Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. STANSLAUS H. NYONGO - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, mimi tu niendelee kuchukua au kuomba fursa hii kwa maana ya kwamba nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia siku ya leo na hasa katika kuchangia hoja ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, tumepata wachangiaji wengi, Wabunge takribani 15 wamechangia na Mawaziri ambao wamechangia moja kwa moja kuhusiana na Kamati yetu ni Mawaziri wanne.

Mheshimiwa Spika, nishukuru tu kwamba wachangiaji wote wameungana na Kamati, wameungana na hoja zote za Kamati na mapendekezo ya Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niendelee tu kumpongeza, nimpongeze Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na hasa ya kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya Wizara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwapongeza Mawaziri ambao wanasimamiwa na Kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kwa kweli wamekuwa wanafanya kazi na kazi hiyo wanayoifanya ni ya ushirikiano wa hali ya juu na Kamati yetu. Hapa leo wamekuja kujibu hoja mbali mbali kwa kweli Mawaziri hawa wameonesha commitement ya hali ya juu kwa maana kwamba wanakwenda kutekeleza yale majukumu au yale maoni ambayo Kamati yetu imeyatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee tu kusema kwamba maazimio ya Kamati ambayo tunakwenda kuyapitisha leo hapa katika Bunge lako tukufu basi waende wakayasimamie, wayafanyie kazi kadri jinsi walivyotoa maelezoyao na jinsi tulivyoweza kutoa maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati baada ya kutoa maoni, wachangiaji wengi wameweza kuchangia na kabla sijaenda kwenye Wizara moja moja kuna hoja za jumla ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, katika michango yote ya Wabunge, jambo lililojitokeza kubwa zaidi ni suala zima la upungufu wa watumishi hasa katika sekta ya afya na sekta ya elimu kwa maana ya walimu.

Mheshimiwa Spika, katika taarifa yetu ya Kamati iliyopita ya mwaka jana, tulisema na tulisisitiza kwamba Serikali ichukue jukumu maalum au jukumu mahsusi kuhakikisha kwamba inaajiri walimu, madaktari na manesi ili kusudi waende wakatoe huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kusema kwamba ninaishukuru Serikali imechukua hatua za dhati, lakini bado jukumu ni kubwa, wanatakiwa waajiriwe walimu wa kutosha pamoja na watumishi wa sekta ya afya.

Mheshimiwa Spika, leo umesikia hapa masomo ya sayansi ni kilio kikubwa, upungufu wa walimu wa sayansi umeonesha unaendana kabisana failure ya wanafunzi katika masomo ya sayansi. Kwa maana hiyo, kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ufaulu mdogo wa wanafunzi katika masomo ya sayansi na upungufu wa walimu wa masomo hayo. Hivyo basi jukumu hili Serikali tunaomba ilichukuwe, ilibebe kwa hali ya upekee ili kusudi tuondokane na changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa zaidi ni ukatili wa kijinsia kwa kina mama na watoto. Nimshukuru sana na Mheshimiwa Waziri Mkuu leo ndiyo ilikuwa mada yake kuu. Ukatili wa kijinsia umezidi kukithiri na hata leo hapa Waheshimiwa Wabunge wamesema hata kwa watoto wa kiume napo tutupie jicho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili halipingiki ni lazima tuchuke hatua za kipekee. Sasa hivi ukiwa na mtoto wa kike unatakiwa umlinde, lakini ukiwa na mtoto wa kiume naye unatakiwa umlinde tena zaidi, haya yote nadhani ni vizuri tuamue kwa pamoja, tupambane na ukatilii huu wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine katika masuala ya kijumla ni afya ya akili; suala la afya ya akili limekuwa ni changamoto kubwa, tuchukue sasa juhudi za kipekee kuhakikisha kwamba tunapambana na matatizo ya akili ambayo wanachi wetu yanawakabili.

Mheshimiwa Spika, kwa Wizara ya Afya ni kwamba namshukuru sana Mheshimiwa Waziri ametoa commitement kubwa na kwa suala la MSD, tunaomba sana wawekezaji wa ndani wapewe nafasi na fursa kwa ajili ya kuzalisha dawa kwa ajili ya kuondoa changamoto ya upungufu wa dawa, lakini vilevile kwa ajili ya kufanya biashara katika nchi ambazo tuna mahusiano nazo kwa maana ya nchi za SADC na nchi za Afrika ya Mashariki.

