Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Naomba nianze kuchangia kwenye Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba mwaka jana Serikali iliongeza bajeti ya TARURA, lakini bado kuna matatizo makubwa ya barabara. Katika Mkoa wa Dar es Salaam, kama kila siku tunavyoongea Wabunge wa Dar es Salaam, wakazi wa Dar es Salaam wanatumia sana barabara kwa sababu Mkoa wa Dar es Salaam ni mkoa wa kibiashara na watu wengi wanapofanya biashara wanatumia barabara. Kwa hiyo kwa mpango ambao unaenda nao TARURA, TARURA ni kila mara bajeti yao haitoshi na kwa sasa hivi kwa huu mpango wa kugawana fedha kwamba mfano, Mkoa wa Dar es Salaam ugawane na mkoa mwingine tuseme kama vile labda Mkoa wa Kigoma au mikoa mingine ambayo haina watu wengi.

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Dar es Salaam bado tunahitaji sana barabara kwa sababu wananchi wetu kazi zao nyingi zinatumia barabara na zinatokana na barabara.

Mheshimiwa Spika, ninaongea kuhusiana na barabara za Mkoa wa Dar es Salaam specially Jimbo la Segerea, bado tunahitaji barabara. Nasi watu wa Dar es Salaam hatuhitaji tena barabara za changarawe. Kwa hiyo, katika Mkoa wa Dar es Salaam, barabara hizi za TARURA tunaomba tuongezewe bajeti ili wafanyabiashara wetu waweze kufanya kazi vizuri na mapato yaweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalopenda kuongelea ni kuhusiana na mradi wa DMDP. Mradi wa DMDP Phase II mpaka sasa hivi ninavyoongea haujamalizika. Bado kuna sehemu nyingi sana zina matatizo. Mfano, Stendi ya Kinyerezi. Stendi hii imejengwa, ni nzuri, lakini haina sehemu ya kupumzikia, haina sehemu ya kusimama, yaani bado haijamalizika, na hii iko kwenye phase II. Mpaka sasa hivi mradi wa DMDP Phase II haujamalizika na hii inaifanya mpaka hii DMDP Phase III ambayo ametoka kuiongelea hapa Mbunge aliyemaliza kwamba itaanza, tuliambiwa kwamba wanaanza mwaka 2022 mwezi wa Tatu, lakini mpaka leo hizi barabara hazijaanza; ilikuwa pamoja na Bonde la Msimbazi, halijaanza.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoongea hapa mwenzangu kwamba tunavyoenda kuwatangazia wananchi kwamba kuna miradi ambayo inategemea kuanza kwenye makazi yao halafu mradi hauanzi mpaka mwaka mmoja unapita, ni shida sana kwetu Wabunge kwenda kujielezea kwa nini huu mradi umesimama mpaka sasa hivi. Mpaka sasa hivi hatujui huu mradi utaanza lini? Tulikuwa tunaomba Mheshimiwa Waziri akija kujibu, basi atuambie huu mradi wa DMDP utaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ninachotaka kuongelea; hili ninalotaka kulisema, siyo kwamba siungi mkono wafanyabiashara kuondolewa barabarani. Ninachokipinga mimi, tumesema sawa wafanyabiashara wanaondolewa barabarani, mfano Kariakoo na sehemu nyingine ambazo kuna watu wengi. Siku hizi kumekuwa na tabia, mtu anatoka jijini ndani kabisa huko mjini, anakuja sehemu kama Bonyokwa, anamkuta mama wa watu anajiuzia nyanya; anavunja lile banda la kuuzia nyanya, anachukua na zile nyanya. Anasema ni kwa sababu yule mama amekaa barabarani. Hiki siyo kitu kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaunga mkono kwa maeneo ya nje, hao waliokaa barabarani kuondolewa ni sawa, kwa sababu ni pamoja na usalama wao; lakini hawa ambao wapo kwenye mitaa; mtu anakuja kumvunjia au kumwondolea mtu biashara yake sehemu ambayo hata Manispaa haijajenga barabara, hakuna kitu chochote ambacho kinahusiana na Serikali imefanya hilo jambo, ametengeneza kibanda chake yuko sehemu ya vumbi, mtu anatoka huko anakuja anamwondolea chakula chake, na biashara zake na ukiangalia ile sehemu hakuna hata gari moja linalopita. Sasa unapomwondoa pale, atapitiwa na gari gani? Kwa sababu barabara mbovu au hakuna barabara inayopita hapo, unakuja unamwondolea, huo ni unyanganyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba kabisa TAMISEMI iangalie ni jinsi gani hawa watu wake inawaelekeza. Kwa sababu hawa watu ambao wanaitwa Mgambo wanakuwa hawana busara, kwa sababu kwa akili za kawaida umemkuta mtu, unamnyang’anya vitu vyake, halafu unavichukua unaenda navyo Manispaa, siyo vizuri. Hili jambo liishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wote wa Kinyerezi ambao wako mtaani, mtu kaweka banda nje ya nyumba yake, wamebomolewa na hakuna kitu chochote ambacho kinafanyika. Hilo naomba watakapokuja waweze kutusaidia kwamba hawa Mgambo wavunje huko Kariakoo au sehemu nyingine ambazo kuna watu wengi, lakini huku wamama wanapojifanyia biashara, maisha yenyewe sasa hivi ni magumu, wamama wanajihangaikia, wanawafuata kule kule kwenye mitaa ya ndani kwenda kuwavunjia, siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni kuhusiana na tathmini ambayo inaendelea kwenye Jimbo langu la Segerea. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hawa watu wamekaa tangu mwaka 1997, naishukuru Serikali sasa hivi inawafanyia tathmini na imepeleka daftari la uhakiki. Naomba watakapomaliza uhakiki hizi fedha ziwepo. Isije tena ikakaa miezi mingine sita.

Mheshimiwa Spika, ikikaa miezi sita, zoezi limefutika tunaanza upya. Kwa sababu sheria inasema kila baada ya miezi sita. Tangu tumeanza kufanya tathmini, sasa tuko mwezi wa Tano, bado tuna mwezi mmoja. Kwa hiyo, naiomba kabisa Wizara ya Fedha, tutakapomaliza, tuna siku 19 waende wakawalipe hawa wananchi ili waweze kuondoka. Tusije tena tukakaa miezi sita halafu ikaonekana kwamba hela hazijawa tayari. Kwa hiyo, wananchi wangu nitakuwa nao, nitawaambia tunaanza tathmini upya.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Nimesikia hiyo. (Kicheko)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kuongelea ni kuhusiana na walimu.

MBUNGE FULANI: Ehe!

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Tunaishukuru sana Serikali, imeweza kuleta pesa nyingi sana ajili ya kujenga madarasa na kutengeneza miundombinu ya elimu. Tulikuwa tunaomba Serikali iajiri walimu ili hiyo kasi ya kuwa na madarasa mazuri iendane na uwepo wa walimu wa kufundisha. Kama wenzangu walivyosema kwamba darasa moja anafundisha mwalimu mmoja, tutakuwa hatupati matokeo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia madarasa yaendane na miundombinu ya walimu kwa sababu mwalimu anapokuwa anafundisha yuko kwenye darasa zuri, lakini hana ofisi nzuri ya kukaa. Naomba hizi pesa zinazoletwa ni nyingi sana, tunashukuru, lakini zinaletwa tu kwa ajili ya madarasa, hakuna ofisi za walimu. Tunaomba walimu pia wajengewe ofisi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru. (Makofi)