Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia ripoti za Kamati zilizoletwa mbele yetu. Nitapenda kujielekeza kwenye ripoti ya Kamati ya Masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Madawa ya Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende sana kuipongeza Serikali, Wizara na taasisi kwa namna zinavyopambana na masuala haya ya UKIMWI; lakini pia nipende kuwapongeza wadau kwa kushirikiana na Serikali kwa namna wanavyopambana na kutokomeza haya masuala ya UKIMWI kwa kufanya tafiti, kutoa huduma, kutoa vifaa tiba na kuwezesha matumizi ya takwimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili ni juu ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali ukiwemo ule Mradi wa Fikia Plus, Mradi wa Timiza Malengo na Mradi wa THIS (Tanzania HIV Impact Survey). Miradi hii ni mizuri na ina malengo mazuri kwa Taifa letu kwa kuwa ina dhamira njema ya kupambana na kutokomeza masuala ya UKIMWI, lakini pia inataka kuja na data na takwimu sahihi kabisa. Vilevile wanahitaji kuibua wanaohitaji tiba ya methadone kwa upande waraibu pamoja na matibabu ya UKIMWI na Virusi vya UKIMWI kwa watu walioathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kusema miradi hii ni mizuri isipokuwa kuna changamoto kubwa kwenye Mradi wa THIS. Tama unavyojieleza ni Tanzania HIV Impact Survey kwamba una lengo la ku - survey masuala haya ya UKIMWI. Changamoto iliyokuwepo kwenye mradi huu, mradi hauwatambui watoto wenye umri chini ya miaka 15 ilhali tunafahamu sasa hivi kumekuwa na hatari kubwa kwa watoto wetu. Tunafahamu kuna maambukizi ya UKIMWI toka kwa mama kwenda kwa mtoto, kumekuwa na vitendo vikubwa vya ubakaji kwa watoto. Kumekuwa na vitendo vikubwa vya ulawiti kwa Watoto, lakini pia kumekuwa na tabia ama wimbi limezuka la watoto kufanya mapenzi ya jinsia moja halafu Serikali inafanya mradi kabambe ya masuala ya UKIMWI wanawaacha watoto wenye umri chini ya miaka 15. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo hapa niseme kwamba haijafikiriwa ama haijawekwa sawa sawa…

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Hawa Mchafu kwa mchango wake mzuri, hususan kuhusu kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Nataka tu kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba juzi Mawaziri wa nchi 12 za Afrika tumekubaliana kwa vitendo kwamba tutaweka program maalum za kupunguza maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hususan watoto wenye umri wa miaka 18. Kwa hiyo, hili tunalifanyia kazi na Tanzania ndiyo nchi ya kwanza Barani Afrika ambayo imekubali kufanyiwa tathmini na nchi zote duniani katika mpango huu wa kupunguza maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Hawa taarifa hiyo.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ninaipokea. Ninachokisema Dada yangu Ummy, Mheshimiwa Waziri, mradi unaoendelea wa THIS ambao ni 2022/2023 unaelekea mwisho. Mradi hauwatambui watoto kwa maana hiyo sasa tutakuwa sasa tumeshafanya mradi kwa lengo la kutafuta data na takwimu za UKIMWI tunaacha kundi muhimu la watoto halafu tunasema tuje kufanya tena mradi mwingine? Hebu tuangalie kama tunaenda sawa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninaipongeza miradi hii ni mizuri ina nia nzuri ila tunachopaswa, hata huo mradi unaokuja tuzingatie na tuangalie watoto kwa sababu wimbi la ubakaji, wimbi la ulawiti na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa watoto wetu, watoto wamekuwa ni kundi la hatari sana. Watoto wapo kwenye kundi hatarishi. Kwa hiyo nitaomba sana na mradi mwingine na mwingine uweze kuzingatia hilo. Nimeipokea taarifa na nakushukuru Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango mwingine ni kuhusiana na masuala ya UKIMWI na Virusi vya UKIMWI kwenye maeneo ya visiwani. Hapa najumuisha visiwa vyote na nikizungumza kwa maeneo ya mialo ama visiwani kule Mwanza. Mkoa wa Mwanza hususan kwenye maeneo yake ya visiwa, maeneo mengi yanaongoza ya wagonjwa kutokufikiwa na huduma ya 953 kwa sababu ya nature ya jiografia ya mazingira yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali wana mpango kwamba ifikapo 2030, kuwa na maambukizi sifuri.

Kwa hiyo nataka tuangalie kama kwa namna hivi tunavyoenda, maeneo ya visiwani, matibabu ya huduma ya afya hayapo sawasawa. Utakuta tunacho kituo cha afya lakini idadi ya Madaktari hawatoshi ama vifaatiba havitoshi ama niseme kwamba wataalam hawatoshi kwa hiyo tunajikuta tunapambana ifikapo 2030 kufikia maambukizi sifuri, lakini kwenye maeneo kama hayo unakuta bado hatujafanya ama hatujayafikia sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza. Nataka kusema kama kuna kitu muhimu Watanzania tunakihitaji ni bima ya afya kwa wote. Tunahitaji bima ya afya kwa wote kuliko kitu kingine chochote. Watanzania tuache masihara na afya zetu, tunahitaji bima ya afya kwa wote. Nitakupa mfano, mgonjwa mwenye Virusi ya UKIMWI ama mwenye UKIMWI. Tunashukuru kwa mgonjwa huyu ambaye anapata matibabu ama niseme dawa bure kutoka Serikalini lakini ni vipi akipata magonjwa nyemelezi na hana bima ya afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, matibabu yamekuwa ghali sana, kwa maana hiyo kama hauna bima ya afya, mgonjwa anaumwa UKIMWI ama ana Virusi vya UKIMWI halafu ana diabetes, mgonjwa ana UKIMWI ama ana Virusi vya UKIMWI ana hypertension, mgonjwa mwenye UKIMWI ama ana Virusi vya UKIMWI ana hepatitis B ama C. Hebu angalia mgonjwa huyu atakuwa yuko katika hali gani. Ama hakika atakuwa yuko katika hali ya hatari sana kwa sababu magonjwa ya sukari, presha ni sehemu ya magonjwa yanayochukua bajeti kubwa ya Serikali kwa ajili ya kuwatibu Watanzania. Kwa hiyo naomba sana hili jambo Watanzania na Serikali tuliangalie ili tuweze kuharakisha jambo hili la bima ya afya kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwapongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya na dhamira yao njema ya kutaka kuhakikisha wanafikia maambukizi sifuri ifikapo 2030, lakini nitapenda kujua, Serikali ina mpango gani, ina mkakati gani na imejipanga vipi kuondokana na maambukizi mapya na tusifikie maambukizi sifuri ikifika mwaka 2030 kwa kuyafikia makundi yafuatayo: -

(a) Wanaojidunga;

(b) Wanaojiuza; na

(c) Wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema maambukizi sifuri 2030 lakini leo tuko 2023 na bado ipo changamoto kubwa kuyafikia makundi haya. Kwa hiyo nitapenda kusikia kauli ya Serikali mpango mkakati tumejipangaje kuweza kuyafikia makundi haya matatu ili kutimiza dhamira njema ya kufikia maambukizi sifuri ifikapo 2030.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)