Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nami napongeza Kamati zote mbili, nami ni Mjumbe wa Kamati ya NUU. Hili ninalolisema mara zote nimelisema na sitaacha kulisema kwamba, Mheshimiwa Rais, kama mwanadiplomasia namba moja, ameendelea kuitendea haki nafasi yake, ameendelea kufanya ziara, ameendelea kutafuta wawekezaji, ameendelea kufanya shughuli zote ambazo zinathibitisha kwamba Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan ni mwanadiplomasia namba moja katika Taifa letu. Hizi shughuli anazozifanya zitakuwa na thamani na manufaa kwa Taifa letu kama kutakuwa na connection na kama kutakuwa na link kati ya shughuli ambazo zinaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara nyingine za kisekta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa yetu, mojawapo ya jambo ambalo limejitokeza ni kukosekana kwa mkakati maalum wa kiushirikiano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na Wizara nyingine za kisekta. Ni kweli kwamba ushirikiano upo, lakini tunachokitaka ni ushirikiano wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitatoa mfano. Kwa takribani miaka minne, na bahati nzuri Waziri wa Kilimo yuko hapa; Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa ikiratibu vijana takribani 100 kwenda nchini Israel kujifunza masuala ya kilimo kwa muda wa miezi 11. Hapa ninalo tangazo la 2019 ambalo limeandikwa, “Tangazo la Mafunzo ya Kilimo Nchini Israel.” Tangazo hili linaalika vijana waliomaliza SUA waende Israel wakajifunze kilimo kwa muda wa miezi 11. Sasa wakisharudi wale vijana ni wa nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale vijana sio tena wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Wale ni vijana wa Kilimo; lakini mpaka hapa tunavyozungumza sijui kama Wizara hata ina takwimu vijana hawa ni wangapi in total na wako wapi? As far as I know, majority wamerudi. Sana sana the best they can do, wanajiajiri katika biashara ya boda boda. Sasa tumewapeleka vijana miezi 11 wamejifunza very advanced skills za mambo ya kilimo, lakini kwa sababu hakuna mkakati mahususi wa kuonesha hiyo link, Wizara ya Mambo ya Nje imeshatimiza wajibu wao, lakini wale ambao wangepaswa kuwalea wanakuwa hawajatimiza lile ambalo lingekuwa ni endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri. Katika maazimio ya Kamati ya Bajeti, maoni na mapendekezo mahususi, ukurasa wa 68, imeeleza ya kwamba, katika huu mpango ambao Mheshimiwa Bashe anakujanao wa block farming Serikali ianze na vijana wa JKT. Naomba kulishawishi Bunge lako, kama sehemu ya hayo maazimio ambayo kwa namna moja au nyingine yatakuja kulisaidia Taifa letu kukabiliana na mfumuko wa bei, hususan katika kipengele cha mafuta ya kula. Katika bajeti iliyopita, katika Muswada wa fedha, tulisema hapa tumetoa ahueni kwa waagizaji wa mafuta, lakini tuwe honest katika nafsi zetu, je, mafuta ya kula yamepungua bei kutokana na hilo punguzo ambalo tumewapa waingizaji wa mafuta? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli tukiwa wakweli wa nafsi, hakuna punguzo ambalo linamfikia mlaji, isipokuwa ni manufaa wanayojinufaisha wafanyabiashara wakubwa wanaoagiza mafuta hayo. Kwa sababu hiyo, nashawishi Bunge lako, tuongeze azimio kwamba, katika hii hoja mahususi ambayo wenzetu wa bajeti wamesema, tuseme kwamba, Bunge liazimie tuwape kazi na nyenzo wenzetu wa JKT na SUMA-JKT ya kuhakikisha kwamba Taifa hili ndani ya miaka miwili, litajitosheleza kwa mafuta ya kula na litaweza kusafirisha mafuta ya kula kwenda nje. That is the only way ya kuhakikisha tunakabilana na mfumuko wa bei katika baadhi ya vitu ambavyo tunaweza tukazalisha hapa nchini. Vinginevyo tutabaki na taarifa za UVICO, na taarifa za vita ya Ukraine na Urusi. Lazima tuje na mikakati, tubuni namna ambayo tutaondokana na shida hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tumesema