Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuja hapa leo kujadili ripoti tatu mbazo zote zinahusu usimamizi wa fedha za walipa kodi. Sisi kama Bunge anayetusaidia kwenda kwenye ukaguzi kwenye taasisi zetu na mashirika na halmashauri zetu zote nchini ni CAG ambaye kwa mujibu wa Katiba tumempa mamlaka hiyo kama Bunge, lakini na sisi Bunge tuna haki ya kuhoji na kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesimama hapa kama Wabunge kwa Kanuni mbalimbali za Bunge na sisi hapa tupo kwa niaba ya wananchi wa Tanzania nzima, kwa hiyo tunapoleta maoni yetu hapa si maoni ya sisi kama Wabunge tulipo huku ndani, ni maoni ya wananchi waliotutuma kuja kuwawakilisha. Kwa hiyo, tunaposema ubadhilifu wa fedha zinazotokea katika Serikali, mambo hayaendi sawa katika Serikali, si kama sisi Wabunge ndio tunayasema ni wananchi wanasema mambo hayaendi sawa. kwa hiyo tunaomba tueleweke kwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ripoti zote za CAG kila mwaka tunapokuja hapa, hata hizi ripoti za Kamati za Fedha, hatuwezi kwenda hata siku moja tukasema Serikali hakuna sehemu ambapo tumepoteza au tumepata hasara. Kila siku tunapata hasara na hasara kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika mchango wangu nataka tuishauri Serikali; tuna miradi mikubwa ambayo Serikali inatafuta fedha, tuna Mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambao tunaweka matrilioni ya fedha, tuna mradi mkubwa wa SGR. Kama tusipoweka mipango madhubuti ya usimamizi wa fedha hata hizi fedha tutakuja tutakaguliwa tena tutaambiwa zimepigwa na bado Watanzania wataendelea kuumia. Katika ripoti ya CAG ambayo leo tumekuja kuijadili hapa, kuna changamoto kubwa ya riba ambazo tunalipa kwa wakandarasi; na hii yote inasababishwa na uzembe wa watumishi wetu katika Wizara na taasisi mbali mbali. Sasa wewe unakuta mkandarasi una mcheleweshea malipo mpaka siku 205, halafu tunakwenda kulipa the deference ya riba ya zaidi ya bilioni 11 halafu bado watu tunakuja hapa, mnasema kama hatuwezi tujadili masuala ya uganga wa kienyeji, tukae kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge kama tusipojisimamia sisi wenyewe kuna siku hapa mtakuja mtukanwe na bado mtapiga makofi. Kwa hiyo, mimi niwaombe tunapokwenda kuishauri Serikali si kwa nia mbaya ni kuisaidia Serikali iweze kufanya kazi. Sasa waganga wa kienyeji tupo, sasa tunawapa mkeka. Wizara ya Fedha, hizi variations zote ambazo tunazisema; wakandarasi kulipwa kwa kuchelewa, tunakwenda kulipa fedha nyingi, zote zinasababishwa na Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia TAA tu, nilikuwa napitia hapa ripoti ya CAG, kuna mkandarasi ambaye alipewa kutengeneza mitambo na mfumo katika Uwanja wa Julius Kambarage Nyerere. Alicheleweshewa malipo zaidi ya siku 216 tukalipa zaidi ya bilioni 13, tukijadili hapa tena unaambiwa kazi yetu kujadili waganga wa kienyeji. Bilioni 11 imekwenda lakini waliochelewesha ni Watumishi wa Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini palikuwa na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, mkandarasi amecheleweshewa malipo tukalipa bilioni 2.5, Wizara ya Fedha, lakini vile vile palikuwa na ucheleweshaji wa msamaha wa kodi ambapo kontena 223 zilikaa bandarini pale tukalipa tena mkandarasi delay ya kucheleweshewa msamaha wa kodi, zaidi ya bilioni 11. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatujawahi kusema shilingi 10,000 shilingi 100,000 kila siku tunazungumzia mabilioni. Ni lini tutashuka kutoka kwenye bilioni kuja kwenye mamilioni, tuje kwenye maelfu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna miradi mikubwa ambayo tunaenda nayo, Mama yetu anajitahidi kuhakikisha miradi iliyoachwa inaendelea na inakamilika na imaleta tija. Kwa stahili hii miradi, tumekadiria Bwawa la Mwalimu Nyerere liishe kwa trilioni 6.5 ngapi huko litaisha kwa trilioni 8. Kama tusipodhibiti mapema kuzuia waganga wa kienyeji kudhibiti hizi fedha; kama mradi wa SGR tumehakikisha tutumie trilioni kumi na ngapi sasa zitaisha kwa zaidi ya trilioni 40. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niiombe Serikali, tunapokuja humu kuishauri Serikali watusikilize, ndiyo kazi yetu. Wananchi walijipanga mstari kwachagua wabunge kwa niaba yao kwenda kuwasemea. Sasa wanatozwa tozo wanavumilia. Hizo tozo ambazo wanajibana na familia zao leo tena zinakuja kuibiwa huku, eti sisi tuwe tumekaa. Sasa tuna maana gani ya kukaa kama Bunge? Basi ijulikane kuna mihimili miwili, Mahakama na Serikali, kazi iendelee, sie tukalime, Wizara imeongezewa bajeti ya kilimo, tukaongeze mashamba, uzalishaji watu wa mjini waje wapate…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)