Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufikia hatua hii ya kuhitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika dunia hii nina madeni makubwa kwa watu sita. Kwanza ni Mwenyezi Mungu, ninamshukuru sana kwa wema wake ninamshukuru sana kwa kutujalia uzima tukaweza kufika mahali hapa jioni hii kwa ajili ya kuhitimisha hoja ambayo umenipa nafasi ya kutoa ufafanuzi kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuniamini lakini pia kwa niaba yake nipokee pongezi nyingi sana ambazo Waheshimiwa Wabunge kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI mmezielekeza kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa nzuri ya kuliongoza Taifa letu ambayo anaifanya na ninyi ni mashuhuda kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Rais wetu ameupiga mwingi sana kwenye mitaa na vijiji, vijijini na mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie nafasi hii kulishukuru Bunge lako Tukufu kwa namna ambavyo mnaisaidia Serikali katika kutimiza wajibu wake, binafsi nikushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Spika pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa kweli deni ambalo ninalo kwenu pamoja na Mheshimiwa Rais na Watanzania ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mijadala hii mmenikumbusha kwamba imani hii ambayo mnayo kwangu, Waheshimiwa Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Wataalam wote ambao wako chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kweli kwa niaba yao niwaahidi hatutawaangusha. Tutalinda imani hii kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili tusimuangushe Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, tusiliangushe Bunge lako Tukufu pamoja na Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika shukrani zangu niwashukuru sana wananchi wangu, mabosi wangu, wananchi wa Karagwe kwa kuendelea kuniamini katika majukumu yangu ya kuwawakilisha hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika shukrani zangu pia niishukuru familia yangu kwa kuendelea kuniombea na kuniunga mkono katika majukumu yangu ya kulisaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee ninakupongeza wewe binafsi pamoja na Mheshimiwa Spika, Wenyeviti, Wabunge kwa uongozi wenu mahiri uliouwezesha Bunge lako Tukufu kujadili bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa weledi mkubwa. Ninawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii na wale ambao hawakupata fursa ya kuchangia kutokana na sababu mbalimbali likiwemo suala la muda. Maoni na ushauri uliotolelewa na Waheshimiwa Wabunge umesaidia kutoa mwelekeo wa kuboresha mpango wa bajeti ili kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa nimpongeze tena Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwezesha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, taasisi zilizo chini yake, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yake katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipoishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mheshimiwa Abdallah Chaurembo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Wajumbe wa Kamati na Sekretarieti kwa uchambuzi makini wa Mafungu 28 ya bajeti yanayosimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kimsingi pongezi nyingi ambazo Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepata katika utendaji wake zinatokana na ushirikiano mkubwa wa Kamati ya USEMI na Kamati ya LAAC chini ya Mheshimiwa Grace Tendega Mwenyekiti na Mheshimiwa Selemani Zedi Makamu Mwenyekiti, tunawashukuru sana kwa namna ambavyo mnatusimamia katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutambua mchango mkubwa wa viongozi wenzangu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kipekee nawashukuru sana Naibu Mawaziri Mheshimwia Dkt. Festo Dugange, Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe na Mheshimiwa David Silinde, Mbunge wa Jimbo la Tunduma na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa Tanzania Bara kwa msaada wanaonipa katika kutekeleza majukumu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Profesa Shemdoe na Manaibu Makatibu Wakuu kwa mchango wao katika kufanikisha maandalizi ya mpango wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, bosi