Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kukupongeza wewe kwa kutuongozea kikao vyema, lakini pia niungane na waliyochangia kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote mbili pamoja na Wajumbe wa Kamati hizi kwa kazi nzuri ambayo mnafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza Wenyeviti kwa Mawasilisho mazuri, lakini kipekee nitumie nafasi hii kuishukuru sana Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mwenyekiti, Mheshimiwa Vita Kawawa, Makamu Mwenyekiti Vincent Mbogo pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa ushirikiano mzuri na maoni, ushauri na maelekezo ambayo mnatupatia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, tunawashukuru sana kwa ushirikiano huu. Pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango na yale ambayo Bunge litaazimia lakini pia maoni na ushauri ambao wametupatia tunaenda kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza mpendwa wetu Mheshimiwa Rais na Amir Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika michango ya leo na katika Bunge hili Mheshimiwa Rais, Waheshimiwa Wabunge wamempongeza kwa kazi nzuri ya kuimarisha diplomasia ya uchumi na diplomasia ya uchumi pamoja na diplomasia ya ulinzi ni vitu pacha. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais, kazi nzuri ambayo ameifanya ya kuhimarisha diplomasia ya uchumi, kazi hiyo hiyo nzuri imetuimarisha katika suala la diplomasia ya ulinzi. Kwa hiyo na hilo tunamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wenzangu, kama wanavyofahamu majeshi yetu yanayo mahitaji makubwa, yapo mahitaji ya kisekta na katika hili niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri. Ukienda kwenye Vikosi na maeneo ya Majeshi yetu utakuta wanahitaji huduma ya maji, kwa hiyo itabidi tukae na Wizara ya Maji; Barabara wakati mwingine kwa shemeji yangu Angellah Kairuki upande wa TARURA; Mheshimiwa Profesa Mbarawa upande wa TANROADS na Sekta nyingi. Kwa hiyo niendelee kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa ushirikiano wanaotupatia katika kuhudumia majeshi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hoja. Moja ya michango ya Waheshimiwa Wabunge, ilikuwa ni ni kuhusu ajira kwa vijana wetu kupitia JKT. Ningependa kuwakumbusha kwamba, jukumu la kwanza na kubwa la JKT toka suala la kujiunga na JKT kwa mujibu wa sheria liliporudi mwaka 2013, yamekuwa masuala ya kuwajenga vijana kimaadili na kiuzalendo. Hata hivyo, kutokana na changamoto ya ajira nchini, Serikali imefanya kila aina ya jitihada hata kupitia JKT, wale vijana ambao wanaenda kwenye mafunzo ama kwa mujibu wa sheria ama kwa kujitolea, jitihada za Serikali zinaendelea kufanyika kuhakikisha kwa kadri inavyowezekana vijana hawa wanapata ajira kupitia kwenye Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Takwimu za 2018, 2019 na 2020, vijana ambao wameenda JKT asilimia 45 wamepata ajira kwenye Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama. Serikali tunaendelea kuwa wabunifu hasahasa kwenye masuala ya mawanda upande Sekta za Uzalishaji ili kuhakikisha hata hii asilimia ambayo hawapati fursa kwenye Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wanapata fursa kwenye maeneo mengine likiwemo suala ambalo Mheshimiwa Hussein Bashe, amelitaja Memorandum of Understanding kati ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Kilimo. Sasa hivi iko tayari na panapo majaliwa wiki ijayo tutaisaini ili kujikita zaidi kwenye program za Wizara za Kilimo, kwa mfano, kuna Skimu ya Umwagiliaji kule Chita. Kupitia skimu hii kwa Takwimu ambazo Mheshimiwa Waziri Bashe, amezisema kwa mfano uzalishaji wa mbegu za alizeti tani 500 zimefanyika kupitia program hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali kwa mfano upande wa MAhindi tumezalisha tani 300 kupitia JKT, upande wa mpunga tumezalisha tani 468, upande wa mazao ya mafuta tumezalisha mbegu tani 206, lakini hata kwenye mazao ya chakula mahindi tumezalisha tani 3,876, Mpunga tani 1,276, hizi ni takwimu za mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kila sekta kuwa wabunifu katika kuhakikisha tunazalisha ajira milioni nane kama tulivyoahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 – 2025, tutaendelea kushirikiana na Wizara za Kisekta kubuni mawanda ambayo yatasaidia vijana wengi kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tunaliangalia ili kusaidia vijana kupata ajira ni kuangalia mitaala ambayo inafundishwa kwenye upande wa ufundi stadi na JKT. Kuangalia namna ya kupata accreditation ili vijana wanaopata ufundi stadi upande wa JKT iwe ni sawa na yule ambaye amehitimu VETA na Taasisi nyingine ambazo zinatoa Vocational Training.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie pia hivyo hivyo, kulikuwa na hoja ya uhitaji wa kuweka alama za mipaka pamoja na barabara za ulinzi; Waheshimiwa Mawaziri, Dada yangu Mheshimiwa Angeline Mabula, Waziri wa Ardhi; Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi; pamoja na Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Fedha, tumevichukua hivi, tutaendelea kushirikiana nao ili tuweze kuvitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja.(Makofi)