Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya nzuri na leo hii nikaweza kusimama katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, pia nijielekeze katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwenye suala la afya. Jimbo langu la Mtwara Vijijini nina Kata 21, Vijiji 110. Jambo cha kusikitisha ni kwamba nina zahanati 28 tu, nina vituo vya afya vitatu. Hivyo, niiombe sana Serikali ituongezee vituo vya afya pamoja na zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hospitali yetu pale ya Wilaya Nanguruwe. Hospitali hii imekuwa na uhaba mkubwa sana wa watumishi. Kwa mfano ukiangalia upande wa maabara katika hospitali hii ya Wilaya tuna mtu mmoja tu pale ambaye anatoa huduma, lakini ukija kwenye suala la Mfamasia, ngazi ya degree hatuna Mfamasia kabisa, lakini ngazi ya diploma tuna Mfamasia mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hii ya wilaya ambayo ipo Nanguruwe inahudumia watu wengi sana lakini kuna Manesi Wanane tu katika hospitali hii. Hivyo, niiombe sana Serikali ituongezee watumishi wa kutosha katika hospitali yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali hii bado inaendelea kujengwa, kuna wodi ambazo zinajengwa, idadi ya watumishi ni chache. Kwa hiyo ninaomba tuongezewe watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zahanati, katika Kata ya Mpapura Kijiji cha Nanyani, kuna ujenzi wa zahanati pale tokea Julai, 2017, lakini mpaka leo takribani miaka minne mitano, zahanati ile imekwisha na imejengwa vizuri lakini haijafunguliwa mpaka leo. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili, ile zahanati sasa hivi inaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimetembelea, mchwa wameanza kula katika milango na madirisha. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri lichukue hili, zahanati hii ianze kufanya kazi ili wananchi waweze kupata huduma pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja kwenye suala la TARURA. TARURA ni muhimu sana katika barabara zetu, lakini changamoto kubwa ambayo inatokea katika TARURA ni ukosefu wa fedha, wana shida ya fedha ya kutengeneza barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu za vijijini ni mbovu mno, hasa katika Jimbo langu. Barabara ni mbovu na hazipitiki kabisa. Barabara nyingine zimejifunga kutokana na mvua kubwa ambazo zilikuwa zinanyesha. Kwa mfano, barabara ya Mkunwa – Namayakata. Barabara hii ni mbovu nayo, haipitiki. Pia kuna barabara inayohudumia Wilaya ya Tandahimba – Newala, barabara hii pia ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Msanga Mkuu, ni kilometa 17. Barabara hii inahudumia vijiji takribani vinne; Ziwani, Nalingu, Msakara pamoja na Mkubiru. Barabara hii nayo imekuwa ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo barabara nyingine ambayo nayo imejifunga kabisa, yaani haipitiki, wa huku wa huku, wa huko wa huko. Kwa hiyo, naomba barabara hii iangaliwe. Barabara ambayo inaanzia Naumbu – Kabisela. Barabara hii nayo ni mbovu, ni kilometa 21.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni barabara ya Dihimba (kilomita 17) nayo ni mbovu sana. Hivyo, niombe sana Serikali na Wizara mlichukue hili muweze kututengenezea barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu kwa haraka haraka. katika Jimbo langu la Mtwara Vijijini tuna changamoto kubwa sana katika Sekta hii ya Elimu. Tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi kwa shule za msingi na sekondari, pia tuna changamoto kubwa za nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu hali ni mbaya mno. Nyumba za walimu hakuna. Kwa mfano, Shule ya Msingi Mnete, hakuna nyumba za walimu. Mdui, Nanyati, Nanyani, Milumba hakuna nyumba za walimu. Nina vijiji 110…

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Mchango mwingine nitaleta kwa maandishi. (Makofi)