wangu, nakushukuru sana kwa namna unavyotuongoza. Ninakushukuru sana kwa maelekezo ambayo unaipatia Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kuwahudumia Watanzania. Kwa hiyo pongezi hizi ambazo tumezipata na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri Mkuu pia zije kwako unatusimamia vizuri, wewe ni Kiongozi mahiri, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hoja mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezizungumza. Ninawashukuru Manaibu Mawaziri kwa ufafanuzi mzuri na mimi naomba kwa muda ambao umenipa nitoe ufafanuzi kwa hoja mbalimbali na nianze na hoja ambayo pamoja na kwamba haikutokea kwenye Bunge hili lakini mitandaoni kulikuwa na sintofahamu. Suala la ununuzi wa pikipiki 68 za Maafisa Ustawi wa Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge tarehe 14 mwezi Aprili, 2022 niliwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Katika eneo la utekelezaji wa bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, sehemu ya huduma ya Ustawi wa Jamii nilisoma kwamba, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya ununuzi wa pikipiki 68 aina ya boxer zenye thamani ya Shilingi Milioni 789.9 kwa ajili ya Maafisa Ustawi wa Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge ninaomba kutoa taarifa kwamba idadi ya pikipiki 68 iliyotajwa kwenye Hotuba yangu siyo sahihi na hii imetokana na makosa ya kiuandishi. Usahihi ni kwamba pikipiki 68 zimenunuliwa na wadau kwa gharama ya Shilingi Milioni 227.5 ambao walikuwa wanatekeleza miradi ya USAID Kizazi Kipya, katika baadhi ya Halmashauri katika Mikoa 21 ambazo zilinunuliwa na kusambazwa mwezi Septemba mwaka jana, 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lengo la kutosheleza mahitaji ya pikipiki kwa Maafisa Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais, TAMISEMI iliona inunue pikipiki 200 aina ya boxer, kwa sasa ziko katika hatua ya mwisho ya manunuzi. Pikipiki hizi zinanunuliwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa gharama ya Shilingi Milioni 562.4. Pikipiki hizo zitasambazwa kwenye maeneo ambayo hayakupata kwenye mgao wa pikipiki 68. Hivyo jumla ya pikipiki zitakuwa 268.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba ofisi ya Rais, TAMISEMI imenunua pikipiki moja kwa Shilingi Milioni 11 siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la miundombinu ya wafanyabiashara wadogo yaani machinga. Waheshimiwa Wabunge hapa Dodoma tunayo tuiite modal ya soko la machinga ambalo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, Kamati ya USEMI mlipata fursa ya kutembelea soko hili na ninaamini hata Waheshimiwa Wabunge katika zunguka zunguka yenu mmeshapata fursa ya kuangalia soko hili ambalo linajengwa nasi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa niaba ya Serikali na kwa ushauri wa Bunge kupitia Kamati ya USEMI tumeona ni vyema soko lile ambalo wote tumependezwa nalo tutafute master plan na tutengeneze standard ambayo kwenye Majiji na Manispaa tutakuwa tunajenga masoko ya wazi ya machinga kama hili ya Dodoma ili wafanyabiashara wadogo wamachinga waweze kuwa na maeneo rafiki ya kufanyia biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha miundombinu ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo - machinga, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha shughuli zao zinafanyika kwa tija. Hatua ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuwapanga machinga kwenye maeneo rasmi kwa utulivu pasipo kutumia nguvu katika Halmashauri zote zilizokuwa na machinga wengi kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine iliyochukuliwa ni Serikali kutoa Shilingi Bilioni Tano kwa ajili ya kuboresha maeneo ya kufanyia biashara machinga katika Halmashauri 11.