Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii inayoongozwa na Mheshimiwa Mbunge Stanslaus Haroon Nyongo kwa maoni na ushauri wao katika kuboresha utoaji wa Huduma za Afya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli nami nasema kwamba naishukuru sana Kamati, hawakueleza mambo mengi, sana sana mambo ambayo yameibuka katika maazimio ya Kamati au maoni na ushauri wa Kamati ni mambo matano na nitayatolea ufafanuzi kama kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu utengwaji wa bajeti kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Wizara na kutekeleza miradi ya maendeleo, tumelipokea, na niseme kwamba Serikali naendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za sekta ya afya na pia kwa miradi ya maendeleo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli huduma za afya ni moja ya vipaumbele vyake. Kwa hiyo, hili suala tunahakikisha kwamba fedha zitakuja.

Mheshimiwa Spika, pia tuliahidi Bunge lako Tukufu tunapata pia fedha za maendeleo kutoka kwa wadau wa maendeleo, nazo tutazisimamia kikamimilifu kuhakikisha kwamba sambamba na fedha zinazopitishwa na Bunge, lakini pia fedha hizi za wadau wa maendeleo nazo zinatumika kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ya Kamati ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunaimarisha utendaji wa Taasisi ya Dawa na Vifaa Tiba ili kuzuia uingizwaji wa bidhaa bandia za chakula dawa na vipodozi. Hili nalo tunalipongeza na tumetunga kanuni ambayo inasimamia uingizaji wa dawa katika mipaka 15.

