Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii ambayo ni Wizara muhimu sana katika ustawi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nimpongeze Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya ndani ya Taifa letu na nje ya mipaka yake. Leo hii dunia yote inatambua kwamba Rais wa Tanzania yupo na anautangaza utalii wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, niipongeze Wizara ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ambayo inaongozwa na Dada yetu mpendwa Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kweli anafanyakazi nzuri, kazi hii anayoifanya si kwamba ameanzia hapa bali ameanzia kwenye maeneo yote ambayo alikabidhiwa dhamana ya kushughulikia shughuli hizo. Hongera sana Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama, endelea kufanya hivyo Taifa linakutegema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo napenda nichangie kwenye eneo la watumishi tu. Eneo hili ni eneo muhimu. Kwanza, naungana na wenzangu wote, Waheshimiwa wote ambao wamechangia eneo hili kwa kuona na kutambua kwamba mtumishi ana haki yake ya msingi amefanya kazi kwa wakati wake, na anapostaafu anatakiwa atambuliwe kwamba alichangia Taifa hili katika eneo moja au jingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo leo hii kwanza mimi namshukuru Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa nini namshukuru kwa sababu yeye aliniteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vile viti 10. Kutokana na hilo leo hii naweza kusimama hapa na kuzieleza changamoto, hapa nataka nieleze wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wastaafu hawa wapo katika eneo maalum ambao ni Wenza wa Viongozi. Wake wa Marais, Wake wa Mawaziri Wakuu na wake wa Makamu wa Rais. Ninayaeleza haya kwa sababu na mimi nataka niseme nilikuwa ni Mke wa Rais wa Awamu wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu na suala la kustaafu mara Rais anapochaguliwa ili aweze kushika kijiti na kuongoza Taifa. Mke wa Rais anatakiwa astaafu asiendelee kufanyakazi, hatakaa kana kwamba alikuwa ni mtumishi wa umma, unatakiwa kuanzia wakati ule ustaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mfano mmojawapo nilitakiwa niache kazi yangu ya Ualimu niendelee na shughuli nyingine. Sasa kwa muktadha huu kuacha kazi siyo jambo baya lakini kinachotakiwa kifanyike ajue huyu Mke wa Rais au Mke wa Makamu au Mke wa Waziri Mkuu stahiki zake zipo wapi? Stahiki zake ni nini mara baada ya kustaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama akistaafu ni lazima huyu Mke wa Rais basi apate mafao yake yale mapema au haraka kadri inavyowezekana. Sasa itokee Mke Rais huyu, kama huwiwi ina maana kwamba kuanzia siku ile inabidi ukae nyumbani uendelee na shughuli za nyumbani wakati wewe ulikuwa aidha mtalaam kwenye eneo husika, kwa maana hiyo utaalam wako wote ule unatoweka na inakuwa basi, ukiwiwa sana ndiyo unaweza ukasema hebu nianzishe NGO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukianzisha NGO ile hakuna mtu anayeku-support, ni wewe mwenyewe binafsi uhangaike kona zote, kuhakikisha kwamba unapata rasilimali ili uweze kuendesha ile NGO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu au ushauri wangu, tengenezeni utaratibu maalum wa kisheria kwamba, huyu Mke wa Rais mara au mwenza kwa mfano leo si mke wa Rais leo ni mwenza Mama leo ndiyo Rais, Baba ndiyo mwenza wake huyu Baba ina maana anaachishwa kazi leo na akiachishwa kazi anafanya nini? Tengenezeni yale mazingira mazuri ili tunapomaliza ule muda tujue tuna kitu gani ambacho tunatakiwa tukifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, Utawala Bora ni imani yangu kwamba, tutatengeneza utaratibu au sheria inayomuhusu mke wa Rais au wenza nini baada ya hapo kiendelee kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo muhimu sana siyo kwangu mimi bali ni kwa vizazi vijavyo na vijavyo kujua stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ahsante sana Mheshimiwa Mama Jenista Mhagama kwa kazi kubwa na nzuri unayoifanya Mwenyezi Mungu akubariki, Mwenyezi Mungu ambariki Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)