Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba pia niseme kwanza naunga mkono hoja. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI kwa hiyo sehemu kubwa ya mijadala hii tumeijadili na tumemshauri Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kama walivyosema wenzangu, naomba pia nitumie nafasi kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya hasa kwa juhudi kubwa anazozifanya sasa hivi za kuitangaza Tanzania huko nje. Niliwahi kusema kwenye Bunge hili kwamba tuliwahi kusafiri na Kamati ya Bunge kwenda mji mmoja China, tulipofika hawaijui kabisa Tanzania na wakawa wanashangaa ukiwaambia Tanzania mpaka wa-google waangalie Tanzania iko wapi. Kwa hiyo kwa Mheshimiwa Rais kwenda kwenye vyombo vya kimataifa sehemu kubwa ya watu wasioijua Tanzania wataanza kuifahamu Tanzania, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza suala moja kuhusu umuhimu, kwanza kuipongeza Serikali kuhusu ajira mpya zilizotangazwa, lakini umuhimu wa uwepo wa kanzidata kama ilivyozungumzwa na mchangiaji mmoja jana. Tumeshauri sana jambo hili kwenye Kamati, nataka nitoe mfano kule kwangu kuna Kijiji kinaitwa Mgusu, ili mwananchi wa Mgusu aweze kuhudhuria interview moja Dar es Salaam au Dodoma anahitahi karibu siku saba. Moja atatoka Mgusu kuja kulala Geita na pale atalipa shilingi 20,000, atalala guest shilingi 20,000, atatoa nauli kwenda Dar es Salaam shilingi 50,000, akifika Dar es Salaam siku mbili kabla atakaa guest atalipa shilingi 50,000, 50,000. Kwa hiyo mpaka siku anafanya interview ameshatumia 300,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtanzania huyu atafanya interview, ataambiwa hakuchaguliwa atarudi. Kwa hiyo mwananchi, huyu Mtanzania ambaye anatafuta kazi anahitaji takribani 400,000 mpaka 500,000 katika kila interview moja inayotangazwa na Serikali. Ili aweze kupata kazi au asipate kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Lusinde atahudhuria interview zisizopungua 10. Wapo watendaji, Watendaji tu wa Mitaa wameenda mikoa karibu 20 kutafuta utendaji wa mtaa na kila akienda jina lake halimo. Vile vile zinatangwa ajira hapa TRA wanatakiwa 1,000 wanaomba 10,000 na wote 10,000 wanaitwa, yakisomwa majina hayumo. Inatangazwa Uhamiaji, wanatangaza nafasi 400, wanaomba na kuitwa 8,000, yakisomwa majina hayumo. Matokeo yake huyu mtu anayekuja kwenye interview Uhamiaji amehudhuria interview karibu 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi nchi hii haiwezekani mimi niliyefanya leo interview nikabaki kwenye database kwa miaka miwili au mwaka mmoja. Jibu la Wizara ni kwamba wanafanya kwa miezi sita, miezi sita haitoshi Mheshimiwa Waziri anao mfano, tumefanya interview mwezi wa 11 za TRA juzi wametangaza zingine, miezi minne, lakini wameita watu wote hawajaita ambao walifaulu. Ukiangalia kwenye orodha walikuwa wanataka watu 400, walifaulu zaidi ya watu 2,000. Matokeo yake ni nini? Kila unapoita zinazokwenda kuajiriwa ni zile fresh mentals. Kwa sababu mtu akitoka chuoni anaweza kujibu maswali ya interview vizuri kuliko mtu aliyemaliza mwaka juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe mfano, mimi ni Mhasibu na wengi humu ni professionals, tukichukuliwa leo kwenda kwenye usaili, kozi uliyosomea unahitaji mwezi kujiandaa, lakini hutajibu sawa na mwanafunzi aliyetoka chuoni jana. Matokeo yake ni nini? Aliyemaliza chuo mwaka 2017, 2018, 2019, 2020 anachanganywa kikapu kimoja na wa mwaka huu, anayefaulu ni wa mwaka huu, wa mwaka jana anabaki mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niiombe Serikali kwa sababu nina uhakika hatuna first in, first out, wanaohudhuria kwenye usaili wakifaulu wawekwe kwenye kumbukumbu tuepuke kuwa na mtu anastaafu kabla ya kufanya kazi, amesema hapa Mheshimiwa Lusinde. Hii inatokeaje huko nje, kwanza tuna shida moja tumeweka carders nyingi kwenye Universities ambapo sina uhakika kama kuna research imefanyika kuangalia ni kozi gani ni muhimu. Mwingine kasoma sijui public sijui nini, mwingine sijui public nini, kwa hiyo huko mtaani watu wana vyeti vingi, hakuna ajira, hakuna kazi, kila akisoma tangazo la ajira kozi aliyosomea haimo. Waliojaa mtaani huko Procurement, sijui Uhasibu, sijui nini, public sijui, lakini akisoma ajira hayumo, matokeo yake wanaotangazwa hayumo, wanaoajiriwa hayumo, miaka 45. Ndiyo maana mwaka jana, mwaka juzi tulijikuta kwenye uchaguzi wa CCM Jimbo moja wamechukua fomu watu 60 asilimia 80 walikuwa ni graduate hawajapata kazi. Ushauri wangu hapa kwa Mheshimiwa Waziri, nafahamu alilichukua jambo hili, tuwe na hii kanzidata, mtu akihudhuria interview mara moja tu-communicate, tumuulize bado una interest na kazi hii. Kama kazi hiyo hana interest nayo hatuna sababu ya kumsafirisha tena kumleta Dodoma, inakuwa ni kero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wote unaowaona wanakuja Dodoma kufanya interview Wabunge tunachangia nauli. Sasa nataka tujiulize, una watu 20 wanakuja hapa, wakifika wanakwambia sisi tumemaliza interview hatukuchaguliwa wote, tunaomba nauli ya kurudi nyumbani, unatoa wapi pesa hiyo? Naomba jambo hili lichukuliwe serious sana, lakini tufanye utafiti kuangalia soko la ajira nchini limekaaje ni ajira zipi ambazo tuhamasishe watu wasome. Watu wanasoma wanamaliza hawana pa kwenda, wanadaiwa mikopo na tumetunga Sheria hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili, tumeiona PCCB, ipo kwenye Kamati yetu, tunawapongeza kwa kazi nzuri wanazofanya. Nataka kujiwekeza kwenye jambo moja tu, wakati wa uchaguzi PCCB ni very active na inakuwa very, very active kwa Wabunge walioko madarakani. Sasa huwezi kumaliza rushwa kwa kumvizia mtu mmoja unayemjua peke yake. Nilishuhudia uchaguzi ulioisha kila unapokwenda wewe upo monitored lakini mko 40, wale wengine hakuna anayewatafuta. Sasa tuwe na utaratibu, tuna vyombo vingi, wagombea wanajulikana, kama wapo watu wanataka, kwa mfano ukiangalia kuna nchi ambazo wagombea wanajulikana, waanze kufuatiliwa mapema. Ukimsubiri mtu siku ya uchaguzi alishamaliza kampeni, utafanya kazi ya zimamoto na utajikuta siku moja umepata Viongozi wote hawana sifa kwa sababu wameshinda kwa rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)