Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye mawasilisho ya Kamati hizi mbili.

Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na niwapongeze Mawaziri wote wanao-appear kwenye Kamati yetu wanatoa ushirikiano mkubwa na wanapokea ushauri.

Mheshimiwa Spika, mimi nilitaka nishauri jambo la kwanza hapa kuhusiana na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwenye mapato yote ya halmashauri kwa ajili ya kwenda kukopeshwa kwenye makundi ya Vijana, akina mama na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishauri na ninaomba sasa Serikali ikubali kupokea ushauri huu, kuongeza kundi la akina baba. Inatuletea migogoro na sasa hivi imefika mahali wakina baba wanalazimika hata kama hana mpango wa kuoa inabidi aoe ili apate mama ambaye atapata sifa ya kwenda kukopesheka maisha yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matatizo haya ya kijinsia tunayohangaika nayo mengine psychologically yanasababishwa na sisi wakina baba kukosa kitu mfukoni.
Sasa unaona mama ndiye anayetoka anaenda kwenye VICOBA, mama ndiye anayetoka anaenda kukopeshwa, sisi wababa tunabaki ndani tusubiri mama alete. Hili jambo linatuathiri akina baba kisaikolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali ifanye mabadiliko, sheria hii wakina baba waingizwe, makundi yote yaweze kukopeshwa na uzuri mfuko huu umeshakua sana, sasa hivi kwa mwaka zinatolewa zaidi ya shilingi bilioni 68. Kwa hiyo, naomba nianze na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuhusiana na soko la Kariakoo; sheria iliyoanzisha soko hili la Kariakoo ni ya mkoloni, imefanyiwa mabadiliko mwaka 2002, lakini hapa kwenye Kamati tumeshauri soko hili sasa tufanye mabadiliko ili liweze kusimamia masoko yote nchini bila kuathiri mapato ya halmashauri husika. Maana wasiende kusimamia halafu wakachukua na mapato ya halmashauri, hapana wasimamie.

Mheshimiwa Spika, sasa wakati tunapitia kwenye taarifa za utekelezaji wa soko la Kariakoo nilihangaika na wenzangu kutafuta wapi madalali wanaingia kuchangia Serikali, hatukuwaona. Kwenye organization structure hawamo, lakini leo ukienda pale Kariakoo umelima nyanya yako kutoka kule Ng’uni, Mkalama, ukibeba pale Kariakoo kuna watu wananitwa madalali. Hawa watu ndio wanaopanga bei, Wizara ya Kilimo hawawajui, uongozi wa soko wenyewe hawawajui, lakini ndio wenye sauti.

Mheshimiwa Spika, leo tunazungumza Mheshimiwa Rais ametupatia bilioni 958 zimeenda kwenye Wizara ya Kilimo, lengo ni nini? Zikamguse yule mkulima wa chini. Sasa tusipomlinda huyu mkulima wa chini ambaye ndiye mzalishaji anufaike, leo analima kuna mtu anakuja kumpangia afanye nini.

Mheshimiwa Spika, kule kwangu kuna terminology kubwa sana za madalali na lumbesa. Mkulima akishalima, yaani kazi ya mkulima wa nchi hii yeye analima, akishavuna tu sio kazi yake. Kuna mtu pale anaitwa dalali yeye ndiye anayeamua nini kifanyike, kuna mtu anaitwa mchambuzi; kwanza bidhaa yake akishavuna kama ni kitunguu anapokea mchambuzi, anachambua ni cha aina gani? Anampa dalali na moja ya sifa/principle ya dalali ni marufuku mkulima kukutana na mnunuzi, yaani yeye analima anamkabidhi dalali, dalali ndiye apange. Hiki kitu naomba tukitazame vizuri, kinaua uchumi wa wakulima wetu kule chini.

Mheshimiwa Spika, kama tunawapenda hawa madalali basi kuwe na mfumo rasmi wa kuwasimamia, wachangie pato la Taifa, lakini na wao wajue kwamba Nyanya inalimwa shilingi ngapi, kuna process ngapi za kulima nyanya, sio kusubiri nyanya wachukue wao wapange bei.

