Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Nianze mchango wangu katika kipengele cha kwanza kuhusiana na watumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba watumishi wa umma ndiyo injini ya nchi. Kama ambavyo tunatambua umuhimu wa injini katika magari yetu vivyo hivyo watumishi wa umma ni muhimu katika nchi hii kwa sababu wao ndiyo wapanga mambo yote na watekelezaji wa mambo yote hapa nchini na bila wao hakuna mafanikio yoyote ambayo sisi wanasiasa kwa namna moja au nyingine tunaweza kujivunia nayo. Hivyo basi, hawa watumishi wa umma wanatakiwa kwa umuhimu huo kujengewa mazingira yote muhimu na rafiki ya kuhakikisha kwamba wanapofanya kazi zao wanafanya kazi katika mazingira ambayo yanaleta matokeo tunayotarajia sisi wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni pamoja na watumishi wa umma wote ambao wana-qualify kupandishwa madaraja na vyeo Serikali haina budi kuhakikisha watumishi hawa kwa wakati madaraja yao na vyeo vyao vinapandishwa. Tumesikia kupitia taarifa ya Waziri amesema kati ya Julai 2021 na Machi 2022 watumishi laki 190,781 walipandishwa vyeo na madaraja, lakini hajatuambia kati ya mahitaji mangapi. Huwezi tu kusema umepandisha hawa lakini hamjatuambia ni wangapi wana-qualify kupandishwa madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vyema sana Waziri ukatuambia wanao-qualify ni wangapi na kwa awamu hii mmepandisha wangapi. Kwa hiyo tusijifiche kwa kutoa hizi takwimu tu zikaonekana ni nyingi kumbe uhitaji ni mkubwa sana huko kwa watumishi ambao wanapaswa kupandishwa vyeo na madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, uhaba wa watumishi wa umma, kama ambavyo nimeanza kwa kuelezea umuhimu kama kuna uhaba wa watumishi wa umma automatic ufanisi wa mambo katika nchi hii hauwezi kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema, mahitaji halisi ya watumishi wa umma hapa nchini ni milioni 1,232,089 lakini waliopo mpaka sasa takwimu zinaonyesha ni mia 679,995 kuna upungufu wa laki 558,134 sasa tuna upungufu wa laki 558 plus lakini ajira zilizotangazwa juzi ni 32,000 katika kada zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuone tu kwamba bado tuna uhitaji mkubwa sana wa watumishi wa umma. Swali linakuja hivi ni kwanini ni kwamba labda hatuna watumishi ambao ni qualified? Lakini si kweli. Kwa mujibu wa taarifa ya TCU wanaohitimu Vyuo Vikuu, nina takwimu hapa za miaka mitatu; 2018, hiyo ni Vyuo Vikuu tu sijachukuwa takwimu za vyuo vya kati, Vyuo Vikuu wanamaliza na kuingia kwenye soko la ajira ni 49,154 kwa mwaka 2018, 2019 ni 51,000, 2020 elfu ni 48,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, kama tuna upungufu ukitaka kusema hatuna wanao-qualify sio kweli kwa sababu tafiti za TCU itakuonesha ndivyo sivyo; na maana yake kwa miaka mitatu tunazalisha wahitimu laki 148,853. Kati ya hao laki 148,853 wenye degree ya kwanza ndio wengi zaidi ambapo kwa mwaka 2020 tu tunatoa walio na degree ya kwanza 34,168. Katika ya hao 1,468 ambao wanaongoza ni wale waliosoma degree ya kwanza ya education, ambao kwa mwaka 2020 tu tumewatoa wahitimu 14,644, wa degree tu ya kwanza ya education. Halafu ajira tulizozitangaza kwenye specific elimu kwa maana ya walimu wa sekondari na msingi ni elfu 9,800 out of tunaowazalisha wenye first degree ya education ambao ni 14,664.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni ukweli kwamba bado mahitaji ya ajira na upungufu uliopo ni lazima vioanishwe ili tuone kwamba tunapunguza upungufu uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili suala la ajira linakuwa kama zimamoto. Hivi kwa nini Serikali haina mpango maalum, kwamba katika mwaka mmoja wa Mwaka wa Fedha, inakuwepo kabisa, tuna mpango katika mwaka mmoja wa fedha ni lazima tuajiri kiasi fulani, inabaki ni utashi wa awamu hiyo…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa nchi.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani katika hili kabla sijapata muda wa kujibu baadaye nafikiri nilitolee taarifa, kwamba Serikali haiajiri kwa utashi. Bunge lako Tukufu ndilo linalotupitishia bajeti hapa kila mwaka, na katika kila bajeti ya mwaka tumekuwa tunasema tunaajiri idadi gani ya watumishi. Bajeti ya mwaka 2021/2022 ndiyo ajira hizi ambazo tutakamilisha na nyingine 32,000 ambazo tutazitoa na tumeshazitangaza, kati ya ajira elfu 44 plus zilikuwa zote kwenye bajeti na kamati ya USEM nadhani wao wanajuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwaka huu wa fedha unaokuja 2022/2023 tumeweka, nimesoma hapa kwenye bajeti, tumeweka bajeti ya watumishi 30,000. Kwa hiyo naomba niseme kwamba hatuajiri kwa utashi ama mtu anaamka tu, hapana. Kwa hiyo tusipotoshe. Serikali inaajiri, na kuna vigezo ambavyo vitafikia idadi hizo ambazo za watumishi tunaotakiwa kuajiri katika hilo naomba niliweke sana.