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine inayoendelea ni kuwepo kwa majadiliano na Wizara ya Fedha na Mipango ili kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura Na. 290 ili kuruhusu sehemu ya fedha za mikopo ya asilimia 10 kutumika katika kuboresha miundombinu ya machinga. Marekebisho ya sheria hii yamependekezwa kufanyika kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022. Majadiliano hayo yakikamilika, tunatarajia kiasi cha Shilingi Bilioni 38 zitapatikana kupitia mlango huo kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya wafanyabiashara wadogo yaani machinga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo kingine cha mapato kinachotarajiwa ni kupitia asilimia 10 ya fedha zilizotengwa kwenye miradi ya maendeleo ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Kupitia chanzo hiki kiasi cha Shilingi Bilioni 36.82 kinakadiriwa kupatikana. Mapendekezo ya kutumia asilimia 10 ya fedha za miradi ya maendeleo zinalenga kuhusisha Halmashauri zenye mapato yanayozidi shilingi bilioni tano pamoja na Halmashauri nyingine ambazo zimejumuishwa kwenye mpango wa kuboresha maeneo ya machinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia vyanzo hivyo, Halmashauri zitakusanya jumla ya shilingi bilioni 74.83 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya machinga. Jumla ya fedha itakayotumika katika kuboresha miundombinu hiyo itakuwa shilingi bilioni 79.83 ikijumuisha shilingi bilioni tano ambazo zimekwishatolewa na Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kama seed capital.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge katika hii seed capital ambayo Mheshimiwa Rais ametupatia shilingi bilioni tano ndipo tumekaa na Wizara ya Fedha na Mipango kuangalia vyanzo vingine ambavyo vitadunduliza kwenye hii Bilioni Tano ili tuweze kujenga miundombinu ya masoko ya wazi ya wamachinga kwenye Majiji, Manispaa na hata baadhi ya Halmashauri za Mji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa kundi hili katika kukuza uchumi, hivyo ninapenda nitumie fursa hii kuwaelekeza viongozi wote wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha vitendo vya kuwanyanyasa machinga na kutumia nguvu katika kuwaondoa na kuwapanga ikiwemo kuharibu bidhaa zao kama ilivyotokea kwa Jiji la Mwanza vinakomeshwa mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tangazo la ajira. Naomba nitumie fursa hii kwanza kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa idhini ya ajira za watumishi wa sekta ya elimu na afya 17,412 ambapo nafasi 9,800 ni za Walimu na 7,612 ni Kada za Afya ambao watatarajiwa katika Mwaka huu wa Fedha 2021/2022, wataajiriwa Mwaka huu wa Fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa taarifa rasmi kuwa watanzania wenye sifa wanaelekezwa kuanza kuomba kuanzia leo. Napenda kuwaelekeza kuwa maombi ya ajira hizi ni bure na yanafanyika kupitia mfumo wa kieletroniki ambao maelekezo yake yatakuwa katika tangazo la ajira. Asilimia tatu ya ajira hizo ni kuajiri ndugu zetu wenye ulemavu kulingana na sheria inavyotutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaelekeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha wanawanunulia ndugu zetu watu wenye ulemavu mafuta kwa ajili ya sun screen. Jambo hili Mheshimiwa dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa alichangia kwa hisia na uchungu mkubwa. Tumekusikia Dada yangu kwa niaba ya ndugu zetu hawa wenye uhitaji huu, sasa nitumie nafasi hii kuwaelekeza Halmashauri zote kuhakikisha mafuta haya yanapatikana kwa ndugu zetu hawa wenye uhitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TARURA. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi walizozitoa kufuatia utekelezaji wa agizo la TARURA kuanza mapema ununuzi wa mikataba ya utekelezaji wa miradi ya barabara. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 ununuzi wa kazi utaanza mwanzoni mwa mwezi Mei. Waheshimiwa Wabunge katika hili yani nikimaliza kusoma bajeti na mkatupitishia, TARURA wanaanza maandalizi ya manunuzi, tofauti na zamani bajeti inapitishwa, Mwaka wa Fedha unaanza, mikataba inachelewa kusainiwa na mahali pengine wakandarasi wanaenda mvua zimeanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo Waheshimiwa Wabunge baada ya kuja kwenye Wizara hii tulivyofanya study tukakuta TANROADS wao wamekuwa wakitumia utaratibu huu kwa miaka mingi sana. Kwa hiyo, tukaona hata TARURA, bajeti tuu inapopitishwa na Waheshimiwa Wabunge niwaombe sana mtusaidie mtupitishie bajeti hii ili kesho TARURA waanze kujipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha ugawaji wa rasilimalifedha za TARURA, inafanya mapitio ya formula itakayotumika katika kugawa rasilimali fedha za