kwamba, lazima tu-link. Kuna hawa vijana wa JKT, hawa waliotoka Israel wangeweza kuwa ndio wasaidizi wao katika hiyo block farming. Katika ku-link, nakushukuru wewe unatoka Mufindi, sisi tunazalisha mazao ya kilimo. Katika diplomasia ya uchumi tunasema kwamba, pawepo na mkakati kwamba hii elimu ifike mpaka kule chini. Sisi watu wetu wa Mafinga, Mufindi, Iringa, Kilolo na Njombe waweze ku-access masoko ya mbao, milunda na mazao ya misitu kwenye soko la Congo. Waweze ku-access soko la nafaka kwenye soko la Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri bashe shahidi, wale Bodi ya Mazao Mchanganyiko walipeleka kule mazao yamekaa miezi mitatu yanashindwa kuingia kwa sababu tu kumekosa link kuwashirikisha watu wa mambo ya nje kushirikiana na Kilimo na Viwanda na Biashara kujua je, soko la Congo limekaaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe soko la Congo kule Lubumbashi ni lazima ushirikiane na wale tycoon ujue wanapita njia gani ndio uweze ku access lile soko, sasa kama hakuna hiyo link tutabaki tu tunalaumiana, hivyo itoshe tu kusema kwamba tunahitaji kuwa na link kati ya diplomasia yetu ya uchumi, uzalishaji wetu na Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze umetusomea hapo tangazo, nimeona kutakuwa na Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo itakuwa ni mojawapo ya link nzuri sana kwa sababu bila viwanda, bila mazao huwezi kuwa na Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhitimisho niende kwenye suala la NIDA kwa haraka sana, pamoja na maazimio ya jumla. Katika suala la NIDA kwenye taarifa yetu tumesema ya kwamba NIDA inafanya kazi nzuri so far inafanya kazi nzuri, lakini wananchi wanataka vitambulisho. Mpaka hapa tunapozungumza NIDA wanafanya kazi mbili utambuzi, usajili na kutoa vitambulisho. Mpaka sasa wameshatambua wananchi takribani milioni 23 kati ya wananchi milioni 34 mpaka kufikia 2025/2026 wanaenda vizuri kwa sababu ni asilimia 68.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hao waliotambuliwa ambao ni milioni 23 ni milioni 19 sawa na asilimia 84 tayari wana ile namba ya NIDA, lakini wenye vitambulisho ni milioni 10 tu sawa na asilimia 56. Maana yake kila watu 100, 56 wana kitambulisho cha NIDA 44 hawana kitambulisho cha NIDA. Kwa hiyo, pale Serikali inayo wajibu wa kuisaidia NIDA kama ni Fedha au namna nyingine isaidie ili mwananchi apate kitambulisho, kwa sababu baadhi ya huduma zinataka siyo uwe na namba bali uwe na kitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maazimio ya jumla naomba kuhitimisha ipasavyo tuzisaidie Wizara hizi za Fedha, kwa sababu tumeona utekelezaji wa maazimio na tumesema kwamba Bunge linapoazimia siyo Mheshimiwa Chumi au Siyo Mwenyekiti wala siyo Mheshimiwa Vita Kawawa, sisi tunaazimia kwa niaba ya Wananchi. Kwa hiyo, matarajio yetu ni kwamba yale tunayoyaazimia ni kutatua changamoto na kero za wananchi, sasa yasipotekelezwa maazimio, maana yake ni kwamba hatujatatua na kupunguza kero za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu na ushauri wangu kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha pamoja na changamoto za kibajeti tuhakikishe kwamba yale tunayoazimia ambayo yanahitaji fedha kuyatekeleza basi wenzetu wapewe fedha. Kwa kuhitimisha Wizara ya Mambo ya Nje tu kwa mfano, kwa miaka mitano walitakiwa wapewe bilioni 48 za kuweza kujenga majengo na kuyaboresha ambayo majengo haya tungeweza kuyapangisha yangetupa mapato lakini mpaka ninavyozungumza ndani ya miaka mitano wamepewa tu bajeti ambayo haizidi asilimia 19. Kwa hiyo, katika kutekeleza maazimio ambayo yanahitaji fedha wenzetu wa fedha wajitahidi kutoa fedha ili tutekeleze, tupunguze kero za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja zote, Mungu atubariki wote, abariki wananchi wa Mafinga na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)