Housing ili miji ile kwanza iweze kukua, na pia kuleta tija kwamba watumishi watakaa pale, kwa sababu, vinginevyo utakuwa unawabana watumishi kukaa kwenye sehemu ile, lakini sasa hakuna makazi ambayo wanaweza kukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Watumishi Housing i-plan vizuri ili tuweze kuwa na makazi ya kutosha hasa kwenye eneo hilo nililolitaja la pale Wilaya ya Kilolo ambapo Mji ule ni mdogo na unahitaji sana huduma hiyo. Jambo la mwisho ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu upungufu wa watumishi. Wilaya ya Kilolo kama zilivyo Wilaya nyingi za vijijini ina upungufu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeweza kusoma takwimu nyingi, lakini kwa sababu ya muda niongelee kwenye sekta ya afya. Ili angalau tuweze ku-operate, Zahanati ambazo zimemalizika kujengwa na Vituo vya Afya tulivyomaliza kujenga, tunahitaji watumishi 39. Kwa hiyo, nikitaja yale maelfu, najua huenda yasiwe na tija sana. Hawa 39 watatusaidia angalau kwa kuanzia na hawa wanaweza kupelekwa kwenye Vituo ambavyo, ni kama Zahanati ambazo hazijaanza kabisa kama Zahanati ya Mbawi, Masege, Lugalo, Ilole, Mlafu, Ibofwe, Ikuka na Idunda Vituo vya Afya vya Ng’uluwe na Nyalumbu ambavyo hivyo nilivyovitaja, vimekamilika, lakini sasa hatuwezi kuanza kufanya chochote kwa sababu hakuna watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kwa sababu najua kuna ajira hivi karibuni, basi ninaomba kwamba yale maombi yetu yatakapoletwa ieleweke kwamba hizi ninazozitaja zinahitaji kwa kiwango kikubwa sana attention ya karibu na kama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)