Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Sophia Mattayo Simba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu ili na mimi niweze kutoa yangu machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na utukufu kwa kuniwezesha kuwa mmoja wenu katika Bunge hili. Aidha, nawapongeza Wabunge wenzangu ambao wamefanikiwa kuingia katika Bunge hili. Nakupongeza wewe kwa nafasi hiyo, nampongeza pia Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wenzio, nawatakia kila la kheri katika kazi hiyo na najua mnaimudu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mimi sikupata nafasi ya kuzungumza wakati wa kuzungumzia hotuba ya Mheshimiwa Rais, naomba kidogo nichukue nafasi hii na mimi kumpongeza Mheshimwia Rais, kwanza kwa ushindi mnono alioupata lakini pia kwa hotuba nzuri sana aliyoitoa ambayo imegusa nyoyo zetu sisi na wananchi karibu wote. Kwa kweli Mheshimiwa Rais ameonyesha uwezo mkubwa na ameonyesha ukweli wake. Kwenye kampeni alikuwa akisema nipeni nifanye kazi, msema kweli mpenzi wa Mungu na kweli tunamuona anatenda yale ambayo alisema angefanya. (Makofi)
Mheshimwia Mwenyekiti, kabla sijaingia kwenye Mpango, napenda nimfahamishe kijana wangu ambaye alizungumza hapo awali, nadhani ni Mbunge wa Liwale, ni kijana madogo kwa hiyo anahitaji kusaidiwa. Amenigusa alivyoanza kuzungumzia Mtwara Corridor, misamiati, kaulimbiu zinazotolewa, Mheshimiwa Rais Mkapa amekuja na Mtwara Corridor ipo wapi, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amekuja na maisha bora yapo wapi. Mheshimiwa Mbunge pengine kwa ajili ya umri wako, leo unaizungumzia Mtwara Corridor! Sasa hivi wenyewe wa Mtwara wanasema Mtwara kuchele. (Makofi)
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mtwara Corridor isingewezekana bila ya kuwa na miundombinu na moja ni barabara. Wakati Mheshimiwa Mkapa akizungumzia Mtwara Corridor hata barabara ilikuwa hakuna, daraja lile la Mkapa lilikuwa halipo na limepewa jina sahihi kabisa, limejengwa katika ku-facilitate Mtwara Corridor. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa ukienda Mtwara siku nyingine unaweza ukalala mwezi mzima daraja la Mkapa hujafika kule. Leo Mheshimiwa Mbunge najua kwa umri wako pengine wakati ule hujawahi hata kusafiri, lakini mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Kazi nzuri imefanywa na Mtwara Corridor, ule mradi wote wa gesi umeanzia huko kwa Mkapa. Maendeleo ni mchakato, maendeleo hayaji siku moja. Mchakato ule ndiyo sasa unaonekana kule Mtwara, viwanda vinajengwa na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, inauma sana ukimsikia mtu anasema maisha bora kwa Mtanzania ilikuwa inapitapita tu, kweli tulikuwa hivi, hata Bunge halikuwa kubwa kama hili. Sekondari za Kata mara hii mmezisahau, vituo vya afya, zahanati kila kona, nchi hii imefunguliwa kwa kuwa na mtandao wa barabara, kama siyo maisha bora kwa kila mwananchi ni nini hiyo? Isitoshe angalieni UDOM hiyo ni kazi ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wake university ngapi zimeongezeka hapa nchini? Ndiko tunakoenda kuchukua maisha bora kwa kila Mtanzania ndugu zangu. Pamoja na simu zilizokuwa mifukoni kwa kila mwananchi yale yote ni matokeo mazuri ya maisha bora kwa kila Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi kwenye vipaumbele. Kwanza nampongeza sana Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri aliyoifanya na wameweka vipaumbele vizuri. Nataka nimkumbushe kwamba Mheshimiwa Rais alipokuwa akisoma hotuba yake alisema tutakamilisha miradi ya mwanzo na kuanzisha mipya. Hivyo basi, ni bora tukakumbuka miradi mikubwa ambayo ilikuwepo kabla ya Mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni suala zito sana duniani, huko tunakokwenda ukiangalia mabadiliko ya tabianchi, wataalam wanasema vita ya tatu itatokea kutokana na kugombea maji.
Kwa hiyo, miradi mikubwa ya maji ambayo napenda kuikumbusha, napenda wakumbuke kwamba zaidi ya miaka kumi iliyopita kuna mradi mkubwa wa maji wa Kipera, tuliambiwa kule Kibada kuna bahari ya maji kule chini, mradi ule upo wapi? Tunakazania Mradi wa Mto Ruvu lakini kuna bwawa la Kidunda silioni! Bwawa la Kidunda ni lazima lijengwe, vinginevyo tunaachia maji yanaenda baharini, bahari haina shida ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mikubwa ya Ziwa Viktoria kupeleka maji Lamadi, Magu na Tabora. Hebu tuhakikishe miradi hii ya maji na mengine inakamilika. Maji ni suala linalomhusu mwanamke na watoto, mwanamke anaamka asubuhi sana kutafuta maji, watoto wengine hawaendi shule ili waende kutafuta maji. Kwa hiyo, sisi wanawake linatugusa sana suala hili la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni la elimu. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuja na utaratibu wa elimu bure. Ndugu zangu kama nilivyosema maendeleo ni mchakato, elimu bure tulianza kwanza kujenga shule nyingi sasa wengi wataweza kusoma kwa elimu bure. Tatizo langu tunahitaji kuwa na elimu bora (quality education). Hiyo quality education isianzie sekondari tunahitaji elimu ya awali iweze kujenga msingi bora kwa watoto waweze kujiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi ilivyo sasa hivi mtu anamaliza university hajiamini, lakini ameanza toka kule kwenye msingi kujifunza kwa uoga. Kwa hiyo, naomba sana kwenye elimu tuwasaidie walimu kwa kuwaendeleza zaidi, tupate walimu bora ili watoto waweze kupata elimu bora zaidi na hasa elimu ya awali. Mimi naamini sana akitoka na elimu nzuri kwenye elimu ya awali hawatapata tabu huko watakapokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. (Makofi)