ujenzi wa matengenezo ya miundombinu ya barabara kulingana na hali ya maeneo husika. Jambo hili Waheshimiwa Wabunge mmetueleza sana kwa hiyo naomba muendelee kutupa ushirikiano tutalifanya kwa tathmini ya kina ili kuwe kuna formular kulingana na jiografia na ukubwa wa uhitaji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kuleta weledi na usimamizi makini tutapima utendaji kazi za Mameneja wa TARURA ngazi za Mikoa na Wilaya na nimeagiza kila quota niwe napata taarifa ya utekelezaji wa miradi ya barabara kwenye Wilaya zetu. Kutokana na taarifa hiyo tutaweza kuchukua hatua kwa wale Regional Managers na District Managers ambao watakuwa hawatoshi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwashukuru sana kwa namna ambavyo mnaendelea kushirikiana na sisi, mnapoona kuna kasoro kwenye maeneo yetu tupeni taarifa ili tuweze kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana Mheshimiwa Zeeland baada ya kufanya ziara kule Mvomero, nilitoa maagizo Machi 10, jana katika mchango wake akanitaarifu kwamba yale maagizo ambayo nilikuwa nimeyatoa kule Mvomero hayajafanyiwa kazi, leo mmeona hatua ambazo nimechukua. Kwa hiyo niendelee kuwaelekeza Wakurugenzi wawe makini tumewaamini katika kusimamia Halmashauri hizi, Mheshimiwa Rais wetu, mpambanaji wetu, mnaona ninyi ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge miradi inatiririka kwenye Majimbo yetu haijapata kutokea. Kwa hiyo, lazima tushirikiane Waheshimiwa Wabunge katika kuhakikisha fedha hizi zinapoenda zinasimamiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwa ushirikiano wenu ninawaahidi wale Wakurugenzi ambao watakuwa wanatimiza wajibu wao, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutakuwa wabunifu katika kuwa-recognize kwa kazi nzuri ambayo wanafanya, wale ambao watakuwa ni wazembe tutaendelea kuchukua hatua kama mlivyoona leo kule Mvomero. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ufuatiliaji na tathmini, uratibu katika ngazi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha ufuatiliaji na tathmini katika ngazi za Makao Makuu, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha usimamizi kwenye Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Rais amemteua Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Sekta za Uchumi na Uzalishaji kama ilivyo Sekta ya Elimu na Afya. Waheshimiwa Wabunge kama mnavyofahamu pale TAMISEMI tunae Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Elimu, tunaye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya na Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo mmetueleza kwamba Wizara hii inamgusa kila mwananchi ilimpendeza akatuongezea Naibu Katibu Mkuu ambae anashughulikia masuala ya Utawala yaani ya TAMISEMI. Sambamba na hilo kama mlivyochangia productive sectors, sectors ambazo zinazalisha na kwa sababu TAMISEMI ndiye mratibu mkuu wa miradi ya kisekta, Naibu Katibu Mkuu huyu pia anajukumu hilo, kwa hiyo ningependa kuwaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ambazo zinazalisha Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Ndaki, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa shemeji yangu Dokta Kijaji, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, tunaendelea kushirikiana ili hizi productive sectors sisi TAMISEMI kwa sababu utekelezaji wote unafanyika ngazi za Halmashauri, tuji- coordinate vizuri ili kuhakikisha vipaumbele vyao na bajeti zao ambazo wanazitenga kupitia Idara hii ambayo inasimamiwa na Naibu Katibu Mkuu huyu ambaye Mheshimiwa Rais ametupatia tuweze kuwasaidia wenzetu ambao wanasimamia sekta za uzalishaji kuhakikisha vipaumbele vyetu na vya kwao vinasomana ili kupeleka huduma bora kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge kwenye hili tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuwezesha kupata hii additional manpower na nimpongeze Dokta Sweetbert Mukama anafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na Naibu Makatibu Wakuu na Katibu Mkuu. Kwa hiyo, tutaendelea kupitia Idara hiyo kuweza kutoa huduma hata kwenye productive sectors. