Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia wasaa na mimi wa kuweza kutoa mchango wangu kwenye hizi Kamati zetu mbili, USEMI, lakini na Huduma. Ninawashukuru na niwapongeze Kamati kwa kazi kubwa waliyoifanya, hususan Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuwasemea wana-Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Spika, wakati tunapata uhuru ardhi ya Manispaa ya Dodoma au ya Halmashauri wakati huo ya Dodoma ilikuwa chini ya wana-Dodoma, lakini mnamo mwaka 1973 Serikali ikaamua kuiweka ardhi yetu chini ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA), ili Dodoma kama Makao Makuu ya nchi iweze kupangwa na kupangika ili ifafane na miji mingine duniani.

Mheshimiwa Spika, CDA ikaishi takribani miaka 43 kuanzia mwaka 1973 mpaka 2016 ambapo Hayati Rais John Pombe Magufuli aliamua kuivunja CDA. Ilivunjwa kwa sababu CDA hawakuweza kufanya kazi ya kupanga Mji badala yake walikuwa ni chanzo cha migogoro kwa wana-Dodoma. Tukaivunja, ikavunjwa CDA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matarajio ya wananchi wa Dodoma yalikuwa baada ya kuondolewa CDA ardhi yao imerudi Halmashauri kwamba, wana-Dodoma sasa watakwenda kumiliki ardhi yao na migogoro itakwenda kuisha. Kwa bahati mbaya sana hivi tunavyozungumza wananchi leo wa Dodoma wanasema ni afadhali ya CDA kuliko ardhi ilivyorudi kwenye Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Spika, hawa Watumishi baadhi baada ya CDA kuvunjwa, baadhi walipelekwa kwenye Halmashauri zingine, baadhi wamebaki ndani ya Jiji la Dodoma kwenye kitengo cha ardhi. Mkurugenzi leo wa Dodoma ndiye aliyekuwa Afisa Mipango ndani ya CDA. Leo ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, anafahamu vizuri suala la mgogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tuna hati wananchi kiwanja kimoja kina hati zaidi ya tatu. Wale wenye fedha wenye mabavu ndiyo wanaoweza kumiliki ardhi leo kwenye Jiji la Dodoma, wale wanyonge hawawezi kumiliki ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, kwenye ushirikishwaji wa upangaji ama wa upimaji wa ardhi, makubaliano yalikuwa ardhi yako ukionesha unatoa asimilia 10 kwa ajili ya barabara, asilimia 30 wanachukua Jiji, asilimia 70 unapewa mwananchi, haifanyiki hivyo. Wale wengine ambao wana viwanja vidogovidogo wanaunganishwa hapo baadae wakija kuhoji viwanja vyao viko wapi wanaambiwa kimeliwa na barabara, kwa hiyo huna kiwanja. Hayo ni mateso wanayopitia watu wa Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Spika, hiki kitu iinaumiza sana. Tuna wajane, tuna wagane, tuna watoto yatima wako hapa ambao leo wananyimwa ardhi yao kwa sababu ya Watanzania wenzetu ambao tumewapa nafasi, waweze kuwasaidia na wao watoke kwenye wimbi la umaskini walilonalo, wao wako wanaatamia ile ardhi, wanaitumia wanavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati imesema kwamba, watu wachukuliwe hatua kuhusiana na suala zima la migogoro ya ardhi ya Dodoma. Naomba niongezee, hawa watu ambao walikuwepo tangu CDA na mpaka leo bado wako pale ofisini wapaki magari yao pembeni, uchunguzi upite, wakiwa wao wako pembeni, ili tujue shida iko wapi Dodoma, kwa nini Dodoma na siyo sehemu nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nihame kwenye suala zima la Dodoma, naomba niende kwenye suala zima la elimu. Tunashukuru Serikali kwa kutuongezea madarasa kwenye shule zetu mbalimbali, lakini wakati tunaomba haya madarasa wakati mwingine na sisi huku vijijini ama kwenye maeneo yetu tunakuwa tunaendelea kuwaza tufanye nini ili watoto wetu waweze kupata elimu yenye mazingira rafiki.

Mheshimiwa Spika, tunayo changamoto moja Halmashauri ya Wilaya ya Chemba. Tulipewa Shilingi Milioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa Saba shule ya Sekondari Mrijo. Kata ya Mrijo ina Vijiji Saba, Vijiji Vitatu mwanafunzi anatakiwa kutembea zaidi ya kilometa 60 kwenda na kurudi. Wananchi wakaamua kujihamasisha waweze kutoa Kijiji ambacho kipo katikati wajenge, waanzishe pale shule ili waweze kujenga shule nyingine ya sekondari, waache shule mama ya Mrijo waje wajenge shule nyingine pacha ya Mrijo ambayo itakuwa inaitwa Mrijo Juu.

Mheshimiwa Spika, sasa tukawaomba na wananchi wakajitolea, wamefyatua tofali, wamesomba mchanga, wamesomba…

SPIKA: Sekunde 30, malizia.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, tukawaomba Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa haya madarasa saba badala ya kupelekwa pale Mrijo Chini ambako tuna madarasa 24 tunaomba tuyalete huku Mrijo Juu ili wanafunzi wetu ambao wanatembea zaidi ya kilometa 60 kwenda na kurudi tuwapunguzie huo umbali ili waweze kusoma katika mazingira rafiki, lakini Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hawajaweza kutuelewa hilo. Kwa hiyo, niombe sana hebu watuone kwenye jicho hilo, kutembea kilometa 60 ni mtoto wa Mbunge gani anayeweza kutembea kilometa 60 kwenda na kurudi halafu sisi tunawanyima wananchi wetu kwa kodi zao wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenye suala hili waweze kuliangalia vizuri. Nakushukuru kwa wakati. (Makofi)