Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi pia kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia kuhusiana na bajeti kimsingi tunazungumzia uwezo wa Serikali kuhimili, namna bora ya kuendesha shughuli za Serikali kwa maana ya miradi ya maendeleo na miradi ya kawaida, haya yote yanategemea sana uwezo wa Serikali kukusanya kodi na kodi inatoka kwenye shughuli za uzalishaji, hakuna maajabu katika uchumi ni kuzalisha ndiko ambako kunapelekea Serikali kuwa na uwezo wa kuuza bidhaa, ndani na nje ya nchi, kuvutia fedha za kigeni na kugharamia shughuli za maendeleo. Ndiyo maana Waziri wa Fedha alipokuwa anatuletea Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2022/2023, alijikita na alijielekeza katika mpango ule na hali ya uchumi kwenye sekta za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona Serikali ikiweka msukumo katika sekta za uzalishaji katika kilimo, mifugo, nishati lakini pia katika ujenzi wa miundombinu ambayo inaweza kwenda kutusaidia katika kuimarisha uchumi wetu. Kwa maana ya reli ya mwendokasi - SGR, mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa kule Mwalimu Nyerere, ununuzi wa ndege za ATCL, miradi ya elimu, afya, maji, regrow kwa maana ya utalii na maliasili lakini pia teknolojia ya TEHAMA pamoja na sanaa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni mikakati ya ndani, ni sera za ndani katika kuimarisha uchumi wetu. Lakini sera hizi za ndani hatuwezi kwenda ku-achieve kama sera za nje hazita–complement jitihada za ndani. Kimsingi naweza kuzungumza kwamba hakuna kitu kinachoitwa sera za nje, sera za nje ni mwendelezo tu wa sera za ndani, kitu gani tunakitaka ndani na tunapataje nje, katika hilo wataalamu wetu ama wanadiplomasia wetu wanapaswa kuainisha misingi ambayo inaweza ikajenga mahusiano na nchi nyingine, katika kushawishi, kutetea maslahi yetu ya ndani ili tu–achieve goals za ndani kupitia mahusiano yetu ya nje. Kwa hiyo, sera za nje ukitafsiri ni uwezo wetu wa kutafsiri mikakati yetu ya ndani na jinsi gani tunaweza tukapata ama tuka-achieve nje. Tukatafsiri dunia pana kwa rasilimali zake kuona zinatujibu vipi changamoto zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wizara ya Mambo ya Nje ni muhimu sana katika utekelezaji wa sera za ndani na mikakati yetu ya ndani. Sera ya nje ni lazima ijibu mikakati na shida zetu za ndani. Kwa hiyo utakuta katika hili unaweza kuona kwamba sera ya asili ya nchi yetu ilikuwa kusimama na wale wanaoonewa, kusimama na wanyonge kwa sababu tulijua uhuru wetu ulikuwa hatarini kama nchi nyingine za jirani hazitakombolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sera yetu ya nje kwenda kuzikomboa nchi jirani ili tujiimarishe na tusimamie usalama wetu sisi wa ndani, na ndiyo maana ndugu zetu walikwenda vitani kukomboa nchi nyingine ili kuhakikisha kwamba tunalinda uhuru wetu wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo usimamizi thabiti wa kanuni hii na nyinginezo wakati wa uhuru ndizo ambazo ziliipa heshima kubwa nchi yetu kwa sababu tulisimama na wanyonge lakini katika kulinda uhuru wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Mambo ya Nje si Biblia wala Msahafu, si Amri Kumi za Mungu, zinapaswa kubadilika kulingana na wakati. Na ndiyo maana tunaona kwamba mabadiliko ya fikra, mwenendo na mitazamo siku zote inabadilisha pia hata mikakati ya ku-achieve mambo yetu ya ndani kupitia mahusiano yetu ya nje. Na ndiyo maana mwaka 2001 tulikuja na kitu kinaitwa diplomasia ya uchumi. Dhana na lengo la diplomasia ya uchumi ni kuhakikisha kuwa mbali na malengo ya kidiplomasia, mfano kiulinzi, tunajikita katika kujenga na kuimarisha mahusiano na nchi nyingine kwa ajili ya kuimarisha uchumi wetu. Na katika hilo tunaweza kuona kwamba katika miongo miwili iliyopita tuliweza kuimarisha sana mahusiano yetu na ndiyo maana tuliweza kuvutia wawekezaji wengi na watalii wengi walikuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijielekeza katika kitabu cha mwelekeo wa Sera za Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 207 unatuelekeza kwamba diplomasia ya nchi yetu haitafungamana na upande wowote. Lengo ni kushirirkiana na nchi yoyote ambayo ina mapenzi mema ambayo matarajio yao na matumaini yetu yanaweza kukutana. Katika msingi huo diplomasia ya uchumi wetu ni lazima iwezeshe Tanzania kuwa kitovu cha uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki pia katika Bara la Afrika kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo ni lazima turudi kwenye misingi ya asili kusimama na wale wanaoonewa. Sasa hivi unaweza kuona vita imetamalaki katika maeneo