Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kunipatia fursa hii kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini shukrani zangu vilevile ziende kwa Viongozi wetu Wakuu kuanzia kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, vilevile niwashukuru Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi wamekuwa washauri wakubwa na washauri wazuri sana kwa Mheshimiwa Rais. Hata haya mafanikio makubwa unayoyaona ni matokeo ya ushirikiano mzuri wa viongozi wetu na sisi kama Wasaidizi wao tumekuwa tukifata miongozo ambayo wamekuwa wakitupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia hoja kubwa mbili, hoja ya kwanza ni kwa upande wa elimu. Mwaka wa fedha huu unaokuja Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu anatarajia kupitia hotuba ya bajeti ya TAMISEMI tutajenga shule nyingine mpya 234 nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa unaona haya ni mafanikio makubwa sana, mwaka jana tulijenga 232, Mwaka wa Fedha 2022/2023 tunajenga 234, kwa hiyo ndani ya miaka miwili tu ya Mheshimiwa Rais tutakuwa na shule 466, kwa hiyo ni mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani hapa kuna shule zile za kimkoa, mwaka jana tulijenga shule 10 ambazo zinaendelea na ujenzi shule 10 za kimkoa za wasichana na mwaka huu vilevile tumetenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa shule 10 nyingine za kimkoa kwa wasichana katika mikoa 10 nchini, kwa hiyo ni kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu kupitia bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Rais anakusudia vilevile kujenga madarasa zaidi ya 7,600 mapya nchi nzima, lengo lake ni kuona kwamba mwaka huu tunatarajia watoto wa Darasa la Saba watamaliza zaidi ya Milioni Moja Laki Tano na Elfu Sitini, sasa kwa wastani wa pass rate ya asilimia 80 mpaka asilimia 85 ambayo imekuwepo kwa miaka mitano mfululizo, tunatarajia wanafunzi zaidi ya Milioni Moja na Laki Mbili watakwenda kujiunga na kidato cha kwanza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais bado anaendelea na azma yake ya kuhakikisha hakuna mtanzania yoyote anabaki nyumbani kwa kukosa nafasi ya shule. Kwa hiyo, bajeti hii itakapopita maana yake tunakwenda kutekeleza hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi Mheshimiwa Rais amezingatia maombi ya Waheshimiwa Wabunge wengi ambao walikuwa wameyatoa hapa, kwamba tumekuwa na upungufu ndiyo bado tunahitaji nyumba za walimu maeneo ya pembezoni lakini mwaka huu kupitia bajeti yetu tumetenga Bilioni 81.48 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za misingi na sekondari nchini. Kwa hiyo, unaona ni kazi njema na nzuri ambayo inakwenda kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia bajeti hii tutaendelea kukarabati shule kongwe za msingi zile ambazo zimeainishwa katika maeneo mengi. Tumezitambua nyingi lakini kwa awamu hii ya kwanza tutaanza karibu na shule 100 na tuna miradi mingi ambayo tutaipeleka kwa ajili ya kukarabati shule, kujenga madarasa mapya pamoja na kumalizia yale ambayo wananchi wameweka nguvu zao. Kwa hiyo miradi kama SEQUIP, EP4R, GPE LENS yote ni sehemu ya miradi ya kuhakikisha kwamba kwenye upande wa elimu tunatekeleza vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliona niliseme hili ili Waheshimiwa Wabunge watambue kabisa kwamba tunapokwenda kupitisha bajeti hii maana yake tunakwenda kupeleka haya maono ambayo Mheshimiwa Rais anayo kwa nchi yetu. Kwa hiyo, mpaka itakapofika 2025 ninaamini kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kila Mbunge ataacha alama katika Jimbo lake na atakuwa na kitu cha kusema. Kwa hiyo, niseme tu maono haya ya viongozi wetu wakubwa yataleta tija kwenye hili Taifa kuliko kipindi chochote ambacho kimewahi kutokea katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ni kwenye upande wa barabara tumeona kabisa kwamba, moja Mheshimiwa Rais ametuongezea fedha nyingi sana kwa mara ya kwanza na ndiyo maana unaona hata Wabunge wengi safari hii wamepongeza upande wa TARURA kwa sababu TARURA kwa umri wake TARURA imeanzishwa mwaka 2017 mwaka huu ndiyo itakuwa inatimiza mwaka wa tano tangu kuanzishwa kwake. Kwa hiyo, kwa mara ya kwanza mwaka jana walau imepata bajeti ambayo imewafikia Majimbo yote kwa hiyo, vivyo hivyo hata mwaka huu tutafika katika maeneo yote nchini na tutahakikisha yale maeneo korofi na moja ya mkakati wa kwanza ambao tulionao ni kuhakikisha tunakwenda kurekebisha madaraja korofi katika maeneo yote ambayo tumeyafanyia tathmini hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu cha kwanza ni kuhakikisha tunawaunganisha wananchi wetu kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Pili ni kuhakikisha kwamba maeneo korofi yote yale na yenyewe yanafikiwa kama ambavyo tumekuwa tukikusudia. Kwa hiyo, tutakachokifanya ni kuhakikisha tunakwenda kusimamia vizuri fedha ambayo itapitishwa na hili Bunge na sisi hapa pamoja na Mheshimiwa Waziri wetu Bashungwa tumekubaliana tu kwamba, moja wa wajibu wetu ni kuhakikisha tunazunguka kila eneo nchi hii na tutafika karibu Majimbo yote ndani ya Mwaka mmoja ili kuangalia value for money na kuangalia kazi inafanyika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kabisa huo uwezo tunao, hiyo nguvu ya kufanya hiyo kazi tunayo kwa sababu Mheshimiwa Rais ametuamini na ametuwezesha kufanya hii kazi kwa urahisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Bunge lako Tukufu liweze kutupitishia hii bajeti ili iende ikatekeleze yale ambayo yamekusudiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na yale ambayo Mheshimiwa Rais pamoja na Wasaidizi wake kwa maana ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wamekusudia kwa ajili ya Watanzania naisi tuahidi tu kwamba tutafanya kazi kwa uaminifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwa umuhimu mkubwa nimshukuru sana Mheshimiwa Bashungwa sisi Wasaidizi wake amekuwa akitupa ushirikiano mzuri kabisa, kiukweli kabisa tumekuwa tukijifunza sana kutoka kwake ni Waziri ambaye anasikiliza, Waziri ambaye hajinyanyui, kwa hiyo ukija kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI pale utaona kama wote ni Mawaziri lakini kumbe yeye ndiye Waziri wetu na sisi ni Wasaidizi wake, kwa hiyo anatuheshimisha sana, kwa hivyo nimpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kabisa kwamba kwa kuwa tunae hapa tutafanya mambo mengi, tuwakaribishe sana Waheshimiwa Wabunge wakati wowote muda wowote mkiwa na jambo lolote, sisi tuko tayari kufanya kazi kwa ukaribu na Bunge hili tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tunaamini bila Bunge hili mambo mengi hayatakwenda kwa hiyo hilo tuliona tuliseme hapa. Mwisho tunalipongeza Bunge lako tukufu, mjadala wa TAMISEMI kwa hizi siku zote ambazo zimejadiliwa ni mjadala ambao ulikuwa wenye mantiki, uliokuwa unaonyesha dira umetukosoa vizuri na kutupa mwelekeo, nasi tumekubaliana hapa kwamba yale yote ambayo yamejadiliwa hapa tumeyapokea tutayafanyia kazi na yale ambayo kama kuna mtu analo kwa wakati wowote aje kwetu tutalipokea. Kwa hiyo, haya nimeyasema kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)