Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja hizi mbili. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehema kunijalia afya na kunipa kibali cha kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali namna inavyofanya kazi. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Januari Makamba, Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya. Wasichoke waendelee kuwa wabunifu na kuendelea kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafsu hii kumponeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu kipenzi Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoandika historia Tarehe 22/12/2022 kwa uzinduzi wa ujazaji maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. Nampongeza sana Mama kwa kazi nzuri aliyoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza, naomba nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuandika historia kwa mara ya kwanza mwaka jana kuweza kuwasha umeme wa Gridi ya Taifa katika Mkoa wetu wa Kigoma. Nashukuru sana Mungu aendelee kuibariki Serikali yetu inayoongozwa na Mama yetu mpendwa kwa kuweza kuukumbuka Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma wakiwemo wanawake tunatoa shukrani nyingi sana kwa kuweza kutuunganisha kwenye Gridi ya Taifa. Mkoa wetu una Wilaya Sita, Wilaya zilizokwisha pata umeme huo ni Wilaya ya Kakonko Kibondo, Kasulu na Buhigwe. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri Januari Wilaya zile ambazo bado hazijapata neema ya kupata umeme huo, kwa maana ya Wilaya ya Kigoma Vijijini, Kigoma Mjini na Uvinza nazo ziweze kunufaika kwa kupatiwa umeme pindi itakapowezekana, kwa sababu tukipata umeme watu wa Kigoma tutaweza kuzalisha na kuweza kuwahamasisha wawekezaji waje kuwekeza katika Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu tayari umefunguka kwa sababu barabara zinaendelea kujengwa na tukipata umeme tutaweza kukimbia sawasawa na wenzetu ambavyo wamekuwa wakikimbia. Kwa mara ya kwanza umeme ule ulipokuja changamoto kidogo huwa hazikosi, ulikuwa unakatika katika lakini kwa sasa kutokana na jinsi Serikali inavyoendelea kuimarisha miundombinu nafikiri tutaenda vizuri tutaondokana na kukatika kwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya miradi ya umeme, miradi yake inatekelezwa kwa kusuasua nilikuwa ninaomba sasa, Serikali ijitahidi kuhakikisha miradi inakamilika. Kwa mfano, mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, mradi wa Rusumo na mradi wa Kinyerezi. Miradi hiyo ikikamilika itatusaidia sana kwa sababu umeme utakuwa ni wa uhakika na ninyi mnafahamu kabisa umeme ukikatika katika hatuwezi kufanya shughuli za uzalishaji kwa maana hiyo basi umeme huo wa miradi hiyo mikubwa ukikamilika utaweza kutusaidia kuondokana na tatizo la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Bwawa la Mwalimu Nyerere lingekuwa limeshakamilika sasa kwa vile mmeongezewa muda mjitahidi kuhakikisha mradi huo unakamilika mara moja. Pia, nilikuwa ninashauri upande wa REA, baadhi ya miradi ya REA imeshindwa kukamilika kwa wakati hali inayosababisha vijiji vingi kukosa umeme, kumekuwa na malalamiko wakati mwingine kwamba kuna ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kuunganishia umeme, naomba Serikali ijitahidi kuwasimamia wale Wakandarasi ambao walichukua kazi maeneo mbalimbali ili waweze kukamilisha kazi kwa wakati na kuweza kuwaondolea wananchi wetu adha ya ukosefu wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya, ninaamini mkifanya kwa kudhamiria tutaweza kuondokana na tatizo la umeme. Nakushukuru sana. (Makofi)