MWENYEKITI: Ahsante kwa taarifa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Paresso unapokea taarifa.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa. Hakuna ambaye hafahamu nchi hii awamu ya tano ajira zilizotolewa ni kidogo na wakati mwingine zilikuwa hazipo kabisa, huo ndio ukweli. Halafu tuliondoa watumishi hewa wengi na hatukuajiri, nani ambaye hajui? Tunamshukuru leo Rais Samia angalau hizi japo ni chache lakini zimetoka na wananchi wameziona na wamezisikia, huo ndio ukweli. Kwa hiyo taarifa siipokea ukweli utabaki hivyo kama ulivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kushauri lazima kuwepo na mpango, kwamba Serikali kila mwaka ni lazima, kwa sababu unaangalia wahitimu tunaowatoa kwenye vyuo vikuu ni wengi, hao mwisho wa siku wanaenda. Kwa hiyo tuna wahitimu tunaowatoa kuna wanaostaafu lakini hatuajiri tunasubiri tu, tunaangalia hatuna mpango hatuna utaratibu hatuna chochote tunasubiri tufanye hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilindie muda wangu mawaziri wana nafasi ya kujibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Paresso hebu keti kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri hebu keti kwanza. Mheshimiwa Paresso hili Bunge linakutana kila mwaka kujadili bajeti, linapitisha ndiyo hoja ya Waziri pale. Kwa hiyo unapoenda kuajiri ili uajiri lazima u-create nafasi iwepo, iwe wazi utafute bajeti utafute fedha halafu unatangaza.

Kwa hiyo, hoja aliyoitoa Mheshimiwa Waziri tulidhani pengine imeeleweka vizuri. Ninakuruhusu kuendelea kuzungumza lakini you take into consideration la sivyo nitatumia mamlaka ya kiti changu.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, no mimi hiyo taarifa siipokei na huo ndio mchango wangu na hayo ndio maoni yangu mawaziri watapata nafasi ya kuchangia katika hayo.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendele kuchangia na muda wangu ulindwe.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nollo nimekuona; taarifa.

T A A R I F A

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe tu taarifa mzungumzaji, kwamba kuajiri si kwamba ni jambo la kila wakati unalifanya unategemea na national wages. Kwa hiyo unaweza ukadhani kwamba Serikali inabana isiajiri; kuajiri inategemeana na GDP kuna percentage yake. Kwa hiyo unaweza kuona kwamba Serikali haitaki kuajiri zipo economics ambazo zinafanya kwamba na kuajiri uende kwa stahili hiyo. (Makofi)

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa Paresso ukumbuke muda wako unakaribia kwisha kwa hiyo uanze ku-wind up (kelele)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe.

MWENYEKITI: Unapokea taarifa?

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio hicho ninachotaka kusema kwamba hata anachoeleza Mheshimiwa Nollo haya yanayosemwa yawekwe kwenye mipango na watu wajue, kwamba wage bill ni kiasi gani according to wage bill tunaweza kuajiri kiasi gani huo ndio ukweli na ndicho ambacho tunatamani kukisikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia suala la utawala bora. Utawala bora ni pamoja na kuhakikisha sheria kanuni mifumo na taratibu inafuatwa. Katika nchi hii watanzania wengi wapo wamekuwa clustered kwenye vijiji, na katika vijiji kuna taratibu ya kuendesha mikutano mikuu ya vijiji na kufanya maamuzi ya miradi mbalimbali ya maendeleo, ya mapato na matumizi na kila kitu. Sasa, kumeibuka utamaduni, kwamba mikutano mikuu ya vijiji siku hizi haifanyiki, mikutano mikuu ya vijiji kwa mujibu ya sheria kusoma mapato na matumizi haifanyiki, mipango mbalimbali ya miradi maendeleo katika vijiji haifanyiki; sasa, huu ndio utawala bora ambao tunapaswa kuusimamia na wananchi wakaulewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nchi hii kuna baadhi ya watendaji wa kata na vijiji na wenyeviti wa vijiji, baadhi si wote, wanageuka miunguwatu kwenye maeneo yao, wananchi hawawezi kuwahoji. Baadhi ya watendaji wa vijiji leo wanafanya majukumu ya kutengezea watu tuhuma, wao ni polisi wanakamata wao ni mahakama wanahukumu, wao wanapokea faini. Yaani wao ni final kwenye vijiji na kata zao. Hii haiwezi kukubalika, huu si utawala bora. Ni lazima sasa Serikali mkomeshe huu utamaduni unaotaka kujengeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona jana kwenye mitandao ya kijamii mwananchi mmoja amekatwa panga kwa sababu alikuwa anahoji mapato na matumizi kwenye Mkutano Mkuu wa Kijiji. Sasa ni haki ya mwananchi, ni lazima hao watu wajue kwamba mabosi wao ni wananchi wa Tanzania, wanaweza wakawahoji as long I am-provoke na kwamba havunji sheria hivyo ana wajibu wa kuhoji mapato na matumizi na wale wenye mamlaka kwenye vijiji lazima wahitishe mikutano kwa mujibu wa taratibu. Tunaomba hili lisimamiwe kwa dhati kabisa ili wananchi wafurahie kuwa Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)