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imeongeza bajeti ya matumizi mengineyo katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa kutoka Bilioni 57.44 hadi Shilingi Bilioni 79.09 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya ofisi hizo ikiwemo ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya hivyo na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuwezesha. Ofisi ya Rais, TAMISEMI hatuwezi kwenda na manual system, yaani Waziri likitokea jambo Katavi kule toka Dodoma unakimbia na wakati kuna RC ngazi ya Mikoa kwa maana ya Tawala za Mikoa lakini ngazi ya Serikali za Mitaa yuko Mkuu wa Wilaya, kwa hiyo mkakati ambao tunao na tumeanza kuufanyia kazi ni kuhakikisha tuna-strengthen Regional Secretariat pia hata Halmashauri zetu CMT ili kuweza kusimamia miradi kwa kufuata mtiririko huo wa mifumo na changamoto ambazo ziko kwenye mifumo tunazirekebisha. Hii in the long term itasaidia sana kuwa kuna mifumo na structure ya Serikali ambayo badala ya ku-divert yaani Wizara inafanya kila kitu kwenye vijiji, mitaa, tuna-strengthen Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ili sasa structure ya utumishi iweze kufanyakazi kwa weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hii pia ndiyo imepelekea kwanza tuwawezeshe Sekretarieti za Mikoa, sasa tuwadai kazi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala kazi kwenu. Waheshimiwa Wabunge wakitupitishia bajeti hapa tumewaongezea bajeti, matararajio yangu ni kwamba hamtakuwa mnafanya basic work mtakuwa mnaenda kwenye Halmashauri na kusimamia miradi ku-monitor na ku-evaluate na kutoa taarifa ili wale wanaofanya vizuri tuwape promotion tuwape recognition na wanaofanya vibaya tuweze kuchukua hatua stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeimarisha mfumo wa kupima utendaji wa Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kwa kutumia viashiria muhimu yani KPI’s ukusanyaji wa mapato ya ndani ni moja ya kigezo, upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maendeleo ni kipimo kingine, matumizi sahihi ya fedha hizo ni kipimo kingine, usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ikiwa ni pamoja na marejesho ni sehemu ya kipimo, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzuiaji na utekelezaji wa hoja za CAG ni moja ya vipimo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye quarterly report ambazo nitakuwa nasoma za mapato tunabadilisha mfumo kidogo tutakuwa tunatoa grade, zipo Halmashauri zitapata A, zipo zitakazopata B, C sasa watakaopata mswaki ndiyo kama yaleyale ya hati chafu, ni kuwachukulia hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia KPI’s hizi hata Mkurugenzi anaweza akajipima kabla hajachukuliwa hatua yuko wapi katika kusimamia miradi na vigezo hivi ambavyo tumeviweka. Ofisi ya Rais, TAMISEMI nimezungumzia hizo KPI’S na matokeo ya upimaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Mamlaka za Serikali Mitandao yani e-GA tumeanza kuboresha mfumo huu ili kuwezesha kutumika kwa urahisi kwa vituo vyote 5934 vya Serikali hususani hivi vilivyopo vijijjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwezo wa kuunganika na kusomana na mifumo ya Kitaifa ili tuweze kupata taarifa na takwimu ngazi ya Taifa na kuhakikisha usalama wake wa mifumo hii na database. Lengo la Ofisi ya Rais -TAMISEMI ni kuweka mfumo huu kwenye vituo vyote ifikapo mwaka 2024/ 2025 kazi hii itafanywa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na kusimamiwa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hatua za kinidhani kwa watumishi. Ofisi ya Rais - TAMISEMI katika kusimamia masuala ya nidhamu na maadili ya kazi katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, imekuwa ikichukuwa hatua za kinidhamu kwa watumishi wanaokiuka sheria na taratibu za kazi ikiwemo ubadhilifu, uzembe, ukiukwaji wa maadali ya kazi na taaluma zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Ofisi ya Rais -TAMISEMI imewasimamisha kazi Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Wanne, imewashusha vyeo Waganga Wakuu wa Mikoa wawili, Waganga wa Wakuu wa Halmashauri - 14, Afisa Elimu Mkoa - Mmoja, Maafisa Elimu ngazi ya Wilaya - Tisa na Wakuu wa Vitengo vya Manunuzi ngazi ya Halmashauri - 24.