Mheshimiwa Spika, vilevile suala la TMDA pamoja na TBS; yale majukumu ya TBS aliyozungumza Mheshimiwa Waziri na yeye ametoa support hiyo ni kwamba kweli majukumu ya chakula basi yarudishwe kwa TMDA aweze kuyashughulikia kwa sababu ana utaalamu wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, kwa Bodi ya Mikopo kwenye suala la Wizara ya Elimu, wewe katika Bunge lako hili hapa majuzi, Bunge lililopita uliweza kutoa, ulituongoza na Bunge likatoa ushauri kwa Serikali kwa wanafunzi ambao walikuwa hawajapata mkopo wapatiwe mikopo mara moja na waweze kuingia madarasani waendelee na masomo.

Mheshimiwa Spika, uamuzi huu ulikuwa ni uamuzi wa busara na wa kipekee na umakini wa hali ya juu uliotoka katika Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jana nashukuru Kaka yangu, Ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba hapa alisema kwamba Bunge hili, Wabunge wangekuwa kidogo makini wangetoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais. Naomba niseme umakini wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wa kusahauri Serikali iongeze fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi ulikuwa ni umakini wa hali ya juu kupita kiasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze sana wewe, ninakupongeza sana na Bunge lako kwa maamuzi haya, tunaomba na tumesema katika taarifa ya Kamati, Bodi ya Mikopo iongezewe fedha. Udahili wa wanafunzi siyo suala la dharura. Udahili wa wanafunzi ni suala linaloweza kufanyiwa forecasting ya kutosha, fedha iliyotoka, Shilingi Bilioni 570 ilijulikana, na udahili wa wanafunzi kwa mwaka huu uliongezeka na Bodi ya Mikopo ilitoa taarifa kwa Wizara ya Fedha ili iongeze fedha kwa ajili ya mikopo, tunaomba siku nyingine Wizara itambue kwa wepesi na kwa haraka kwamba kuna ongezeko la udahili ili iweze kuongeza fedha kwa ajili ya kuwapa wanafunzi mikopo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile suala la maendeleo katika Sekta ya Maendeleo ya Jamii, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha sekta hii au Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii. Ukatili unaoendelea, msimamizi mkuu wa masuala haya ni Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum. Waziri huyu ana instrument yake. Yanapotokea matukio kama haya wakati mwingine yeye ndiyo anatakiwa akemee. Hivyo basi, tuangalie Serikali iangalie kwa umakini, Wizara hii ikiwezekana iwe chini ya ofisi kubwa za Serikali, aidha iwe chini ya Waziri Mkuu au iwe chini ya Makamu wa Rais, au iwe chini ya Ofisi ya Rais ili Waziri huyu anapoona kuna suala lolote la kukemea au suala lolote ambalo linaonekana kuna uvunjifu wa amani au ukatili wa kijinsia awe na power ya kumwambia Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Sheria, Waziri wa Elimu au Waziri yeyote ambaye anashughulika na watoto na akina mama awe na power hiyo, nadhani hili tutakwenda vizuri zaidi tukilirekebisha. (Makofi)

SPIKA: Dakika moja malizia Mheshimiwa.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mwisho kwa Wizara ya Utamaduni na Michezo, tunawashukuru sana na tunampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya. Wizara hii ilikuwa haionekani sasa hivi imekuwa ni Wizara ya mfano, wanafanya kazi vizuri sana, hivyo waendelee kujenga viwanja, waendelee kuhakikisha kwamba vijana wa Kitanzania wenye talent za kufanya michezo au kucheza michezo mbalimbali waweze kuonesha talent zao, na iwe chanzo cha vijana hawa kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, matajiri vijana na watoto wanatokana na talents. Matajiri wanaotengenezwa katika umri mdogo ni wale wenye vipaji maalum. Wizara hii tukiiwezesha, tutapata matajiri vijana kutokana na vipaji walivyonavyo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niseme sasa naomba kutoa hoja. Ahsante.

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Spika, naafiki.