Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nikiwa mchangiaji wa kwanza jioni ya leo. Awali ya yote naomba nitamke kwamba Taarifa ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira pamoja na Kamati nyingine ya Kilimo, Ardhi na Maliasili taarifa zote hizo nazikubali na naziunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nichangie upande wa Viwanda, Biashara na Mazingira na nimechagua maeneo hayo kutokana na ukweli kwamba nchi yetu au nchi yoyote ile ili ipate maendeleo ni hakika lazima iwe na uwezo mzuri sana wa kukusanya mapato yake na mapato ya nchi yoyote ile iwe ni upande wa kodi ama mapato ambayo si ya kikodi, lazima yawe yanatokana basi na shughuli ambazo ni za kibiashara, kilimo na viwanda. Sasa hii ndio sababu ambayo inanifanya niweze kuchangia katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nikiangalia mapato ya Serikali katika bajeti yetu hii ya mwaka 2022/2023, utaona kwamba tunakwenda kukusanya, makisio yetu ni trilioni 41.48 na kati ya hizo trilioni 23.65 zinatokana na kodi, hii ni sawa na 57%. Ukiangalia kiwango ambacho sisi tunakusanya na ukijaribu kukipima na pato la Taifa kuna ratio wanaangalia pale na inaonesha kwamba kodi ambazo sisi tuna uwezo wa kukusanya ni 11.7% ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda pengine kwa wenzetu ambao wanatusikiliza, uwiano huu maana yake ni nini? Uwiano huu ni zile fedha ambazo Serikali tunakuwa na uwezo wa kuzikusanya kutoka katika shughuli za kibiashara, fedha zinazozunguka kwa maana ya pato la Taifa na ni kipimo vilevile kuonesha ni jinsi kwa gani Serikali ina uwezo wa kukusanya kutokana na shughuli za kiuchumi. Tunajua kwamba hizo shughuli za kiuchumi tulizozizungumza ni kilimo, viwanda, ajira, biashara na vyote hivi katika asilimia kubwa sana ni shughuli ambazo zinafanywa na private sector.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia uwiano wa nchi nyingine hasa nchi zinazotuzunguka wenzetu wako vizuri, uwiano wa wastani unaotakiwa kukusanya fedha kutoka katika shughuli hizi za kiuchumi zisiwe chini ya 15% ili tuweze kukaa vizuri. Ndio maana unakuta tuna pengo kubwa sana katika bajeti yetu ambayo lazima tukope ama tutafute njia nyingine ya kujazia pale. Sasa kwa kuwa tunafahamu na Serikali yenyewe ilifahamu tangu mwaka 2015/2016 ikaamua kuja na kitu kinachoitwa blue- print kama mwarobaini wa kutuondolea matatizo yanayohusiana na ule ugumu wa kufanya biashara katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya nchi 190, Tanzania ni nchi ya 141. Sasa katika hali kama hiyo tunafanyaje biashara ili kuweza kupata fedha za kutosha na hapa ndipo ninapowaita viongozi wa Wizara hii kwamba kuna haja kubwa sana ya kuwa serious, I am sorry natumia hili neno kuwa serious, asubuhi kulikuwa na discussion ya Liganga na Mchuchuma hapa, contract ambayo imekuwa signed mwaka 2011.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu niambie kuanzia 2011 mpaka leo ni miaka mingapi? Miaka kumi na ushee bado tunaambiwa majadiliano hayajamalizika na hata Kamati, situmii neno imelalamika, lakini Kamati inasema haijaridhishwa na inaitaka Serikali iweze kuendelea na majadiliano kwa uharaka sana. Sasa hili neno ni la kisiasa mno, uharaka mimi kwangu linanipa mashaka, kwa sababu miaka kumi tayari imepita tangu mkataba umesainiwa. Uharaka ni mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ningeiomba Serikali, kwa kuwa kuna fedha nyingi pale katika machimbo haya ya makaa ya mawe, machimbo ya chuma na tunahitaji sana chuma katika shughuli zetu nyingi, ni