Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nami nitumie nafasi hii kuzipongeza Kamati zote mbili, kwanza, kwa kuandaa taarifa nzuri na kuziwasilisha vizuri sana. Mmeeleweka vizuri sana Wabunge wenzetu, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sio Mjumbe wa Kamati mojawapo, lakini ni mdau. Kwenye hizi Kamati mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti. Kwa maana hiyo, kama mdau, napenda nichangie jambo la kwanza kabisa kuunga mkono hoja zote mbili za Kamati na kuziwekea msisitizo kwamba, ninaomba Serikali izizingatie, na kwenye utekelezaji waweze kutekeleza yale yote mazuri ambayo yameshauriwa. Maana yake huo ni ushauri wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwenye utekelezaji tunachoangalia ni utekelezaji wa sera. Sera karibu zote ni nzuri. Kwenye utekelezaji kuna kitu kinaitwa usimamizi. Naipongeza Serikali kwa kipindi cha miaka hii kumi, kumi na tano kumekuwa na uboreshaji mkubwa sana wa usimamizi. Kwenye sekta ambazo zinazozungumzwa sana kwenye zile taarifa mbili napongeza sana usimamizi ambao umekuwa mzuri sana kwenye sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ujenzi wa madarasa yote ya Shule za Msingi na Sekondari umekuwa ni mzuri na unazingatia thamani ya fedha iliyotumika (value for money). Ndiyo maana unaweza ukampa Afisa Elimu wa Msingi ukamwambia nakupa Shilingi milioni 20, jenga darasa na uweke humo ndani madawati, ubao, kiti cha Mwalimu na meza ya Mwalimu na Shilingi milioni 20 inatosha.

Mheshimiwa Spika, sasa tatizo liko wapi? Bado tatizo liko kwenye sekta ya afya. Hii naisema kabisa kwamba bado tatizo la usimamizi kwenye sekta ya afya ni kubwa. Mimi binafsi nimeshawasiliana na Mheshimiwa Waziri, Naibu, na ninamshukuru sana Naibu Waziri Mheshimiwa Dugange tumeshawasiliana tayari kwa yale maeneo ya kwenye jimbo langu ambayo yanahitaji kuboreshwa.

Mheshimiwa Spika, nisisitize kwamba ili tufanikiwe vizuri kwenye sekta ya afya, bado tunahitaji kutekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri ya mwaka 2006 yaliyosema ili tutoe huduma za afya vizuri kwa watu wote, tunahitaji kila kijiji kiwe na zahanati, kila kata iwe na kituo cha afya, kila wilaya iwe na hospitali ya wilaya, kila mkoa uwe na hospitali ya rufaa ya mkoa, kila kanda iwe na hospitali ya rufaa specialized ya kanda; na kwenye hospitali ya Taifa kuwe na uboreshaji wa maeneo maalum kwa ajili ya magonjwa maalum na utaalam maalum kama ambavyo wanafanya katika Hospitali ya Muhimbili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika utekelezaji, maeneo haya ya hospitali ya Taifa, hospitali za kanda, hospitali za mkoa na hospitali za wilaya napongeza sana sana. Bado tunadaiwa sana kwenye vituo vya afya, kata nyingi bado hazina vituo vya afya. Vile vile tunadaiwa kwenye vijiji. Kwangu nina vijiji 71. Vijiji ambavyo vina zahanati ni 27, ambavyo havina zahanati kabisa ni 44.

Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Skonge kilometa za mraba 28,773 kutoka kijiji kimoja kwenda kingine ni zaidi ya kilometa 10. Kwa hiyo, wananchi wangu wapo ambao wanatembea kilometa 20 kwenda kuikuta tu zahanati. Sasa katika hali kama hiyo, tunakwenda kwenye Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ninaamini katika watu ambao watapata shida na wataanza malalamiko ni watu wangu. Watachangia Bima ya Afya halafu ili apate huduma anatakiwa atembee kilometa 20 au 15 kwenda kukuta zahanati. Kwa hiyo hili jambo la ujenzi wa zahanati naomba sana litiliwe mkazo na lipewe kipaumbele na Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwenye utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri, kulikuwa na mkwamo ambao ulianzishwa na wataalamu wetu wahandisi. Walipoambiwa choreni ramani sasa ambayo itatumika kujenga zahanati kila Kijiji, wakaenda kuchora ramani kubwa; vyumba zaidi 20 kwa ajili ya zahanati ya Kijiji. Matokeo yake ikashindikana kujenga zahanati kwa wakati kwa sababu fedha iliyohitajika ni kama Shilingi milioni 250 hadi 300 kwa zahanati. Kwa hiyo, malalamiko yalikuja kwa wananchi kwa sababu wanajitolea, ikapunguza kidogo lakini bado usimamizi kwenye eneo hili la gharama.

