Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kipekee namshukuru Mungu tuko hapa tunaongea mambo ya maendeleo ya nchi yetu. Nitamke rasmi kwamba ninaunga mkono hotuba zote za Kamati mbili hizo kamati ya NUU na Kamati ya Bajeti na nawapongeza sana Wenyeviti waliowasilisha hotuba hizo. Pia nawapongea Wabunge wote kwa kuweza kuunga mkono na kuweza kuyazungumzia mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo machache. Jambo la kwanza naomba nizungumzie kuhusu ile asilimia kumi ya mapato ambayo inatoka kwenye local government kwa ajili ya kuwawezesha wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na walemavu asilimia mbili. Makusanyo yalikuwa mazuri sana kipindi chote tunachozungumzia sasa, lakini kinachosikitisha ni kwamba hela ile yote haikugawiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza hapa kuna kama bilioni 18 zilibaki Benki Kuu hazikuchukuliwa na hazikuchukuliwa kwa sababu gani? kwa sababu ambao wanastahili kupewa hawaku-qualify lakini qualification moja wapo ambayo iliwafanya wasipewe hela hizo ni pamoja na kutokuwa na vikundi rasmi vya kuchukua hela hiyo. Sasa shida yangu mimi mpaka nikaja kuizungumzia ni kwamba, je, tunapozungumzia vikundi viundwe, Serikali inasaidia nini kufanya hivyo vikundi vimeundwa na vikaweza ku-access hizo hela? Haina maana tuseme kwamba wanawake wamewezeshwa lakini hela ipo Benki Kuu, hela haitoki, basi hata wale wachangiaji hawakufanya jambo la maana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali sasa iangalie kwamba kuna kila sababu ya kuweka elimu ya kuwawezesha hawa ambao wanatakiwa kuchukua hiyo hela yaani wanawake hao, vijana hao na hao walemavu kupata hiyo asilimia wanayotakiwa. Hii iko kote Tanzania nzima, lakini mbaya zaidi wachangiaji ambao ni halmashauri tofauti, wengine wamechangia asilimia pungufu. Bila kutamka ni halmashauri zipi lakini kuna waliochangia asilimia saba, wengine wakachangia asilimia tano. Ni nani hasa anayetakiwa kuweka msisitizo kwamba lazima iwe asilimia kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linashangaza na tuliliona kwenye Kamati ni ile kwamba unakuta sasa hela hiyo imeshatolewa na halmashauri, inakuwa kwenye suspense, lakini zinakuja shughuli za dharura au Mwenge unapita, ile hela asilimia kumi ambayo haijakopeshwa inapelekwa kwenye shughuli kama hiyo. Hili siyo jambo zuri, hili tunadanganywa, halijakaa vizuri kabisa, kwa nini hela hiyo ya watu hawa mlioona kwamba wao hawana security ya kukopa benki wanatakiwa kusaidiwa uchukue hiyo hela upeleke kwenye mwenge, siyo jambo zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wanzangu Waheshimiwa Wabunge ambao pia ni Waheshimiwa Madiwani wasimamie jambo hili. Hela hiyo inatoka kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu iende kwenye shughuli hiyo. Tusikubali hata senti moja ikaenda kwenye shughuli ambayo siyo. Hil limetokea kwenye halmashauri nyingi, tumesomewa, tumeiona na kwa pamoja tuliona kwamba hilo jambo siyo zuri na pia lisiwe endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tumekuwa tukilizungumza hapa kila kukicha na bado tunaliona ni tatizo japo lilizungumziwa katika changamoto ambazo tulitarajia zingetatuliwa kipindi kilichopita lakini zikatatuliwa kwa asilimia kidogo sana, ni mikopo ya wafanyakazi kuwa na interest rate inayolingana na mikopo ya wafanyabiashara. Hili jambo liko Tanzania tu na ni kwa nini iwe hivyo? Kama taasisi binafsi yakiwemo mabenki yanakopesha basi yatofautishe, risk zilizopo kuwakopesha wafanya kazi na risk zilizopo kuwakopesha wafanyabiashara. Hapo unakuta kwamba mikopo hii imewekewa insurance, lakini utakuta kwamba mfanyakazi ambaye mshahara unakatwa kabla hata hajapewa yeye mwenyewe kwenda kulipia mkopo wake anachajiwa interest rate inayolingana na na commercial rate. Tumewaomba sana Wizara ya Fedha isimamie jambo hilo wamesema watafanya miaka nenda rudi, sasa kwa nini wafanya kazi wawe shamba la bibi? Haingii akilini, naomba sana hili jambo liangaliwe kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ukiwa mfanyabiashara umebeba riski nyingi sana mpaka waje wakufuate kwako, wafuatilie, ni tofauti na mfanyakazi ambaye unaletewa na mwajiri kwamba bwana mshahara wake umeingia lipia hapo. Kwa hiyo naomba jambo hilo nalo niliweke wazi kwamba ni vyema kabisa ikaonekana kwamba hawa watu waangaliwe tofauti na mikopo ya wafanyakazi napendekeza na tuliona hivo iwe single digit, wala isifike kwenye kumi au kumi na, hamna sababu na kwa sababu inarejeshwa yote na pale ambapo anakufa, basi insurance inalipa. Naomba sana hilo tuliangalie na nadhani linawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo niliona ni vyema nilizungumzie ni akiba ya fedha za kigeni. Ilipofikia mwaka jana Juni tulikuwa na Dola za Kimarekani milioni 510.3 ambayo ilikuwa pungufu kwa ilivyokuwa mwaka 2021 ambayo likuwa ni milioni 5,209.8. Kupungua kwa fedha za kigeni kunaathiri mfumko wa bei, kwa hiyo kama Kamati na mimi mwenyewe nasisitiza kwamba kuweka akiba ya forex, kutumia dhahabu ni kitu bora zaidi kwa sababu haibadilikibadiliki wakati ambapo thamani inabadilika. Kwa hiyo basi, napendekeza na nasisitiza tuwekeze hela zetu kwenye dhahabu na katika forex reserve yetu kwenye dhahabu. Hili jambo tuliliongea mwaka juzi, mwaka jana na tunaliongea mwaka huu, nataraji Serikali itatusikia, ione kwamba hilo pendekezo ni muhimu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha. (Makofi)