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa watumishi wote wa umma kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma, ninazielekeza Mamlaka za Nidhamu kuhakikisha zinachukuwa hatua stahiki kwa wale ambao wamebainika kukiuka taratibu. Serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kukiuka taratibu za maadali ya kazi na taaluma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa Vituo vya Afya vya Tarafa na Kata za Kimkakati. Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatambua umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika uendelezaji wa miundombinu sambamba na kuiwezesha kutoa huduma za afya kwa kuwa na vifaatiba na watumishi. Katika kutekeleza hilo Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeweza kufanya tathmini ya uhitaji wa vituo vya afya 428 ambapo vitajengwa kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 ambavyo vitajengwa katika Tarafa zisizokuwa na Vituo vya Afya na Kata za kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge kwenye hili Ofisi ya Rais -TAMISEMI tulileta fomu mkajaza zile Tarafa ambazo hazijapata vituo vya afya lakini zile Tarafa ambazo zimeshapata vituo vya afya maeneo ambayo ni kimkakati yanahitaji kupewa vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuahidi pamoja na Bunge lako Tukufu, kipaumbele ambacho tumejiwekea, mwaka huu na niwashukuru sana mmeunga mkono jambo hili tukamilishe maboma lakini kuanzia Mwaka wa Fedha 2023/2024 tuende sasa kwenye zile fomu ambazo mlijaza maeneo ambayo yanahitaji vituo vya afya tuendelee na utaratibu huo wa kujenga kuhakikisha vinapokamilika vinapata vitendea kazi na masuala ya Wauguzi. Hivyo, Waheshimiwa Wabunge niwashukuru kwa kuunga mkono mkakati wetu wa kwamba mwaka huu kipaumbele kikubwa kiwe kwenye kukamilisha maboma.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais ameshatupatia fedha tuko hatua za uzabuni wa kununua vifaatiba kama hivi mnaona tumeajiri na tutaendelea kuajiri kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ukarabati wa Shule, Vituo vya Afya na Zahanati Kongwe. Kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 mpaka 2021/2022, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeweza kufanya ukarabati wa Shule Kongwe za Sekondari 89 kati ya shule 92. Kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 Ofisi ya Rais- TAMISEMI imepanga kufanya kukarabati wa Shule za Msingi Kongwe jumla ya Shule zilizoanza kabla ya mwaka 1961 ni shule 2,147. Shule hizi zitakarabatiwa kwa awamu baada ya kukamilisha tathmini ya gharama za ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati huu ni endelevu katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 jumla ya vyumba vya madarasa 1,700 vya shule za msingi kongwe ambavyo vimetengewa jumla ya shilingi bilioni 34 vitakarabatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa afya ya msingi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, Ofisi ya Rais - TAMISEMI imepanga kufanya ukarabati wa Hospitali za Halmashauri Kongwe 19 kati ya hospitali 77, ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 16.55 zimetengwa. Ofisi ya Rais - TAMISEMI itafanya zoezi la kutambua vituo vya afya na zahanati zilizojengwa kati ya mwaka 1961 hadi 1970 ili kuweka mkakati wa kuvikarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge haya ni maelekezo yenu tumewasikia tunaenda kufanya tathmini ili kuweka kwenye vipaumbele kwenye mwaka wa fedha unaofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ukamilishaji wa miradi iliyoanzishwa na kutokamilika. Ofisi ya Rais-TAMISEMI inakubaliana na hoja za Waheshimiwa Wabunge za kuwepo kwa miradi iliyoanzishwa miaka ya nyuma na bado haijakamilika ninapenda kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa wote Tanzania Bara kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya kina kuhusu miradi na gharama zake za ukamilishaji ili Ofisi ya Rais- TAMISEMI iweze kuitambua miradi hiyo na kuweka mikakati ya ukamilishaji wake, taarifa hiyo iwasilishwe kabla au ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakubaliana na hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu ukosefu wa vifaa na vifaatiba katika vituo vya afya vilivyokamilika kujengwa. Kuanzia Mwaka wa Fedha 2018/2019 hadi Mwaka wa Fedha 2021/ 2022 Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 82.