Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahasante sana kwa nafasi ya kuchangia ikiwa leo ni mara ya kwanza katika mwaka huu wa 2023; na sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye Enzi na Utukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata fursa hii ya kuchangia kwenye Kamati hizi mbili, na nitajikita kwenye Kamati ya Bajeti ambayo ina watu mahiri, makini na Bingwa kabisa. Napenda nitumie fursa hii kuwapongeza kwa kazi kubwa ambayo wanafanya na wanasikiliza kwa umakini maoni ya wataalamu waliopo ndani ya Bunge hili na kuweza kuyafanyia kazi. Nawapongeza sana Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakwenda kuchangia kipengele cha 2.11 inayohusu Pato la Taifa. Kamati imeishauri Serikali kuweka mikakati ya kuchochea uzalishaji katika sekta za uzalishaji kama vile utalii, kilimo na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niishauri kamati kuongezea yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kuongeza Pato la Taifa tunafahamu mchango wa utalii katika Pato la Taifa. Na pato letu la Taifa walau lirudi pale kwenye asilimia saba kama ambavyo kama imesema. Tunafahamu Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ameshafanya kazi kubwa ya kulitangaza Taifa hili kwenye sekta nzima ya utalii. Lakini tusipokuwa makini kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Rais inaweza isilete matunda tarajiwa kama tusipoamua kuboresha viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Wizara ya Mawasiliano imekwenda juu ya Mlima Kilimanjaro ikaweka mtandao kule. Tusifikiri tu wanaweza kupeleka yaliyo mazuri kwa wenzao kwamba bwana nipo juu ya Mlima Kilimanjaro njooni Tanzania kuna hivi lakini pia wanaweza wakapeleka yaliyo mabaya kama tusipoamua kuboresha viwanja vya ndege nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa International Civil Aviation Organization (ICAO) inazitaka kila mamlaka za viwanja vya ndege kuwa na vyanzo vya mapato. Sisi Tanzania tumeweka passenger service charge ambayo n idola 40 kwa kila anayesafiri kwenda nje na shilingi 10,000 kwa kila ambaye anasafiri ndani ya nchi. Hela ambayo katika low season tunapata bilioni 40 na katika high season tunafika bilioni 55. Fedha hizi zinachukuliwa na TRA na mamlaka ya viwanja vya ndege haiwezi kufanya lolote katika kuboresha viwanja vya ndege kwa sababu haina fedha ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni kwa nini mamlaka inayosimamia viwanja vya ndege (TCAA) iweze kuwa na mapato lakini Mamlaka ya Viwanja vya Ndege isiwe na mapato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni kwa nini Mamlaka inayosimamia Viwanja vya Ndege TCAA iweze kuwa na mapato lakini Mamlaka ya Viwanja vya Ndege isiwe na mapato? Kwa hiyo ili kuifanya kazi ya Mheshimwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kulitangaza Taifa hili kupitia Royal Tour kuwa endelevu, ni lazima tuiache Mamlaka ya Viwanja vya Ndege iboreshe Viwanja vya Ndege kwa kuachiwa ile hela inayokusanywa kwa passenger service charge itumike na mamlaka ile na isiwe inang’ang’aniwa na TRA, wenyewe hawapati hata shilingi moja. Kwa mtindo huo hatuwezi kuifanya kazi nzuri ya royal tour kuwa kazi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa taarifa iliyopo ni kwamba Kenya wanafuata Sheria hii ya ICAO, wanakusanya Viwanja vya Ndege wenyewe, Rwanda wanafanya hivyo, Malaysia wanafanya hivyo. Kwa hiyo nchi nyingi za jirani zenye viwanja vya ndege ambavyo ni bora wameweza kukusanya hizi fedha wenyewe na kuboresha miundombinu yao. Sasa Tanzania tuamue sasa kufanya juhudi za Mheshimiwa Rais za Royal Tour kuwa sustainable na kuleta tija inayotarajiwa kwa kuhakikisha tuna viwanja vya ndege vilivyo bora kwa