Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ikikupendeza kabla Mheshimiwa Simbachawene, Chief Whip hajazungumza, naomba tu nitoe ufafanuzi wa mambo mawili ambayo nimeona ni mazito na ningepata fursa ya kuyasemea hayo ningekuwa nimefarijika sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri unaweza kuzungumza ikiwemo lile la mrundikano wa watu wanakusanywa wengi Dodoma, mfumo kuzima, unaweza ukatumia nafasi hiyo pia kufafanua kidogo. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi nianze na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa bajeti mwaka jana Waheshimiwa Wabunge walitoa hoja nzito na za msingi kuhusu mfumo mzima wa recruitment kwenye Sekretarieti ya Ajira nchini na ilikuwa imejitokeza sasa kama ni mazoea. Sekretarieti inapotangaza ajira, labda mahitaji ya ajira zinazotangazwa ni 50, lakini maombi yaliyokuwa yanapokelewa na Sekretarieti ya Ajira yalikuwa yanafika maombi labda 2,000 na watoto wetu wa Kitanzania wote walikuwa wanakusanywa hapa Dodoma kwa ajili ya kufanya huo usaili. Wanakuja watoto 2,000 lakini wanaohitajika walikuwa ni watoto 50 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako wakati wa bajeti mwaka jana Waheshimiwa Wabunge waliotoa hoja na kupitia Kamati ya USEMI walitupa maelekezo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuona namna gani tunaweza kutatua tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliarifu Bunge lako tukufu kwamba Serikali imechukua hatua na hatua zilizochukuliwa ni hizi zifuatazo; hatua ya kwanza, tumeamua kuanza kupeleka vituo vya usaili kwenye kanda ili kutoa haki kwa watoto wote wa Kitanzania kwenye kanda husika. Kwa hiyo, sasa hivi interview zetu zimeanza kufanyika kwenye kanda. (Makofi)

Pili, pamoja na kupeleka usaili kwenye kanda, bado watoto wanaokuja kwenye interview ni wengi, wanafaulu wengi, lakini nafasi zinakuwa ni chache. Serikali imesikiliza pia maelekezo ya Bunge, tumeamua kuhuisha database ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ilikuwa inadumu kwa miezi sita, sasa hivi database hiyo kwa Tangazo la Serikali Namba 580 itakuwa inadumu kwa mwaka mmoja wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa tumekwisha kuiagiza Sekretarieti, wale watoto wanaokuwa wamefaulu usaili kupitia kwenye kanda zote, wawekwe kwenye database. Hao 50 kwa mfano waliohitajika wachukuliwe, lakini wale wengine waliofaulu waachwe, inapotokea nafasi au fursa inayotokana na kufanana na hiyo, badala ya kuwaita tena watoto kwenye usaili, wachukuliwe wale wa kwenye database na wapewe hizo fursa.

