Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii awali ya yote nianze kwa kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais na Mwenyekiti wa CCM, Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa kumpongeza yeye naamini kabisa nimewapongeza pia wateule wake wote pamoja na Watendaji na Wataalam wanaomsaidia kazi, hasa ukizingatia kwamba Wizara hii tunayoijadili ni ofisi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi nzuri inafanyika Tanzania, Watanzania wanaona na dunia inaona. Jimboni kwangu Mwanga pia kazi inafanyika vizuri. Mimi Mbunge wa Mwanga ninaiona kazi na wananchi wangu wa Mwanga pia wanaona kazi nzuri inayofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mwanga siyo Wilaya changa sana, ina umri wa takribani miaka 44 sasa, lakini kwa mara ya kwanza sasa tumepata jengo la utawala la Halmashauri ambalo tulikuwa hatujapata siku zote. Tumepata katika maana ya kwamba tumetengewa fedha Shilingi Bilioni Moja. Tumetengewa pia Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya. Kwa haya yote mawili naishukuru Serikali pia ninatoa wito kwamba kule tumeshaanza kazi tayari ya maandalizi, kiwanja kipo, tunaanza kusafisha na kukusanya vifaa.

Kwa hiyo, tunaomba Wizara isituangushe, tupate hizo fedha kwa wakati ili tuweze kukamilisha hii miradi kama ambavyo wananchi wanaitarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanga kuna changamoto ya vyanzo vya mapato. Kwa ajili hiyo tuliamua kubuni miradi ya kimkakati ili kuweza kuongeza mapato. Mradi wa kwanza ni stendi na kwa bahati nzuri sana tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu alipokuja Kilimanjaro tulizungumzia suala hilo na akalibariki, kwa hiyo ile ni ahadi ya Rais. Tunaomba tupatiwe stendi ya kisasa Mwanga kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa pili wa kimkakati ni soko la samaki. Kwa kutumia mapato ya ndani tumekarabati jengo la chakula barafu na kujenga mialo kama 24 hivi. Alipokuja kututembelea aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alivutiwa na ule mradi na akatuahidi barabara ya kufika kwenye lile eneo. Tunaomba ahadi hii kwa sababu ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri na alikuwa na timu ya wataalam ni ahadi ya Serikali, tunaomba itekelezwe ili Mheshimiwa Waziri tutakapokukaribisha kuelekea mwishoni mwa mwaka huu kuja kufungua huo mradi usipate shida ya kufika barabara iweze kukufikisha vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba shule za Kata kwenye Kata mbili ambazo hazikuwa na shule. Tumepata Kata moja ya Kivisini, tunaomba Kata ya Toloha ipate shule kwa sababu ni Kata yenye changamoto za wanyama tembo na wanaoishi kule ni ndugu zetu wa jamii ya kifugaji. Tunatamani shule isogee ili waweze kupata huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto ya shule chakavu kama maeneo mengine yalivyo lakini kipekee naomba niiseme shule moja, Shule ya Msingi ya Ndorwe ambayo ilianguka baada ya kutokea tukio la landslide. Wananchi wamejitahidi wametafuta kiwanja kingine wamesafisha uwanja na wameanza kuweka vifaa. Tuliomba fedha kwenye mfuko wa maafa, tunaomba sana tusaidiwe fedha hizi ili tuweze kukamilisha kwa sababu watoto wanatembea umbali mrefu sana kufuata huduma ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vituo vya afya tuliomba vituo viwili vya kimkakati, tumepata kimoja, tunaomba sana kwamba na hiki kingine tukipate kwa sababu ni changamoto kubwa sana, vituo vya afya ni vichache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nizungumzie suala la ajira. Kwanza nishukuru kwamba tumepata ahadi hiyo ya ajira nyingi katika sekta za elimu na afya. Mwanga tuna Walimu wanaojitolea, upande wa sekondari wako walimu 55 na upande wa shule za msingi walimu 83.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba walimu wale wangeajiriwa palepale, ingetupunguzia mambo kama mawili. Jambo la kwanza, ingetupunguzia gharama za kuwapeleka huko mbali ambako pengine watapata ajira, lakini jambo la pili, hata wao maisha yao yatakwenda vizuri kwa sababu pale wana nyumba hata wakiwa nacho kipato kinaweza kikatosheleza. Kwa hiyo, ninaomba katika kufikiriwa ajira za walimu, wale walimu wanaojitolea Mwanga waajiriwe palepale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba iko sera ya ajira na nini, labda tunazungumzia mambo ya umoja na kadhalika kwamba waende huko na huko, lakini hili sasa ni janga kwa sababu kuna watu wamemaliza chuo mwaka 2015 mpaka leo hawajapata kazi. Wasije wakafikia umri wa kustaafu kabla hawajapata kazi. Tulichukulie kama janga, hawa watu waajiriwe ili waweze kutumia elimu yao ambayo wameipata kwa gharama kubwa kwa ajili ya faida ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hayo tu kwa leo kwa sababu ya muda nisiseme mengi. Nakushukuru sana kwa nafasi hii, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)