Mheshimiwa Spika, nina wasiwasi mkubwa sana. Ni kitu gani ukiangalia kinahitajika kwenye zahanati? Kuna maeneo saba ya muhimu sana kwenye zahanati, yaani point source of service. Eneo la kwanza kwenye zahanati ni mapokezi; eneo la pili, kumwona mganga; eneo la tatu, maabara, eneo la nne, chumba cha dawa; eneo la tano, chumba cha sindano; eneo la sita, chumba cha kufunga vidonda na upasuaji mdogo kama upo; eneo la saba, ni chumba cha dharura au mapumziko. Hivi vyumba saba ndiyo vyumba vya priority kwenye zahanati. Kwa hiyo, unahitaji gharama ndogo sana kujenga vyumba saba hivyo, na hasa kwenye mapokezi wala haiwi chumba. Kwa hiyo ni vyumba sita. Kwenye mapokezi pale linaweza likawa ni eneo la wazi tu wanapokelewa pale, lakini vyumba sita ndiyo vya muhimu sana kwenye zahanati.

Mheshimiwa Spika, we need just a point of service, mtu anakwenda, anahudumiwa, anarudi nyumbani. Kama mtu amezidiwa, ndiyo atapelekwa kwenye kituo cha afya kwa maelekezo ya Mganga.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ni muhimu kwenye eneo la zahanati ni nyumba ya Waganga. Kwa hiyo, unaweza ukajenga nyumba aidha two in one au three in one. Kwangu kule kuna Kijiji kinaitwa Utimule, wamejenga nyumba ya two in one ambayo ni ya gharama nafuu kabisa. Kama Wizara ya Afya na TAMISEMI wanataka kuja Sikonge waione ile nyumba…

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kakunda, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa ajili ya muda, naomba tu kumkumbusha pamoja na jitihada ya kutetea zahanati katika eneo la muhimu alilosahau ni sehemu ya kujifungulia wakati anataja zile sehemu za muhimu katika zahanati, ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Kakunda unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, naipokea, lakini mara nyingi kwa sababu ni kwenye kijiji kile chumba cha dharura ndiyo mara nyingi huwa kinatumika kama sehemu ya kujifungulia, lakini baadae kwa sababu anapokea fedha za RBF wanaweza wakatumia fedha za RBF kujenga chumba maalumu cha kujifunguliwa, lakini kwa kuanzia unaweza ukaanzia na vile vyumba sita nilivyosema.

Mheshimiwa Spika, ya pili ni nyumba ya waganga, halafu ya tatu ni kichomea taka na ya nne ni choo cha wanaume na wanawake na mwisho kabisa ni umeme na maji. Kwa hiyo, ukiwa na huduma hizi tano tayari unakuwa umeshakuwa na zahanati ambayo inaweza ikahudumia wananchi kwenye kijiji baadae uboreshaji utaendelea.

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye gharama; mimi nimepanga gharama hapa ukinipa milioni 35 naweza nikajenga jengo la zahanati kwa kushirikiana na wananchi, kwa sababu tayari wananchi wameishachangia unaweza ukajenga jengo la zahanati; ukinipa milioni 40 naweza nikajenga nyumba ya waganga, two in one au three in one; ukinipa milioni 10 naweza nikaweka vyoo vya ku-flash (choo cha mwanaume na choo cha wanawake); halafu ukinipa milioni 10 nyingine naweza nikajenga kichomea taka, ukinipa milioni tano naweza nikagharamia umeme na maji kwa mwaka, ina maana hiyo ni bajeti ya shilingi milioni 100 inatosha kabisa kujenga jengo la zahanati kwenye kijiji, nyumba ya mganga na hizi huduma zingine.

Mheshimiwa Spika, sasa wasiwasi wangu mkubwa uliopo ni kukosa uzalendo kwa watu wetu ambao tumewaamini kusimamia utekelezaji. Mimi namshukuru sana Dkt. Dugange nimeshampa mfano, nimempa mfano wa zahanati ya Mwamayunga.

Mheshimiwa Spika, zahanati ya Mwamayunga ilianza kujengwa mwaka 2009 kwa fedha za kutoka ADB…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 malizia.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi ile zahanati imetumia shilingi 158,300,000 na bado haijakamilika.

Mimi naomba sana eneo la usimamizi naomba sana liboreshwe. Mtamuona baadae Mheshimiwa Waziri wa Afya naona alikuwa anaandika andika ili nimpe data tuweze ku-share. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)