Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwa uchache kulingana na dakika zilizoko mbele yangu. Kwanza kabisa nipongeze Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kazi kubwa ya kutukuka na ya kizalendo wanayoifanya katika Taifa letu. Natangulia kupongeza kwa sababu vyombo hivi havina bajeti ya kutosha lakini kazi wanayoifanya ni kubwa sana. Nafikiri wangekuwa wanafanya kazi ambayo haina mashiko tusingekuwa tuko salama leo. Kwa heshima hii nawapa kwa sababu wanafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda moja kwa moja kwenye Bajeti ya Maendeleo. Tumesikia maoni ya Kamati, nami naungana nayo asilimia 100, lakini kwa masikitiko yangu makubwa, tumeangalia Ngome fungu namba 28 wamepokea asilimia 17.74 tu. Kwenye hii Jeshi letu liko hoi bin taabani, lakini wajibu wake ni mkubwa mno kulingana na bajeti ambayo wameipokea. Tunaelekea Bunge la Bajeti na hawa watu hawajapokea hata robo ya bajeti yao, ni hatari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua JKT ni eneo ambalo kila mtu anaangalia baada ya Taifa letu kuonekana kwamba ajira imekuwa ni duni kwenye Taifa letu, vijana hawana ajira hata awe na kitu gani, lakini nafasi ya ajira kwenye Taifa letu ni ndogo, wako mtaani, wana fani zao, lakini hawaajiriki mahali popote, hawawezi kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekimbilia kwenye chaka la Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambao wameonesha kuajiri vijana wengi kwenye Taifa letu. Hii siyo siri ni lazima tuseme ili tuone ni wapi palipotoboka? Eneo kubwa zaidi ni JKT ambao kimsingi mpaka sasa hivi vijana wetu wako huko kwenye mafunzo kwa maaana ya uzalendo lakini baadaye wataingia kwenye ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT pesa walizoomba jana za bajeti mpaka leo naongea hapa wamepata asilimia sifuri, the shame. Asilimia sifuri, tukajiuliza maswali kwamba hawa watu huenda vigezo hawajatimiza wakaja kwenye Kamati, tukawahoji wakasema na certificate walishapeleka, kuna nini kinaendelea kwenye Jeshi letu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawawezi kulia wakasikika au kusema popote kutokana na ethics za kazi zao, lakini sisi kama Taifa tunalionaje Jeshi hili ambalo linalinda ulinzi, mali zetu, uraia na watu wetu, wamepata asilimia sifuri? Mwaka jana walikuja hapa wakaleta Miradi yao ya Maendeleo wanayotaka itengewe fedha, Chita ambapo kuna Kilimo wameweka hekari 12,000, tukiamua kuhudumia eneo lile hata mfumuko wa bei utapungua. Tunafikiria nini kuhusu Taifa kama Vyombo vya Ulinzi na Usalama hatuwezi kuviangalia, hatuwezi kuvitengea bajeti kwa manufaa ya Taifa letu. Mama yetu kipenzi anazunguka kutafuta pesa huku na kule, nia yake ya dhati ni kulisaidia Taifa, Taifa linasaidikaje kama usalama wa nchi unakuwa tete? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia hili naona kuna la kufanya. Juzi Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mwigulu Nchemba alikuwa hapa akasema fedha hazigawiwi tu kama peremende, ni lazima kuwe na utaratibu umefuatwa, utaratibu umefuatwa fedha ziko wapi? Akamjibu Mheshimiwa Bashe, hapa akamwambia kwa kuwa wewe hujatimiza vigezo fedha zimejaa, zilizojaa zielekee kwenye Vyombo vya Ulinzi na Usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda naelekea maeneo yetu ya Jeshi la Magereza. Kwenye nchi yetu, kwenye Taifa Jeshi la Magereza mpaka sasa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa nakuongeza dakika moja maana muda wako umekwisha.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshazidiwa…

MWENYEKITI: Malizia sasa.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa Magereza ni watu 29,902, leo tuna watu 321,146. Tuliojaza kule siyo Watanzania, wako wahamiaji haramu 3,809 wako pale. Tuliomba tukasema kuwa kuna mkakati wa ziada wa kuwaondoa wahamiaji haramu, wahamiaji wale kwa siku wanatumia Sh.15,540,000, kwa mwaka wanatumia billion 5.6, bajeti ambayo tungeipeleka kwenye vituo vya afya, tukaipeleka kwenye madawati, tungepata madawati 81,000. Tungepeleka kwenye nyumba za Walimu tungepata nyumba za Walimu 62,200. Leo tunalia lakini watu wako picnic, wale wahamiaji haramu pale hatuwezi kuwapeleka shambani wakalime. Kwanza wako weak na wanafurahia kwa sababu wamepumzika, sisi tunapumzisha watu, wanakula pesa za Mama yetu, anakwenda kuzitafuta Ughaibuni, tuwe na uchun gu na pesa hizi za Rais wetu anatafuta Ugaibuni ili watoto wake wale. Nauliza swali, kiko wapi cha kumpikia mgeni wenyeji kulala na njaa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwe na utaratibu wa vyombo vya sheria wawaondoshe watu hawa, tayari Jeshi la Uhamiaji wamechukua hatua, wameanza kutoa Visa rejea, nawapongeza sana. Hoja hii ilikuwa ya kwangu mwaka jana, wameanza, lakini walioko ndani waondoshwe waende kwao tubaki sisi tubanane humu humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nakushukuru sana. (Makofi)