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba katika ngazi ya Afya na Msingi ambapo Shilingi Bilioni 15 zimetumika kununua vifaa na vifaatiba na kuvisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa vingine manunuzi yake yanaendelea, vifaa hivi vinajumuisha vifaa na vifaatiba kwa ajili ya utoaji wa huduma za upasuaji na huduma za mionzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 imetenga Shilingi Billion 47. 7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwenye vituo vya afya 159, Ofisi ya Rais - TAMISEMI inafuatilia vifaa na vifaatiba ambavyo tayari vimeshalipiwa fedha kutoka Bohari Kuu ya MSD ili kuondoa changamoto ya vituo vya afya vilivyokamilika na kukosa huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Ofisi ya Rais - TAMISEMI itaendela kuzisimamia halmashauri ili ziongeze wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani. Mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuwajengea uwezo Maafisa wanaokusanya mapato, kuboresha mfumo mapato na utambuzi wa fursa na ujibuji wa vyanzo vipya vya mapato. Aidha utendaji wa Halmashauri utapimwa kuzingatia upelekeji wa asilimia 40 kwa 60 na 70 kwa Halmashauri hizi chache zenye makusanyo makubwa zinazotokana na makusanyo ya mapato ya ndani yasiyolindwa katika miradi ya maendeleo, utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, viijana na watu wenye ulemavu na ulejeshaji wa mikopo na ujibuji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati na kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ili kuleta tija na kuimarisha utoaji huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Halmashauri ziliidhinishwa kukusanya shilingi bilioni 863.85 kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani. Hadi Februari 2022 zimekusanya shilingi bilioni 586.07 sawa na asilimia 68. Fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 331.08 hadi Februari 2022, shilingi bilioni 216.11 sawa na asilimia 65.27. Ofisi ya Rais - TAMISEMI itaendelea kusimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapelekwa kwa wakati katika maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 imepanga kuongeza mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kufikia shilingi trilioni 1.1 sawa na ongezo la asilimia 17.18. Mafanikio haya yatafikiwa kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake, kufanya ufuatiliaji mara kwa mara, fedha zote zinakusanywa

kuingizwa benki kabla ya matumizi, vyanzo vyote kuwa na POS katika kukusanya mapato, kufanya tathmini ya wadaiwa na kuweka mikakati ya kukusanya madeni hayo na matumizi sahihi ya mifumo ya kieletroniki ikiwemo mfumo wa TAUSI, GoTHoMIS katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi sahihi ya mashine za kukusanyia mapato (POS) ni muhimu hivyo ninaelekeza kila Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhakikisha POS zote hasa zile za zamani kabla ya mwaka 2019 zinawekewa toleo jipya la APK Toleo la 499649 ili kuondoa mianya ya kupoteza mapato.

Mbili; kufanyika kwa ukaguzi wa POS kila mwezi ili kubaini POS zipo ngapi, zipo wapi, ngapi zipo online, ni nani wanaozitumia.

Tatu; Kuhakikisha POS zote ambazo haziko hewani ziko offline kutokana na ubovu au kutojulikana zilipo zinafifishwa kwenye mfumo yani zinakuwa di-activated.

Nne; kufanya job rotation kuzungusha wanaosimamia ecosystem nzima ya ukusanyaji wa mapato Wahasibu na wengine.

Tano; kuhakikisha mapungufu ya POS kwenye maeneo ya ukusanyaji yanabainika na mkakati wa kununua POS unawekwa kukidhi mapungufu hayo ili kuongeza mapato.

Sita; Kuhakikisha register zote za POS zinahuishwa kuendana na taarifa za mfumo kwa usahihi kutoa hamasa ya kudai risiti kwa kila huduma kutoka kwa mkusanya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI inahuisha mfumo wa ukusanyaji mapato wa TAUSI ambao utafanya yafuatayo: -

i. Usimamizi wa POS, maboresho ya POS na changamoto zake sasa mfumo huu wa tausi unaenda kutibu yale mapungufu ambayo tumeya-experience kwenye mfumo wa POS.

ii. Usimamizi wa float ili kuondoa matumizi ya fedha mbichi na kuondoa madeni ya float management.

iii. Kuhamasisha malipo ya kodi, tozo na ushuru, kwa kielektroniki bila kufika ofisi za Mamlaka za Serikali za Mitaa yani online payment kwa maana ya caShless system.

