Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza kabisa napenda nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha Tanzania inatoka hatua moja kwenda hatua nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda nimpongeze Waziri wa TAMISEMI ndugu yangu Bashungwa kwa kazi kubwa anayoifanya. Mheshimiwa Bashungwa anafanyakazi kubwa kwa kipindi kifupi tu tunaona ni jinsi gani ambavyo anapambana kufuatilia mambo. Ni juzi tu hapa lilitokea tatizo Mwanza kule aka-act mara moja mambo yakaenda vizuri na sasa hivi kuna barua moja inatembea ya mtandaoni taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba kuna Mkurugenzi mmoja ambaye hajatii maelekezo amewekwa pembeni kidogo. Wizara inataka namna hiyo hii Wizara Mheshimiwa Waziri ni Wizara ambayo Wabunge wote tunaitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii itakapokuwa haijafanya vizuri basi sisi sote Wabunge tutakuwa hatujafanya vizuri katika Majimbo yetu, kwa hiyo tukupongeze sana na tutakupa moyo pamoja na kukusaidia ili uweze kufanikisha azma yetu tunayoikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la elimu. Kwanza niishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kweli katika Jimbo langu la Bagamoyo kwa kipindi kifupi tu tumepatiwa madarasa yasiyopungua Shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Tatu. Hii ni kazi kubwa sana ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais na hii imesababisha vile vile katika kipindi kifupi hiki kupata shule mbili za Sekondari mpya kabisa kuna shule ya Sekondari ya Makurunge ambayo ujenzi unaendelea zimepatikana pesa Milioni 600, kuna shule mpya ya Kata ya Nianjema ambayo ujenzi umekamilika na wanafunzi wanaendelea kusoma, kwa hiyo tunazidi kuipongeza sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mama Samia kwa kazi hii kubwa ambayo wanaifanya. Vilevile kuna shule shikizi ambazo tumepatiwa pesa na shule hizi nazo zishaanza kufanyakazi baadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika suala la afya, kuna suala la vifaa tiba. Halmashauri zetu nyingi zina vituo vya afya ambavyo vimejengwa mimi niishukuru Serikali, pale kwangu Bagamyoyo Fukayosi Milioni 500 imepatikana na kituo cha afya kinaendelea kuimarika na kitakamilika muda si mrefu. Lakini tatizo kubwa linalotukabili ni vifaa tiba katika vituo vyetu vya afya hakuna zahanati zetu vile vile hazina vifaa tiba, kwa mfano kituo cha afya cha Matimbwa Yombo hakina vifaa tiba kwa hiyo kinashindwa kufanya kazi vile inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha afya cha Kerege nacho kina changamoto ya vifaa tiba zahanati ya Buma, Kilomo, Zahanati ya Tungutungu Mapinga, Zahanati ya Mkenge, Zahanati ya Kidomole zote hizi zinakumbwa na changamoto kubwa ya vifaa tiba kwa hiyo naiomba sana Wizara izidishe juhudi kuhakikisha kwamba, katika mwaka huu wa bajeti vifaa tiba vinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la TARURA kazi kubwa TARURA wameifanya pesa tulizopata tumefanya mambo makubwa katika Majimbo yetu na mimi kwa upande wangu wa Bagamoyo barabara nyingi sasa hivi ambazo zilikuwa zina matatizo ya kujaa maji na hasa Bagamoyo mjini, maji sasa hivi hayapo kwa sababu barabara zimejengwa kwa kiwango cha mifereji kiasi kwamba maji yanapita na naomba niishauri tu Wizara sasa hivi katika bajeti ijayo basi, tuhakikishe katika barabara zetu tunaimarisha mifereji. Kwa sababu tunapoimarisha mifereji ndiyo barabara nyingi zinadumu lakini tukisema kwamba tunafanya ukarabati wa barabara maji yakijaa yanajaa udongo unaondoka mwakani tunapeleka pesa tena.

Mheshimiwa Spika, kama hizi Bilioni 802 ambazo mmezienga kwa ajili ya TARURA kwa kipindi cha bajeti ijayo mtazifanyia kazi vizuri na mifereji ya barabara itatengenezwa basi itakuwa jambo la kheri na busara kabisa kabisa kwamba barabara zetu nyingi zitapitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la maji RUWASA inajitahidi sana katika suala zima la kusambaza maji vijijini. Mimi kwangu pale Bagamoyo katika Kata ya Fukayose nina mradi wa shilingi milioni 300.000 karibuni na 50,000 lita 75,000 zinajengwa ambazo nina imani wananchi wangu wa vitongoji vya Lusako, Umasaini, Engelo, Mkenge na sehemu zinginezo watapata maji ya kutosha katika kipindi kijacho niipongeze sana Wizara kwa kazi kubwa ambayo mnafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala vilevile la barabara kuna barabara ambazo ni muhimu sana zinakwenda katika mashule pamoja na vituo vya afya na zahanati barabara hizi zipewe kipaumbele katika kuimarishwa kwa sababu wanafunzi wanapata taabu sana wakati wa mvua kwa hiyo katika bajeti hii ijayo Serikali ijitahidi sana kuhakikisha kwamba hizi barabara zinapatiwa kipaumbele na zinaimarishwa, naunga mkono hoja ahsante sana.