Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Utumishi na Utawala Bora. Samahani nina kikohozi kwa hiyo, sauti yangu sio nzuri sana, lakini nitajitahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuendelea kuijalia amani nchi yetu, lakini ameendelea kutupa pumzi Watanzania na Wabunge ili tuendelee kutekeleza majukumu yetu ya kibunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sana viongozi wa Wizara hii, nikianza na Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, Naibu wake Mheshimiwa Deo Ndejembi, Makatibu Wakuu wakiongozwa na Ndugu Ndumbaro pamoja na watendaji wote. Wizara hii ni Wizara inachunga watu, Ndugu Ndumbaro ni mtaratibu na ni mtu mwenye hekima na anaishi kwa utaratibu na yuko makini sana. Kumchunga binadamu inabidi uwe na akili ya ziada kwa hiyo, nawapa hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Wizara hii kwa hotuba nzuri, hotuba makini na imechambua vizuri kuhusu masuala ya utumishi. Misingi ya uongozi wa nchi yetu ililetwa na waasisi wa nchi hii akiwemo baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere pamoja na Mzee Karume. Walitoa matamshi yao ya uongozi kwamba, ili nchi hii iweze kuendelea inahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uongozi bora tunauona kwa Rais wetu mpendwa. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, katikati ya bajeti ya 2021/2022 alifanya jitihada za kutafuta fedha Shilingi trilioni 1.3. Baada ya kuileta fedha ile akaipeleka Kamati ya Bajeti, Kamati ya Bajeti wakaona hii sio size ya Waziri wa Fedha aliyezoea kupanua vifungu, hii hela ni ya kupanua ukomo wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha ililetwa hapa na Wabunge tukapitisha kwa hiyo, sheria hapo ukiangalia utawala bora umetekelezwa. Fedha, bajeti ikaongezeka kutoka trilioni 36 mpaka trilioni 37.94 tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa angalia miongozo ambayo imetolewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, bajeti yam waka huu wa fedha 2021/2022 makusanyo ya ndani walikuwa wamepanga kukusanya Shilingi trilioni 17. Hadi quarter ya tatu TRA walishakusanya trilioni 16. Na kwa ukusanyaji huu wa trilioni 1.84 kwa mwezi ina maana kwamba malengo yatafikiwa na yatapitwa, haijawahi kutokea ni kwa mara ya kwanza tutaona kwamba bajeti inakusanywa kwa asilimia 100. Nampa hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na changamoto za kiuchumi wa dunia zinazoendelea bado Mheshimiwa Rais ameendelea kupambana kupanua vyanzo vya mapato. Ni hapa juzi tu mnaona jinsi ambavyo anaongoza suala la kampeni ya masuala ya utalii kupitia Royal Tour. Matokeo yake unaona bajeti tunayoijadili leo ya mwaka ujao wa fedha sasa tutaingia kwenye Shilingi trilioni 41. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zilizotolewa za Uvico na mimi nishukuru kwamba, jimbo langu lilipata 3,467,110,000 lakini zimefanya nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, zimejenga madarasa ya sekondari pamoja na madarasa ya shule shikizi. Kwa upande wa nchi nzima fedha hizi zimejenga zahanati na kujenga vituo vya afya na hospitali za wilaya. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, activities zimepanuka. Activities zikipanuka maana yake zinahitaji watumishi, lakini kutokana na kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais wetu kwamba, ameongeza fedha mpaka za kuajiri. Niipongeze sana hii Wizara kwa kuajiri kwa kuweka mpango. Kwanza wameshatangaza nafasi za kuajiri watu elfu 11, lakini na sasa wataajiri nafasi za watu elfu 32; na Mheshimiwa Waziri ametuonesha maoteo ya mwaka ujao pengine wa fedha, wanaweza wakatangaza tena nafasi elfu 30. Hongera sana, kweli hapa tunaona siasa safi na uongozi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wenzangu wamesimama kila mtu akasema kwake kuna upungufu kiasi gani wa wawatumishi. Mimi katika Halmashauri yangu ya Mlele nina upungufu wa watumishi 915. Kati ya hao walimu ni 149, lakini wahudumu wa afya ni 546, watendaji wa vijiji 8, lakini kada nyingine ni wahasibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasahivi tutakwenda kujadili ripoti ya CAG na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC. Wakati mwingine hizi hati zenye mashaka na hati chafu zinaletwa kwa sababu ya watu kutokuwa na weledi. Niombe sana na kushauri, kwamba hii kada ya wahasibu na hasa wahasibu wenye CPA, wenye degree pamoja na hizi diploma; na kwa sababu, kwenye bajeti kumewekwa fedha za skill development hawa wakifanyiwa semina nzuri nina hakika kabisa kwamba, hizi hati chafu na hati zenye mashaka zitapungua. Na zinapopungua ndivyo tunavyompa moyo zaidi Mheshimiwa Rais wetu, ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa furaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kutokana na hali yangu ya sauti hii, sikupanga kuongea mengi, lakini nimalizie tu kwa kusema kwamba, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)