Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hoja hii.

Kwanza nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wote wa Kamati zote tatu kwa taarifa zao. Niseme tu kwamba mapendekezo yote yanayohusu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumeyapokea na tunaahidi kwamba tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ufafanuzi kwa maeneo mawili ama matatu kulingana na muda na naomba nianze na eneo la kurejesha majukumu ya ukarabati, ujenzi na kazi zote za viwanja vya ndege kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwenda Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge, CAG, Kamati ya Miundo Mbinu lakini pia na Kamati ya PAC. Niwajulishe Waheshimiwa Wabunge kwamba tayari kazi hiyo imeshaanza na niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba shughuli za TAA kwenda TANROADS zilikuwa ni presidential decree na hii ilikuwa ni baada ya kuona shughuli nyingi wakati ziko chini ya TAA zilikuwa haziendi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tayari wataalam wameshatoa mapendekezo ya namna ya kuhamisha majukumu kutoka TANROADS kwenda TAA kwa hatua kwa sababu ziko kazi ambazo tayari zinaendelea na hatuwezi leo tukaziondoa ghafla. Kitakachoweza kutokea kama tutakifanya hicho, ndio kama walivyosema baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna viwanja vilisimama kwa sababu wakati TAA inatekeleza hiyo miradi ama imeshaingia mikataba tukafanya mabadiliko. Kwa hiyo tutahakikisha hilo halifanyiki na wataalam wameshatoa mapendekezo yao, hatua za kuanza kuchukua, hatua baada ya hatua na tunategemea kwamba zile fedha ama zile kazi ambazo zitafanyika kwa fedha hasa ya Tanzania kwa maana haina wahisani, miradi yote tutakayoanza kutekeleza itaanza hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengine watakuwa mashahidi kwamba hata sasa hivi tumeanza, pale ambapo kunakuwa na kazi wote wanakuwepo kwa ajili ya kuanza taratibu ya kuwajengea uwezo na uzoefu. Hilo kwa upande wa Serikali halina tatizo, tumeshalifanyia kazi na tunaamini kadri tunavyokwenda shughuli zote zitahamia TAA.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu bado vile viwanja vyote tulivyovijenga kama Msalato, Songea vimejengwa na hawa TANROADS na wataalam kwa hiyo tunategemea baada ya hapo pia kutakuwa na kuhamisha wataalam ambao wamepata uzoefu kutoka TANROADS kwenda kule TAA ili kuwajengea uzoefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo kuna Mbunge amelichangia kwa nguvu kuhusu TEMESA. Tunatambua hii taasisi ni muhimu sana kwa sababu ndio inayoshughulikia magari ya Serikali ya Viongozi lakini pia na vivuko. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inapitia hii Taasisi na majukumu yake ili iweze kufanya kazi vizuri zaidi. Kwa hiyo, tumelipokea Kamati ilishauri, lakini pia Wabunge wameshauri na wameendelea kushauri na sisi tunasema tumeshaona kwamba, kuna haja kubwa ya kuangalia muundo wake, majukumu yake na utendaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ilikuwa ni taarifa na mapendekezo ya kiufundi na ufanisi. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara tunaangalia na kuweka mifumo imara sasa hivi ya jinsi ya kuangalia upungufu unaojitokeza wa kiufundi na hasa ya kiuhandisi yanayosababisha baadhi ya kazi zetu kufanyika chini ya kiwango. Niwahakikshie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tumeliona hilo, tumelichukua, lakini tumeshaanza kuweka mifumo ambayo itahakikisha kwamba tunazuia hilo lisitokee na pale ambapo linatokea, hatua kubwa sana zinachukuliwa za kisheria na kinidhamu kwa wale ambao watakuwa wamesababisha kufanyika kwa kazi za kiufundi chini ya kiwango kama ambavyo ripoti imesema na tarifa ya PAC imesema.

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala mengine ambayo yameongelewa hasa ya ulipaji wa certificate, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameelezea vizuri, kwa hiyo hilo naomba nisilieleze tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)