iv. Kujifanyia tathmini ya kiasi mlipaji anachopaswa kulipa (online assessment)

v. Kutoa leseni na vibali vya kieletroniki digital license na permit.

vi. Kuunganisha mfumo na mifumo ya TRA kupata mapato ghafi ya wafanyabiashara kwa ajili ya kupata kodi halisi ya huduma (service levy).

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Mamlaka za Serikali za Mitaa Mtandao inaendelea kuboresha mfumo wa GoTHOMIS ili uweze kutumika na vituo vyote vya kutoa huduma za afya vya ngazi ya msingi, hasa maeneo ya vijijini, maboresho yatazingatia maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais kuhusu kuimarisha mifumo ili izungumze. Mfumo huu unasaidia kusimamia na kudhibiti madawa na vifaatiba, kutoa taarifa ya magonjwa na ugonjwa na kusimamia mapato yatokanayo na uchangiaji wa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo kwa sasa upo kwenye vituo 1,161 na utawekwa kwenye vituo vyote vya afya ifikapo Mwaka wa Fedha 2015/2016. Kuhusu Serikali itoe waraka mpya wa posho za Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri mwenye dhamana za Serikali za Mitaa alishatoa waraka wenye kumbukumbu ya tarehe 23 mwezi wa 12 mwaka 2014 juu ya posho za mwezi za Madiwani. Aidha posho za vikao za Waheshimiwa Madiwani zimeelekezwa katika waraka uliotolewa mwaka 2007 na kusitishwa katika waraka wa tarehe 16 Agosti, 2012 ambapo ni Shilingi 40,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo posho za Waheshimiwa Madiwani ni hisani ya Mkurugenzi wa Halmashauri. Kwa sasa tunaandaa miongozo Waheshimiwa Wabunge ili kuhakikisha posho za vikao za Waheshimiwa Madiwani mwongozo huu tutafanya tathmini ili kuhakikisha angalau kunakuwa kuna mfanano nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiti chako kilishatoa mwongozo kuhusu masuala yanayohusu stahiki za Waheshimiwa Madiwani kupitia Kamati ya Bajeti yataendelea kujadiliwa ili kuweza kuhakikisha tunajenga mustakabali mzuri Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Madiwani katika kuhakikisha tunatekeleza ilani ya Chama chetu vema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kamati ya Fedha peke yake kukagua miradi katika Halmashauri zetu. Kamati za Kudumu za Halmashauri zinaweza kutembelea miradi ya maendeleo au shughuli yeyote inayotekelezwa kwa niaba ya Halmashauri na ambayo inahusu Kamati husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri nyingi Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango ndiyo imebeba jukumu hilo peke yake kitu ambacho ni kinyume na Kanuni za Kudumu za Halmashauri. Waheshimiwa Wabunge jambo hili mmelizungumza tutakaa tulitathmini ili tuweze kulitolea mwongozo mzuri, kwa sababu kamati zote ziliundwa kwa kuleta weledi katika kusimamia miradi, kwa hiyo tungependa kuona kamati zote zinatimiza wajibu wake kulingana na mgawanyiko wa majukumu katika halmashauri zetu, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge ili tumelichukuwa tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoanza nashukuru sana, nikushukuru wewe nimshukuru Mheshimiwa Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri, tumewasikia hoja zote ambazo mmechangia tumezichukua na kwa ushirikiano ambao mmeendelea kutupatia niwahakikishie mimi pamoja na Waheshimiwa Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya Watumishi wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI tutaendelea kuwapa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha yale ambayo mmetuelekeza, mmetushauri tunayaweka katika utekelezaji wa Serikali na kuhakikisha mwaka wa fedha utakaokuja zile hoja ambazo mmezieleza hapa na tumezichukua tunazitekeleza kwa weledi mkubwa ili tutakaporudi hapa tusiwe tuna maswali mengi ya viporo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitumie nafasi hii na Waheshimiwa Wabunge kuwashukuru sana na mimi nawaahidi ushirikiano uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki. (Makofi)