Mheshimiwa Spika, imefika mbali sana, wakati mwingine mpaka watu wanatoka nje ya nchi wanaingia ndani mwetu, tunapenda kweli kufanya nao biashara, wanakwenda kununua kule kwa mkulima chini kupitia dalali. Jambo hili naomba sana Serikali ichukue hatua za haraka. Jitihada hizi kubwa za Mheshimiwa Rais za kuhakikisha anamkomboa mkulima, kama hatutaangalia mwisho wa kazi anayoifanya, maana hapa tunapanga, peleka mbegu, peleka sijui umwagiliaji, peleka sijui vitu gani mwisho wa siku hatuangalii anaenda kuuzaje. Ninaomba sana Serikali ituangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la lumbesa kule kwangu kuna majina mengi kweli kweli tumepewa, kule kuna aina nyingi; moja inaitwa neti ya kuvuta, hii inabeba ndoo kumi na mbili na anayepanga ni dalali na mchambuzi ndiye anayekwambia weka hapa, mkulima hana shida. Yule dalali anakuja tayari akiwa na risiti ya faini ya lumbesa, ameshalipa Serikali/halmashauri. Kwa hiyo, hakuna mtu wa halmashauri anayemfanya chochote kwa sababu ameshalipa faini.

Mheshimiwa Spika, kuna nyingine inaitwa shishimbi, hii inabeba ndoo kumi na nne na mimi niseme tu Mheshimiwa Mwigulu haya ndio uchumi wetu. Hizi principle zenu za uchumi na theory mnazo, maana jana nilimsikia hapa anasema Wabunge kama hujasoma uchumi sijui usichangie mambo ya uchumi. Uchumi ni haya maisha haya tunayoyazungumza na bahati nzuri Wabunge wote waliopo humu wako makini na wanajua uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kwa tafsiri nyepesi tu ukisoma wakina Smith, wakina nani, wataalamu wa uchumi duniani, wanahitimisha kwamba uchumi ni shughuli zote za binadamu zinazolenga kutekeleza mahitaji yao. Kwa hiyo, humu ndani Waheshimiwa Wabunge wote ni wachumi pamoja na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yaani uchumi tunazungumza nyanya hapa, tunazungumza vitunguu, Mheshimiwa Mwigulu ndio uchumi huu na uchumi ukipanda au ukishuka tunauona kwenye hivi vitu. Nikiona nina kuku wangu wawili wakiongezeka wakiwa watatu ndio uchumi huo kwetu sisi. Sasa hayo ma-principle makubwa nendeni nayo huko duniani mtuletee fedha sisi tunataka hivi vidogo vidogo vya kwetu. Tukilima vitunguu vyetu tupate fedha ndio uchumi. (Makofi)

Kwa hiyo, translation ya uchumi ishushwe ije kwa mwananchi wa kawaida ili tukizungumza uchumi tuelewane sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka nishauri hilo na kuitisha kwa kuomba sana mtusaidie hawa madalali wasiwe na sauti, ikiwezekana mkulima ndiye amwambie dalali fanya hiki na sio dalali amwambie fanya hiki na sifa ya dalali na yeye alime, akiwa analima kama ni dalali wa kitunguu tuone shamba lake, halafu ndio tumpe kazi ya kuwa dalali kwa sababu atakuwa anajua uchungu wa kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze kidogo kuhusiana na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, hii Bodi ni ya muda mrefu na yenyewe, imeanzaishwa tangu mwaka 1953...

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mafuwe, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kenneth Nollo.

T A A R I F A

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe tu taarifa mzungumzaji kuwa hoja ya dalali kwamba lazima awe na shamba, anapokuja tu point yake kutofika mwisho ni kwamba tuimarishe Vyama vyetu vya Ushirika viwe strong ili wananchi wetu wawe na uhakika wa sehemu kwenda kuuza, ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, huyo ni shemeji yangu, kwa hiyo, sina namna ya kuacha kuipokea.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa imeanzishwa mwaka 1953.

SPIKA: Mheshimiwa Mafuwe unapokea taarifa ya Mheshimiwa Kenneth Nollo?

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ninaipokea. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 nakuongezea umalizie kengele ya pili imeshagonga.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri Bodi hii ya Mikopo ya Serikali za Mitaa sheria yake imekuwa ni ya muda mrefu sana, yaani ina sura bado ya kikoloni na bado ina madeni mengi sana. Huu mfuko mpaka sasa hivi una kama bilioni 14.6 lakini una madeni ya bilioni nne na bado ni kama Waheshimiwa Wabunge hapa tukizungumza ni kama haueleweki eleweki hivi.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri kwa kuhitimisha mfuko ufanyiwe reforms ili ufanane na mazingira yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja zote. (Makofi)