Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii; na mimi nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na hasa matumizi ya tafiti kwenye hotuba yake, amerejea tafiti mbalimbali; kwa kweli ni hotuba ambayo imenifurahisha sana. La pili; mipango yote ambayo Mheshimiwa Waziri ameeleza ili iweze kutekelezwa kikamilifu itahitaji fedha; na moja ya chanzo cha fedha kikubwa katika nchi hii ni utalii. Ni kwasababu hiyo na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ubunifu wake wa kuja na The Royal Tour ambayo baadhi ya wataalam wa utalii wametuambia kwamba ina nafasi ya kuongeza volume utalii katika nchi hii mara mbili au mara tatu. Hiyo itatuongezea uwezo wetu wa kuweza kujitegemea lakini hasa ku-finance mambo haya mengi ambayo Mheshimiwa Waziri wa Nchi ameeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie maeneo mawili. Kwanza ni suala la hali ya utumishi wa umma nchini. Na niungane na nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza kuongea kwa hotuba yake na mchango wake mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utumishi wa umma ndiyo injini ya utekelezaji wa sera na sheria ambazo tunazitunga humu Bungeni, ndiyo injini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa, kwa hivyo lazima tuwaheshimu na kuwapa recognition ya kutosha watumishi wa umma. Na kuna kipindi kwakweli tunajisahau, tunajimwagia sifa sisi wenyewe wanasiasa tunasahau kwamba nyuma ya sisi kuna watumishi wa umma ambao wanafanya kazi kubwa ya wakati mwingine katika mazingira magumu. Mimi nichukue nafasi hii kuwapongeza sana watumishi wa umma wa nchi hii kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuendesha nchi yetu na Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utumishi wa umma kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri una changamoto nyingi; lakini nataka niongelee changamoto moja kubwa ambayo tushirikiane namna ya kuitatua. Ni kuhusu suala la uhaba wa watumishi wa umma katika sekta mbalimbali. Wakati mwingine tukilizungumza tunaliweka katika kiwango pengine hakiakisi uhalisia. Hebu tuangalie, nitoe mifano katika sekta saba kama muda utaniruhusu.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni elimu. Kwa mujibu wa taarifa za Serikali ambazo nimezichambua kupitia bajeti hii, Walimu wa Sekondari na shule za Msingi mahitaji ya nchi hii ni 433,992, Walimu waliopo ni 258,291, upungufu ni Walimu 175,701 sawa na asilimia 40.

Mheshimiwa Spika, sekta ya afya. Tunahitaji 208,232, waliopo 98,987, upungufu 109,295 sawa na asilimia 52.5. Lakini ukitaka kuangalia tatizo kubwa zaidi nenda kwenye zahanati na vituo vya afya kwa sababu huko ndiko zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanatibiwa kwenye zahanati na vituo vya afya. Vituo vya afya na zahanati nchi hii vinahitaji watumishi 131,547, waliopo ni 48,579, upungufu 82,968 na asilimia 63.1 ni upungufu.

Mheshimiwa Spika, katika sekta ya maji afadhali kidogo ndiyo bora, watumishi 10,279 ndiyo mahitaji, Watumishi waliopo ni 9,207, upungufu ni 169 sawa na asilimia Moja tu ya upungufu. Kwa hiyo sekta ya maji tupo vizuri kwa kiasi cha kutosha. Kilimo (productive Sector). Tunazungumzia mahitaji ya Maafisa Ugani 20,000 waliopo ni 9,600, upungufu ni 13,400, sawa na asilimia 67 ya upungufu.