Mheshimiwa Spika, naomba nikiri. Kweli tunayo changamoto kwa sababu ya mipaka yetu isiyo rasmi. Kwa hiyo, tupo katika mipaka rasmi, hivyo ni kweli mipaka ambayo siyo rasmi dawa zinaingizwa na vifaa tiba ambavyo havina ubora. Tumeamua kung’atua madaraka ya TMDA kwa watu ambao ni wataalamu wa dawa katika ngazi za Halmashauri, na wenyewe tumewapa vitambulisho, wanaweza wakafanya pia ukaguzi wa dawa na vifaa tiba katika maduka ambayo yako mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo tumeliona ni kuimarisha utendaji wa Baraza la Wafamasia. Sasa hivi Baraza la Wafamasia wanafanya ukaguzi wa maduka ya dawa na sehemu za kuhifadhi dawa, TMDA naye anafanya. Kwa hiyo, tunataka Baraza la Wafamasia wao wasimamie fani; wataalamu wa famasia, kama Baraza la Madaktari na Baraza la Wauguzi yanavyofanya, halafu tumwachie TMDA mamlaka ya dawa na vifaa tiba kazi ya kukagua premises (maduka ya dawa). Kwa hiyo, Baraza la Famasia akienda kwenye famasi au sehemu yoyote anamwangalia mwanataaluma, siyo suala la dawa, vifaa na vifaa tiba. Tunaamini kwa hatua hii pia itaimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa dawa na vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo pia limeelezwa na Kamati, na Mheshimiwa Hhayuma ambaye pia ni mtaalamu wa eneo hili, ni kuhakikisha kwamba tunaratibu udhibiti wa chakula na vipodozi ndani ya Serikali. Suala hili lilifika kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, tayari linafanyiwa kazi ndani ya Serikali kati ya TBS na TMDA. Naamini Serikali itafanya maamuzi kuhusu udhibiti na usimamizi wa chakula na vipodozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli anachokisema Mheshimiwa Hhayuma na Kamati, dawa na vipodozi vinauzwa katika sehehmu moja. Pia sasa hivi tumeona kuibuka kwa supplements, vitamins; sasa regulator siyo tena mtu ambaye anasimamia public health. Kwa hiyo, ni jambo ambalo tumeliona ndani ya Serikali tunaamini kwamba suluhisho litapatikana.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la MSD (bohari ya dawa). Tunaishukuru sana Kamati, na kipekee kwa kweli tunapongeza maboresho ambayo yameanza kuonekana ndani ya MSD, na Kamati sasa inatushauri tuweke mikakati thabiti ya kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa Viwanda vya Dawa na Vifaa tiba vinavyozalishwa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, jambo hili tunalikubali. Nami nilishawaelekeza MSD, as long as dawa au kifaa tiba kinazalishwa na kiwanda cha ndani chenye ubora na bei; na bei tumesema kama dawa hiyo au kifaa tiba hicho kinazalishwa na kiwanda cha ndani cha Tanzania, bei yake imezidi kwa asilimia 15 wanunue bidhaa hiyo ambayo inazalishwa ndani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kutoa mfano. Tumeanza kununua IV fluids kutoka Kairuki Pharmaceticals badala ya kununua kutoka Uganda. Nitoe rai kwa wazalishaji wa ndani wa dawa na vifaa tiba. Naogopa isije kutokea tukapiga marufuku tusinunue kutoka nje ya nchi, lakini labda hawana uwezo au capacity ya kukidhi mahitaji ya dawa na vifaa tiba ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nilikutana nao mwezi Januari, tumekubaliana. Kwa hiyo, tutafanya tathmini; huyu uwezo wake ni kuzalisha dawa zipi na kiasi gani? Tukishajua tumeshamwelekeza MSD, marufuku kuleta dawa kutoka nje ya nchi kama dawa hiyo inapatikana ndani ya nchi na ina ubora na pamoja na suala la gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wazalishaji wa ndani wa viwanda vya dawa pia wametuambia, tukinunua nje ya nchi, tunawapa Letter of Credit, ndani ya nchi hatuwapi chochote. Kwa hiyo, suala hili tayari nimemwomba Waziri wa Fedha, tutakutana nao. Hata kama hatutawapa Letter of Credit, lakini tuangalie kama tunaweza tukawapa advance amount ili waweze sasa kujipanga vizuri kununua raw material ili waweze kuzalisha dawa na vifaa tiba ambavyo vinahitajika ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limeelezwa na Kamati ni kuimarisha tafiti za ubora athari na matumizi salama ya tiba asili chini ya NIMR, Medical Research Institute, Taasisi ya Magonjwa ya Binadamu. Tunapokea ushauri wa Kamati, tutalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunaona ni kweli, kuna ujanja ujanja. Utaambiwa dawa hii inatibu saratani, dawa hii inatibu kisukari, dawa hii inatibu magonjwa ya moyo, lakini ukiangalia ufanisi (efficacy) wake, tumeona Watanzania pia wanaibiwa. Ila kwa kweli tunakubali kwamba wapo Watanzania ambao wanatengeneza tiba asili ambazo zingeweza kusaidia na kuokoa maisha ya wengi. Kwa hiyo, tutaongeza fedha za ndani kwa NIMR kama kamati ilivyo tushauri ili weweze kufanya utafiti.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limeelezwa na kaka yangu Mheshimiwa Kakunda, nimelipokea kuhusu michoro ya vituo vya kutoa huduma za afya, tutaliangalia. Naomba nitahadharishe, tujengeni miundombinu ya kutoa huduma za afya kwa kuangalia mahitaji ya sasa na mahitaji ya miaka 20, 30 inayokuja. Maana sasa hivi jinsi unavyoboresha huduma, ndivyo wananchi wanavyodai huduma bora zaidi, ndivyo wananchi wanavyodai huduma za ngazi ya juu zaidi kuliko zahanati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nakubaliana na kaka yangu Mheshimiwa Kakunda katika suala la gharama, lakini gharama hii itakidhi mahitaji ya sasa ya kutoa huduma za afya kwa kizazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: dakika moja Mheshimiwa Waziri umalizie.

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Kakunda tumepokea ushauri wako, tutaufanyia kazi, tutatoa michoro kwa kushirikiana na TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, naomba nimalize kwa kukushukuru sana lakini kuishukuru Kamati yetu ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, wanafanya kazi kubwa na nzuri sana ya kutushauri, nasi tunawaahidi kwamba tutaboresha utoaji wa huduma za afya especially tunapoelekea kwenye Bima ya Afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)