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti,...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda tu kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Waziri ambaye ninamheshimu sana na yeye anajua. Tunazungumza habari ya usalama wa nchi; usalama wa nchi hauwezi kuwepo kama hakuna uwiano wa ajira katika ofisi za umma kwa sura nzima ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuweka utaratibu ya kuwa na pass mark ya mkoa mmoja ukatofautiana na mkoa mwingine wakati wake ilikuwa ni kuhakikisha kwamba kila mkoa nchi hii unapata fursa ya kwenda sekondari na hatimaye vyuo na vyuo vikuu ili ofisi za umma ziwe na sura ya nchi nzima. Hali ilivyo sasa ni mbaya na mimi Mheshimiwa Waziri naweza kushuhudia baadhi ya mikoa niliyofanya utafiti ajira nyingine zilizokuja zilikuwa zinakuja za kutoka sehemu moja ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sura iliyo mbaya zaidi ni kwamba vyombo vya ulinzi na usalama wanapokwenda kuchukua baadhi ya watu, wanachukua watu kutokana na waliokuwa police line, waliokuwa wanafanya kazi polisi wanachukua watoto wao kule kule, waliokuwa jeshini wanachukua watu wao kule kule, wengine wenye nafasi Serikalini wanachukua watu. Mkitaka kapitieni orodha ya Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata, Makatibu Tarafa walioajiriwa katika miaka hii mitatu, minne, mitano; mtakuta hakuna sura ya nchi, kuna ukabila, kuna ueneo na kuna upendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili mbele ya Bunge lako tukufu mkitaka nitakuja kuthibitisha. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa toa taarifa sasa. Mheshimiwa Waziri, unapokea taarifa? Endelea. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba kwa muda mrefu takribani miaka sita tumepata tatizo kubwa la ajira kwa sababu ya Serikali kutoajiri kwa miaka sita, na hivyo hali ambayo imejitokeza kwa sasa ni vijana wetu wengi wako mtaani ambao wamesomeshwa na Serikali hii na walikuwa na matumaini makubwa ya kujiunga na utumishi wa umma ili waweze kusaidia kujenga Taifa lao kupitia kwenye utumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge kwanza tumshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu alipoingia tu aliamua kwanza kufungua fursa za ajira nchi nzima, hilo ni jambo moja linaloonesha utayari kwanza wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposimama leo mpaka tarehe 31 Januari, 2023 Mheshimiwa Rais aliridhia vibali 55,249 vya ajira ili viweze kutolewa na tatizo lianze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kufunguliwa kwa ajira hizo, sasa ndio tunaanza kuona uhitaji wa ajira kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa usawa. Naomba nikubaliane na Wabunge wanaochangia jambo hili, commitment yetu ya Serikali itaendelea kupokea huo ushauri, kufuatilia kwa kina kuona ni taasisi zipi ambazo zimekuwa zikifanya ajira kwa upendeleo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, nakuongeza dakika moja na nusu.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tutafanya utafiti na kama wale tuliowapa dhamana ya kusimamia mchakato wa ajira tutakapogundua wanatumia vibaya dhamana zao, tutachukua hatua kali zinazotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Ajira nchini inataka kutoa fursa sawa kwa wote kwa kuzingatia njia ya ushindani, aliyepewa apate bila kupendelea mtu yeyote. Kwa hiyo, hilo tutalifuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ya mjadala pia wa bajeti wa kuamua kushirikisha kanda zote nchini zipate fursa, nadhani pia kuna kila haja ya kuipongeza Serikali kwa kufanya maamuzi ya kupeleka sasa usaili kwenye kanda na ninawahakikishia kwamba malengo yetu ni kuhakikisha usaili sasa unafika katika ngazi ya kila mkoa huko huko kwenye Taifa letu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunasema hata hili nililolizungumza la kuwa na database ya mwaka mmoja itatusaidia sana kupunguza kadhia hii kwenye mfumo mzima wa recruitment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila ni lazima tukubaliane Serikali sisi peke yetu hatuwezi tukatoa ajira kwa wasomi wote kwenye nchi yetu ya Tanzania na ndio maana tumekubaliana hapa kupitia Wizara nyingine Uwekezaji, miradi ya kimkakati na maeneo mengine, tukisaidiana wote kutoa ajira, nadhani tatizo hili na wimbi hili la kutokupatikana kwa ajira kwa miaka sita litakuwa limeondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawahakikishia Waheshimiwa Wabunge jambo hili tunalisimamia vizuri na mwezi Februari, 2023, tunataraji kuchukua watoto 1,769 kutoka kwenye database na kuondoa ile ya kuwarudisha rudisha watoto wengi kuja kufanya interview na wakati walikwishafaulu na wapo kwenye database. Kazi yetu itakuwa ni kuwachukua na kuwapangia majukumu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja, niwaombe Waheshimiwa Wabunge muendelee kutushauri, ninyi mna uwezo wa kutupa ushauri ni namna gani tunaweza kufanya ili kuboresha mchakato wa ajira katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)