Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kuzindua Royal Tour ile juzi tarehe 18. Niseme kweli amekuwa President celebrity, wale walioangalia waliona ilivyopendeza na jinsi ambavyo alituuza vizuri kwenye interview aliyofanya kule New York. Kwa hiyo tunampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze kwa kuwa na timu nzuri ya Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi wengine Serikalini ambao wanatuwezesha sisi Wabunge kutembea kifua mbele na kusema kwamba kweli kazi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, nimpongeze kipekee Waziri wa TAMISEMI na Manaibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya, nimpongeze Katibu Mkuu kama wenzangu walivyosema, kwa sababu anafanya kazi iliyotukuka sana na hatuna cha kusema isipokuwa kuwaombea Mungu waweze kuendelea wakiwa na afya, wakifanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuende kwenye Jimbo langu. Kwanza niseme kwamba kuna dharura, TARURA wana dharura kule kwetu. Mheshimiwa Spika alitoa tamko hapa akasema TARURA wafanye tathmini katika Sitting iliyopita, wakafanya tathmini. Lakini nakwambia ukienda Vunjo ambako mvua zimeendelea kunyesha toka wakati ule na hazijaisha mpaka sasa, barabara zote za vijijini kwenye Kata zote za Mwika, Mamba, Marangu, Makuyuni, Kahe, Kirua Vunjo, Kilema, kule barabara zote za vijijini hazipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimepita mimi mwenyewe nikashindwa kupita nikaamua kuja kujificha hapa Dodoma, lakini ukweli hali ni ngumu, naomba tukafanye tathmini tena tuone kwenye maeneo haya ya vijijini kule ambako mvua zimeendelea kunyesha kwa fujo ni kitu gani tutafanya ili watu waweze kupita. Imekuwa matope wakati TARURA ilikuwa imetengeneza vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana yule mratibu wetu anaitwa Olota, kwamba walifanya kazi nzuri sana mwezi Novemba na Desemba sasa ukienda kupita ni pa kurudia, ninaamini lazima tutafute mbinu mpya ya kutengeneza barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujaribu kutumia mawe zaidi, tutumie Local Based Contactors ili watumie vijana wale wa kwetu, wapasue mawe tuweke mawe kwenye yale maeneo ambayo ni korofi sana ili barabara ziweze kukaa angalau kwa miezi michache. Tukijenga kwa mawe badala ya kutumia hizi traditional methods tunaweza tukajenga kwa bei nafuu lakini pia kwa kitu ambacho ni sustainable. Hivi tunavyofanya tunacheza, naomba tufanye kitu kama hicho na tutumie hizi force accounts, tuache kusema kwamba TARURA hawawezi kutumia force account. Force account inakuwa ni cheaper na tulifanya tathmini sisi tukapata mambo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia tunatoa pongezi na shukrani kwa Mheshimiwa Rais na Wizara hii ilivyotutumia fedha, tumeweza kukarabati Kituo cha Kirua Vunjo, kimekuwa na majengo sasa ya upasuaji. Tumepata fedha Shilingi Milioni 250 kwenye kituo cha Marangu ambacho hakitaisha ni nusu tu. Naomba hizo hela zilizobaki tupate ili tukamilishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kingine OPD ambapo tumeahidiwa kwamba kimepandishwa hadhi kikawa kituo cha afya, kilikuwa ni zahanati, basi kipate Shilingi Milioni 500 tuweze kukamilisha na penyewe tuwe na kituo cha pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha Mwika ambacho pia ni kituo kongwe sana, kituo cha miaka hiyo ya Hamsini mpaka leo hakijapata ukarabati, hakijapata majengo yale ambayo ni stahiki kuitwa kituo cha afya. Naomba sana Wizara hii sasa ikaangalie hilo katika mwaka huu unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kule kwetu Kilimanjaro kwa ujumla na Vunjo in particular utakuta kwamba shule zote za msingi na sekondari ni kongwe kabisa. Sasa wale vijana wanaosoma kwenye shule kongwe wakaona tumejenga madarasa 32 juzi, tumepewa chini ya UVIKO wanakwenda kutazama na kusema Mungu wangu, hivi hawa wenzetu wanaishi kwenye dunia ya Marekani na sisi tunaishi jehanamu au namna gani? Kwa sababu zile shule zao hazina vyoo, hazina miundombinu, ni za kukarabati kabisa, na ninaomba Serikali iende kwa awamu. Tuende kwa kuangalia ni zipi kongwe Zaidi, zilizojengwa miaka ya sitini, miaka ya sabini, lakini twende hivyo kwa tabaka ili tuweze kwenda kukarabati kufuatia age za shule zikoje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba kama tusipoinua hadhi ya shule hizi za zamani wakati tumewaonesha kwamba kuna uwezekano wa kujenga shule nzuri, madarasa mazuri, wale vijana wanaosoma kwenye shule ambazo zimeoza kabisa wanasononeka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni hili suala zima la mikopo. Mimi niseme hivi, kigezo kikubwa cha mafanikio ya mchakato au mkakati wowote wa Serikali kutoa mikopo kuwezesha wananchi ni ili mikopo inayotolewa kuzunguka, maana yake kurejeshwa, ili iweze kuzunguka kwa watu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini inavyoonekana huu mchakato wa kulenga vikundi duniani kote haufanyi kazi, hata kule benki tulifanya, hai-work. It doesn’t work. Tutumie mbinu mpya sasa kwa sababu kuna njia za kidigitali za kuweza kujua ni nani mhitaji na mwenye mradi mzuri wa kuweza ku-sustain, tuweze kutumia methods ambazo zinatumia big data logistics tuweze kutoa mikopo hiyo kwa wale watu, hata mmoja mmoja utaona kwamba zinarejeshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutoa kwa groups, groups ni vigumu sana kuwajibika, uwajibikaji ndani ya group inakuwa vigumu sana kusimamia, kwa sababu mmoja aki- default na mwingine ana-default, na mwingine na mwingine. Kwa hiyo naomba sana tuangalie, tutathmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mawazo ya namna gani ya kufanya pengine tuangalie upya kabisa, hata tuwe na mjadala mzima ili uweze kusema twende wapi kwenye hili suala zima ambalo ni zuri la kuwezesha wanawake, vijana, walemavu, pengine baadaye tuweke na wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)