mengi katika nchi ambazo zinaendelea. Kule wanaoonewa ni nani? wanaoonewa ni wafanyabiashara wakubwa ambao wamewekewa vikwazo hafanyi biashara kwa sababu tu wamezaliwa katika nchi fulani ambayo wengine hawaitaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule anayeonewa ni nani? ni wataalamu na researches ambao hawana uhuru wa ku- practice utaalamu wao kwa sababu tu wamezaliwa katika eneo fulani la kijiografia. Katika misingi hiyo sisi ambao tunasimama na hao ambao ni victim wa mambo ambayo yanaendelea tunafaidika vipi. Tunapaswa kutumia loop hole hiyo kuwavutia hapa kuja kufanya shughuli zao za kiuchumi, Kama ni wafanyabiashara wa waje walete fedha hapa kwa sababu huko kwao hazina usalama. Kama wana utaalamu wa kilimo waje walime hapa. Kwa mfano nchi kama Ukraine inalima sana alizeti. Sasa hivi hawawezi kulima, wakulima hao hawalimi, wataalam wao hawafanyi kazi. Kwa nini tusiwaonyeshe kwamba hapa kuna fursa ya kuja ku-achieve kile ambacho walikuwa wanakifanya katika nchi zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mitaji mingi kule nje sasa hivi ambayo imefungwa hawawezi kufanya biashara kwa sababu ya vita. Sisi kama Tanzania tunawezaje kutumia loop hole hiyo ku-attract hao watu kuja kuwekeza katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru mwaka jana tuliona dhamira ya dhati ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alipowaita mabalozi wote wa Tanzania ambao wanawakilisha nchi zetu nje, aliwaita pale Zanzibar na alikaa nao kwa siku kadhaa. Moja ya vitu ambavyo vilinivutia ni mwelekeo mpya wa diplomasia yetu ya uchumi ambao ndio ulikuwa msingi wa mkutano ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengi ambayo walijadili, walizungumzia nafasi ya Tanzania katika uchumi wa kimataifa. Katika hili naomba nizungumze kitu kimoja. Balozi zetu zina nafasi kubwa sana ya kutusaidia ku-achieve malengo yetu ya ndani. Lakini tunapaswa kuangalia ni jinsi gani ya kushirikisha sekta binafsi; kwa sababu hatuwezi ku-achieve haya yote ambayo tunayataka kama tunawafanya sekta binafsi kuwa bystanders, kuwa watazamaji. Katika msingi huu hata diaspora ni sehemu muhimu sana ya utekelezaji wa sera yetu ya nje kama tutawashirikisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ambacho kinatokea sasa hivi? Tuna mashirika makubwa ambayo yanashirikiana na utalii. Kwa nini Wizara ya Mambo ya Nje isi-recruit watu kutoka sekta binafsi ambao ni wataalamu wa sekta husika ambao wanaweza wakavutia mitaji, wataalamu wa masoko na biashara wakaenda kuwa stationed kwenye balozi zetu? Si lazima walipwe mshahara na Serikali na wala si lazima walipwe mshahara na hazina, wanaweza wakawa vetted wakawa attached kwenye balozi zetu wakafanya kazi ya kuvutia mitaji, kuweka masoko, kuweka mikakati ya kuleta watalii na shughuli nyingine na wanadiplomasia wetu wakajikita katika shughuli za kidiplomasia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini shughuli za kitaalamu tukatengeneza utaratibu wa sekta binafsi na taasisi za Serikali kushiriki moja kwa moja na kukaa katika balozi zetu wakiwa wanatumikia nchi yetu katika maeneo ambayo wamebobea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote ambayo wenzangu wametangulia kuzungumza bado naweza kuzungumza kwamba Tanzania tumebarikiwa kwa jiografia yetu, tupo katika eneo zuri sana la kiukanda. Kwa mfano Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa hivi ina nchi takribani saba, pamoja na Sudan ya Kusini na Congo. jumuiya hii ina watu zaidi ya milioni 300. Hii inatupa uhakika wa soko kubwa la bidhaa zetu lakini inatupa eneo la mkakati la kufanya mahusiano na wawekezaji wa nje. Hii ni kwa sababu tunasoko la pamoja tuna ushuru wa pamoja na uhuru wa wafanyabiashara wetu kuzunguka na mitaji yao katika eneo la Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kuona nia ya dhati ya Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan. Yeye pekee alifanikiwa kuondoa vikwazo takribani 64 kati ya 68 katika biashara yetu na Kenya. Kuondoa vikwazo hivi kumepelekea ongezeko la biashara kutoka bilioni 800 mwaka 2020 mpaka trilioni 1.2 mwaka 2021. Sasa haya unaweza kuona ni jinsi gani Rais wetu ameweza kuondoa hivi vikwazo na taasisi za Serikali, kwa mfano Wizara ya Mambo ya Nje kupitia balozi zetu zinaweza zika-compliment jitihada hizi katika nchi nyingine. Huu ni mfano mmoja lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DENNIS L. LONDO: …tuna mifano mingi ambayo tunaweza tukaitumia katika ku-attract wawekezaji na kuimarisha miradi yetu ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja nashukuru. (Makofi)