kuiachia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege fedha ile ya passenger service charge ili waweze kufanya kazi yao ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekuwa tukishauri hapa kwamba Mamlaka ile iachiwe Wahandisi wa kuweza kufanya kazi zile za Kihandisi na suala hili limekuwa linapotoshwa kidogo hapa kidogo Bungeni kwamba, Wahandisi waliopo TANROADS hawawezi kufanya kazi katika Viwanja Vya Ndege. Issue siyo suala la Uhandisi hapa, issue ni Mamlaka ambayo TAA imepewa. Mhandisi aliyekuwepo TANROADS yuleyule anaweza kufanya kazi Viwanja vya Ndege kulekule, issue ni impact of the road ndiyo ambayo inaangaliwa katika design tu pale, ndege inaposhuka impact yake ni nini na gari inapopita barabarani impact yake ni nini. Kwa taarifa tu iliyopo Wahandisi waliosimamia Viwanja vya Ndege ndiyo walewale walihamishwa wakapelekwa TANROADS. Kwa hiyo suala siyo knowledge, suala ni mamlaka iliyopewa TAA, warudishiwe Wahandisi wao ili waweze kufanya kazi ipasavyo kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuchangia kuhusiana na maoni mahususi ya Kamati ya Bajeti kipengele cha 7.1. Kamati imeishauri Serikali iandae mpango wa uhitaji wa rasilimali wa Taifa ili taaluma zinazozalishwa ziwe sawa na mahitaji ya maendeleo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana Kamati katika kipengele hiki, lakini naomba kusema kwamba suala la taaluma yetu nchini haliwezi kuanza katika level ya juu wakati mwanafunzi anakwenda Chuo Kikuu, suala la taaluma, suala la rasilimali watu linapaswa kuanzia tangu mtoto akiwa tumboni kwa mama yake. Sasa Mheshimiwa Rais amefanya mpango mzuri wa lishe lakini tuhakikishe kunakuwa na afua endelevu. Kukosekana kwa afua endelevu kumesababisha akinamama wajawazito wanakosa damu ya kutosha na vilevile kuzaa uzao ambao hauna afya njema. Ndiyo hapo tunasema Taifa linakuwa na udumavu, udumavu umeshuka sasa hivi kwa asilimia 34, lakini hakika tunapaswa kushuka zaidi ili tuweze kuzalisha Taifa lenye watu wenye uwezo wa kubuni, uwezo wa kufikiri na uwezo wa kufundishika. Kwa hiyo kama Taifa tunapozungumzia suala la rasilimali watu ni lazima tuwekeze nguvu huku chini mtoto anapokuwa tumboni na mtoto atakapozaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa iliyopo nikwamba Tanzania tunazalisha mabubu kila kukicha, kadri siku zinavyoendelea idadi ya mabubu inaongezeka. Mwaka 2018/2019 tulikuwa na mabubu 6,103 nchini, lakini ninavyozungumza sasa hivi mwaka 2023 tuna mabubu 8,503 nchini. Serikali inatoa fedha nyingi katika shule za mabubu hapa nchini kwa ajili ya kuwezesha chakula chao, kuwalipa Walimu wao, lakini jambo hili kama lingeangaliwa tangu mtoto anapozaliwa idadi hii ya mabubu isingekuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza fedha nyingi unnecessarily, Serikali sasa iamue, kila mtoto anapozaliwa apimwe usikivu. Haya mambo yanawezekana, kila Hospitali ya Wilaya kuwe na kifaa cha kupimia usikivu kwa mtoto anapozaliwa na kifaa kile huwezi amini hakihitaji mabillion ya fedha, kina-range kwenye shilingi milioni nani mpaka milioni 10 kipimo cha kupima usikivu, lakini kwenye hospitali zetu zote za wilaya vifaa vile havipo, ni nini tunatengeneza na ni rasilimali gani tunaitaka nchini? Kwa hiyo Serikali iamue ku- save hizi fedha zote ambazo zinapotea bure, iongeze nguvu katika vifaa vinavyoweza kupima usikivu mara mtoto anapozaliwa. Nchi za wenzetu zinafanya hivyo, lakini sisi tunaangalia tu macho yake ya njano, amelia kwa wakati, amegeuzwa miguu chini, anaonekana mtoto yuko salama, lazima tufanye extra kwa ajili ya kupata afya bora ya mtoto aliyezaliwa ili Taifa lipate rasilimali zilizo bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa fursa hii.(Makofi)