Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja za Kamati zilizopo mezani kwetu. Ninataka kuchangia mambo mawili. Jambo la kwanza ni kuhusu Mradi wa SEQUIP na jambo la pili ni Wizara ya Michezo.

Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa ujenzi wa shule za kata ambao umefanywa na Mheshimiwa Rais, karibu kata zote nchini. Kwa kweli sisi kama Wabunge huko majimboni tumepata kitu kikubwa cha kukisema na wananchi ambao walikuwa hawana matumaini kabisa ya kuwa na shule lakini sasa wana shule kupitia huu Mradi wa SEQUIP, na sehemu kubwa hii miradi ya shule Mheshimiwa Rais ametoa fedha na wananchi wametoa nguvu kazi kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, lakini, hoja yangu ni nini ambayo napenda kuishauri Serikali; kwenye hii miradi ya SEQUIP ambayo imelenga kwenye kila kata, ukizingumzia kila kata, si kata zote zinahitaji hiyo shule moja. Kuna kata zingine kwenye miji kwenye majiji zinahitaji zaidi ya shule mbili. Sasa tuone haja ya Serikali kuongeza kwenye kata mbali mbali kwa sababu idadi ya wanafunzi imekuwa ni wengi kwenye kata mbali mbali. Kwa hiyo tungeweza kuongeza idadi ya shule kwenye kata hizo ili iweze kuendana na wingi wa wanafunzi ulipo pale.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, kwa sisi kwenye Kamati yetu tumezungukia tumeona kwamba kumekuwa na variation kubwa sana ya ujenzi wa shule hizi. Ukienda kwenye halmashauri mbali mbali kuna halmashauri ambazo zina upungufu wa zaidi ya milioni 51 ili kukaimisha ujenzi wa shule hii, lakini kuna halmashauri zingine zimefika hadi milioni 150 zinahangaika kutafuta hizo fedha ili zikamilishe ujenzi wa shule hii. Hii inatokana na umbali wa shule zilizopo pamoja na upandaji wa gharama za vifaa kwenye ujenzi wa shule hizi. Sasa Serikali ione concern, shule ambayo ipo Namanyere haiwezi kuwa sawa sawa na shule ambayo iliyoko Dar es Salaam kwenye gharama za ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni vyema Serikali ikaona namna gani ya kuweza kuziunga, kuzi-support au kuziongezea nguvu kuliko kuwaachia Wakurugenzi na halmashauri waendelee kuhangaika na ujenzi wa shule hizi ili ziweze kukamilika. Milioni 470 tu haiwezi kutosha, hata mimi kule Makete bado na changamoto ya fedha nyingi ambazo nazihitaji kwa ajili ya ujenzi wa shule hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ni kwenye suala la Wizara ya Michezo. Nimesikiliza hoja ya Kamati. Kwenye suala la Wizara ya Michezo, mimi kama Mbunge nina hoja ambazo zinazungumzia kwenye suala la ujenzi wa shule zile za michezo lakini pia kwenye suala la viwanja nchini. Kamati imeshauri kwamba Wizara ione utaratibu wa kufanya partnership na sekta binafsi. Mimi ninauliza, leo tunaenda karibu robo ya tatu ya utekelezaji wa bajeti, lakini hadi dakika hii ninanvyozungumza kwenye ujenzi wa viwanja nchini hakuna chochote ambacho tumeanza kukifanya. Watanzania wana swali kubwa sana huko nje, tumekuwa tukipigia kelele kuhusu ubora wa viwanja vya Taifa letu, na Serikali ilikuja hapa ikatuahidi kwamba kutokana na bajeti ya bilioni 10
kwenye viwanja saba ambavyo tumeitengea itaanza mchakato wa ujenzi wa viwanja.

Mheshimiwa Spika, mimi niiambie Serikali, suala la michezo nchini limekuwa ni suala ambalo linaleta fedha nyingi kwenye Pato letu la Taifa. Kwa mwaka 2020/2021 Serikali imeingiza zaidi ya bilioni tatu kupitia mapato ya magetini kwenye mpira wa miguu. Vilevile, Azam (Bakhresa) amewekeza zaidi ya bilioni 225 kwenye kudhamini ligi kuu, na analipa zaidi ya bilioni 34 VAT. Hivi ninavyozungumza, jitihada za Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara husika tunaziona, lakini je wamepata fedha zozote za kuanza mchakato huu? Tuliahidiwa kwamba watajenga shule 56 za michezo nchini lakini hadi ninavyozungumza sasa hivi hakuna hata shule moja iliyoanza kujengwa. Uzuri Waziri wa Fedha mwenyewe ni mdau wa michezo nchini. Je, ni kipi kinaichokwamisha Serikali kutoa fedha ili viwanja wa michezo vianze kuboreshwa?

Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza sahizi, Azam ambaye anafanya production ya mpira kwenye Taifa letu, uwekaji wa taa kama uwanja wa Jamhuri Dodoma zile taa zimewekwa kwa dola laki tatu, zaidi ya milioni 700. Serikali inashindwaje kumuunga mkono kwa kuweka angalau uwanja ambao unaweza kuchezeka mpira? Anapambana kuweka mazingira mazuri ya soka kama mwekezaji lakini sisi kama Serikali bado tumekuwa tukimkwamisha kwenye suala la kuboresha miundombinu.

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara ya Fedha, Wizara ya Michezo inafanya kazi nzuri sana, ipatieni fedha idara hii ili iweze kuboresha viwanja nchini. Watanzania wanapenda michezo, Watanzania wanapenda soka, lakini kumekuwa na changamoto ya kuboresha miundombinu. Leo ninavyozungumza tuna zaidi ya viwanja sita ambavyo vimefungiwa na TFF mpira usiendee kuchezwa kwa sababu ya ubovu wa viwanja hivyo.

Mheshimiwa Spika, na hii imekuwa ikisababisha gharama kwenye timu kuhamia kwenda eneo lingine kuwaleta wachezaji, kusafirisha timu kwa sababu ya ubovu wa viwanja vya michezo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama mdau wa michezo, ona umuhimu wa kuisaidia Wizara ya Michezo ili iweze kuboresha miundombinu ya viwanja vyao. Mlituahidi kwamba tutajenga uwanja Dodoma, na hapa ndiyo Makao Makuu ya nchi na Watanzania wanajua kwamba mlituahidi mtajenga uwanja lakini hadi sahizi Wizara ya Michezo haijaanza kujenga; ukifuatilia hawana fedha ambayo wamepata kutoka Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili, hizi shule saba ambazo mlisema angalau mtaanza nazo hakuna shule hata moja ambayo imeanzwa kujengwa. Kwa hiyo, niishauri Wizara ya Fedha, ni vyema mkatoa fedha angalau kuweza kui-support Wizara ya Michezo ili angalau Watanzania waone mwanga kwenye kuboresha viwanja vyetu nchini.

Mheshimiwa Spika, mimi baada ya kusema hayo, sina mambo mengine ya ziada lakini ilikuwa ni hoja yangu ya msingi, kwamba kilio cha viwanja nchini kimekua ni kukubwa na ni vyema Serikali ikachukua hatua ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais lakini pili kumuunga Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Michezo ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri sana katika kuhamasisha michezo nchini.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ahsante sana. (Makofi)