uchumi mkubwa huo. Sasa leo kama tunaendelea kuambizana kwamba tuharakishe majadiliano hata kama tumeona matatizo. Ukisoma marejeo mengi sana ni kweli kuna matatizo, lakini hatuwezi kuendelea kukaa tukasema kuna matatizo na tukaambiana kwamba tuchepushe majadiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwamba Bunge hili lingeazimia vilevile katika taarifa hii kwamba Serikali ingepewa muda kama kuna uwezekano wa kuwapa muda, hata kama ni ndani ya mwaka mmoja, its ok, lakini ni ndani ya mwaka mmoja tuwe tumelipatia majawabu suala la Liganga na Mchuchuma. Hatuwezi kuendelea kulikalia kimya na tukafikiri kwamba all is well, all is not well kwa sababu hatuwezi tukaacha mali ikae ardhini na tuna watu ambao wangeweza kufanya uwekezaji, si lazima mwekezaji yule, lakini tufikie mahali tufanye maamuzi basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio ya ufanyaji biashara, nimezungumza yanategemea na urahisi na uzuri wa ufanyaji biashara. Nataka nitumie tena neno lingine seriousness ambayo inatakiwa ionyeshwe kwenye Serikali hii ambayo ni sikivu kwamba yawezekana vipi tutunge blue-print sisi wenyewe na Serikali ikaweka mkono wake pale, lakini ishindwe kutekeleza blue-print. Wana sababu gani kwa Serikali kushindwa kutekeleza blue print? Ingekuwa ni document imeandikwa na watu wengine, wakaletewa wao kwa ajili ya implementation, tungeweza kusema kuna mambo mle ndani hayafai, lakini ni mambo ambayo yametengenezwa na Serikali yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba na ningeshauri Bunge hili lije na maazimio kwamba, Bunge linaazimia kuwa Serikali ije na mpango mahususi wa utekelezaji wa blue print katika maeneo ambayo yataondoa ukiritimba uliopo katika regulators, ni ngumu sana kufanya biashara sasa hivi nchini kwetu. Najua kuna dhamira nzuri sana ya Serikali waliionesha kwenye Bunge lililopita karibu sheria 15 zilifanyiwa marekebisho, lakini marekebisho yale si yenye kushika moyo kabisa wa wafanyabiashara, ni marekebisho ya juu juu. Ningependa Serikali ije na kauli kwamba kweli inakwenda kudhamiria na kama ikiwezekana ituletee ripoti ituonyeshe status ya utekelezaji wa blue print imefikiwa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie upande wa umeme. Bila ya umeme, najua kuna juhudi za Serikali, tunakwenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini hali ilivyo sasa hivi kule kwetu Dar es Salaam ni shida. Ni shida kwa sababu sisi hatuna mashamba, sisi hatuna REA, sisi hatuna labda kilimo, pale Kinondoni tunafanya shughuli za vibiashara vidogo vidogo na kushughulika na viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo yana shida ya umeme ya kukatika kila mara, naomba nikutajie, pale Kinondoni mjini penyewe, Hananasifu, Magomeni, Mzimuni, Kigogo, Mwananyamala, Tandale, Kijitonyama, Makumbusho na Kata ya Ndugumbi, ni maeneo ambayo haipiti siku lazima umeme ukatike. Unafanya vipi biashara katika hali kama hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna Wizara inahusika na masuala ya nishati, lakini Serikali yenyewe izungumze. Hapa siku zote tunasema mifumo katika Serikali haizungumzi, mifumo ya kodi izungumze. Sasa kama mifumo yenyewe haizungumzi, kwa nini Serikali haitaki kuzungumza? Izungumze kati ya Wizara na Wizara kwa sababu hakuna Wizara moja inaweza ikasimama peke yake, kila Wizara inamhitaji mwenzake. Kwa hali hiyo tunapozungumzia suala la biashara, tunapozungumza suala la viwanda lazima viende pamoja na masuala ya utoaji wa huduma ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)