Mheshimiwa Spika, jumla kwa sekta hizi chache ambazo nimezitaja tunazungumzia tunahitaji Watumishi wa Umma 1,238,089, waliopo 679,955, upungufu ni 558,134 jumla ya upungufu ni asilimia 45 maana yake nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ameeleza vizuri hapa kwamba Serikali mwaka huu itakwenda kuajiri na tumepata kibali cha staff 30,000 na tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa kibali hicho. Lakini tunazungumzia 30,000 kati ya upungufu wa 679,955, maana yake tunakwenda kutatua tatizo kwa kiwango cha asilimia 4.4. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimefanya hesabu, trend ikiwa ni hii ili tuweze kutatua gap hii tutahitaji miaka 21, ili ku-address hii gap iliyopo we need 21 years. Ni wazi kwa saizi ya uchumi wetu ni wazi kabisa haitawezekana ku-address tatizo hilo kwa kutoa tu vibali. Ukisoma taarifa za Wizara mbalimbali wanaeleza changamoto ya ajira solution yake nini? Tumeomba kibali utumishi, yaani ndiyo solution inaishia hapo. (Makoni)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kutoa mapendekezo nikiamini kwamba kwa kweli hata iwe ni Serikali ya Marekani kwamba inaweza ikaajiri watumishi hawa tukaziba hii gap haitawezekana. We need to think of alternative ways na Mheshimiwa Waziri utusaidie, mje na mikakati mipya namna ya kutatua tatizo hili. Naomba nitoe mapendekezo manne.

Mheshimiwa Spika, moja, kwanza ifanyike National Audit ya Watumishi wa Umma. Nilipokuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji tuliamua kufanya National Audit ya Watumishi wa Umma tukaenda tukagundua kwamba kuna kazi zinafanywa na wafanyakazi wawili kwa kazi moja, ndiyo ikatusaidia ile ndiyo unaona upungufu katika Wizara ya Maji ni asilimia moja kwa sababu ya National Audit ambayo tulifanya. Serikali ifanye National Audit tupate mahitaji halisi ya Watumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, tutekeleze sera ya D by D kwa uhakika. Kwa mfano, kwa nini Serikari iajiri Maafisa Ugani? Kwa nini mapato ya mazao ya kilimo katika kijiji yabaki hapo wakaajiri wao, kwa nini tusitumie mtindo huo? Hiyo inaweza ikaangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani la mwisho tuweke mazingira mazuri kwenye sekta binafsi ili kwamba kwa mfano katika shule, asilimia Tatu peke yake ya shule ndiyo za sekta binafsi kwa shule za msingi zilizobaki ni za Serikali. Tukiweka mazingira mazuri watu binafsi wafungue shule nyingi zaidi za msingi wataajiri Walimu, hivyo hivyo katika sekta ya kilimo na zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ni Sekta ya Madaktari. Madaktari wengi katika hospitali za binafsi wanatoka sekta ya umma, ni muhimu tuweke mazingira mazuri ili sekta ya umma ya afya iweze kuajiri watumishi wake badala ya kutumia watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie mchango wangu na eneo moja muhimu la haraka. Suala la bodaboda, machinga lipo katika ukurasa wa 42 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, tuelewe vizuri structure ya uchumi wetu ikoje, niwapeni mfano katika Jimbo la Ubungo sisi tunazo Kata Nane, Jimbo la Ubungo tuna bodaboda 4,891. Kimara 728, Mabibo 683, Makuburi 847, Makurumila 839, 655, 656,645 na Ubungo 838. Kata ya Ubungo yenye bodaboda 838, bodaboda wanne wana Masters, bodaboda 21 ni Graduate, Digrii ya Kwanza, hiyo ipo katika Dar es Salaam huko wengi ni Form Four, Form Six, Graduate, kwa hivyo hii ni sekta muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Mikoa waelezwe na Mheshimiwa Waziri mtupe mtamko hapa, hii tabia ya kutoa matamko yakusumbua sekta binafsi yaishe. Tungetaka tamko hapa la Waziri atueleze kwamba anapiga marufuku bodaboda kupigwa marufuku kuingia Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ina vipaumbe Sita, kipaumbele cha Sita kinazungumzia kuajiri wafanyakazi Milioni Nane kutoka sekta iliyorasmi na isiyorasmi tutapataje Milioni Nane tukianza kuwasumbua watu hawa? Hawa ndiyo ajira zetu hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliahidi Dar es Salaam kwamba, tulitoa ahadi kwa bodaboda hamtapigwa marufuku tena kwenda katikati ya Jiji, sasa tupate tamko la Serikali kwamba hili tamko la jana ni la mwisho kusumbua bodaboda katika nchi hii, hawa ndiyo wenye uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Ahsante. (Makofi)