Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa fursa hii uliyonipa, naomba nichangie machache kwenye mawasilisho ya Kamati hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba ninaunga mkono hoja zote za Kamati hizi na mapendekezo waliyotoa, kwa hiyo, nawapongeza Wabunge wenzetu wanaotuwakilisha kwenye Kamati hizi na hususan Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati hizi pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao wanaendesha Wizara hizi ambazo zimewakilishwa na Kamati hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwamba tunafahamu wote kwamba nia na lengo la Serikali kuwekeza sana kwenye miundombinu ni kuhamasisha uwekezaji. Lakini ukiangalia utaona kwamba hatujaona miradi yoyote inayoibuka kwa kasi kwenye maeneo yale ambayo miundombinu hususan ya reli na barabara inapowekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo tunasema ni nini? Na nafikiri kwamba hatujaweza kubainisha sawasawa tatizo la uwekezaji nchini linatokana na nini? Ni changamoto zipi? Zinafanya wawekezaji kutoka nje na hapa ndani wasiweze kuchangamkia fursa zinazotolewa na miundombinu mizuri na yenye uhakika na ambayo kusema kweli ni mingi inakamilika na inaonesha kwamba itaongeza tija sana kwa wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tatizo moja ni kwamba kumekuwa na hisia kwamba tatizo kubwa ni mikopo, lakini niwaambie katika soko letu la mitaji, katika financial market yetu, tatizo kubwa ni mitaji ya usawa au mitaji ya ubia (venture capital), hakuna hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nchini Watanzania wachache sana wanaweza wakaanzisha miradi mikubwa. Na ukweli ni kwamba wale tunaowaona wanajiwezaweza kidogo wameanza kidogokidogo wakajidunduliza wakachukua mikopo na ikafika mahali kwamba hata mikopo hawawezi kuongeza kwa sababu lazima mabenki au taasisi za maendeleo zinaangalia uwiano kati ya mtaji na deni, huwezi kupata mkopo zaidi ya mara mbili ya mtaji wako, kwa hiyo inakuwa ni ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme kwamba Serikali kupitia Wizara hii ya Uwekezaji natumaini ingechukua lessons kutoka katika nchi nyingine. Na hata hapa nchini iliwahi kufanyika; chombo pekee cha kuweza ku-intervene katika kuongeza mitaji nchini ni hizi benki za maendeleo. Benki za maendeleo zisijikite kwenye mikopo, zijikite kwenye kusaidia ku-leverage mitaji ya wawekezaji wa ndani, hata wa nje wanaweza wakasaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hakuna nchi ambayo imekuza private sector bila Serikali kujiingiza yenyewe kwa kuingia ubia na sekta hizi binafsi. Kwa sababu kwanza Serikali ikiingiza hata hela kidogo tu ikaingiza kama hisa ikachukua hata asilimia 20 au 10, hata chini ya hiyo, baadaye baada ya mtaji ku-take off wanaweza wakauza zile hisa kwenye soko la hisa au wakauza kwa wale wanaotaka kujiingiza kwenye biashara husika halafu wakachukua zile fedha zikarudi kwenye taasisi zikaenda kuwekezwa kwenye mradi mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo hivyo benki nyingi zinafanya, benki za maendeleo hizi zilitakiwa zifanye kazi hiyo ya kukuza mitaji na kuhamasisha watu waje kuwekeza kwa sababu kuna mtaji ule ambao ni seed utalinda ule mtaji wa yule mwekezaji binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwamba ifanyike jitihada ili sekta binafsi iweze kusiadiwa na Serikali katika kuwaongezea mitaji lakini Serikali ikae kidogo na ijiondoe ili ile fedha iweze kuzunguka kwenye miradi mingine ya harakaharaka naamini hilo ni jambo la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naamini ni la msingi ni kwamba sera ndiyo ni muhimu kwenye uwekezaji na mazingira hayo ya uwekezaji yakijulikana vizuri inasaidia, pamoja na some incentives. Lakini incentive siyo cha muhimu kama hayo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme hivi; tumefanyia sheria yetu ya uwekezaji marekebisho siku za karibuni na imepita. Sasa kama imepita nafikiri taasisi husika zingekuwa mbele kutangaza yale marekebisho yaliyofanywa na faida yake ili watu waweze kujua. Watu hawajui, siyo wengi wanasoma sheria hizi na ninaamini hilo ni la msingi la kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ardhi, kusema kweli mimi nianze kusema kwamba watu wanaosababisha migogoro ya ardhi ni kile kitendo cha Wizara kuwaacha maafisa wake kukaa kwenye mikoa kwa miaka 20 bila kubadilishwa. Wao wanapima ardhi wanaigawa kiajabuajabu, wanaweza ku-double allocate n.k. kwa sababu tu wamekaa miaka mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba Bunge hili lije litoe fedha kwa Wizara husika ili waweze kubadilisha watu, watolewe kwenye mkoa mmoja wapelekwe kwenye mwingine, wale wengine wakija wataibua na watajua chanzo cha migogoro ambayo ipo na wanaweza pengine kuisuluhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kidogo kwenye suala zima la Wizara ya Utalii na Maliasili. Kule kwetu Vunjo, Kata za Mwika Kaskazini, Mamba, Marangu tumeotesha miti mingi lakini tatizo moja tumekaribisha tumbili na gedere wamejaa kule, ndiyo wanawahi kuvuna mahindi yetu kabla hatujavuna, njaa itakayokuja kule kwetu itatokana na tumbili na gedere! Wale wenzetu wanasema wanyama wakali ni pamoja na tembo, lakini sisi ni gedere na tumbili, wanazaliana hawana mpango wa uzazi, wanazaliana hovyo hovyo, wamekuwa wengi sana! Yaani unakuta unapika wanakuja kuingia ndani wanakula chakula. Kwa hiyo, naomba Serikali ijipange kutekeleza mpango wa kuvuna hawa, sijui watawavuna, sijui watawaua! Wakiwa hawawezi watuambie basi sisi tushughulike nao kwa njia zetu. Lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kukubali kwamba tufe njaa huku tunalima usiku na mchana na tunatumia mbolea ya ruzuku! Hapana siyo vizuri, tutafute namna ya kuwaondoa. Pia katika Kata ya Makuyuni ni wengi sana hawa Wanyama ambao ni waharibifu tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie hapo, mwisho kabisa kwenye hili la ardhi, nilisahau kusema kwamba Rais wetu wa Awamu ya Tano, alitoa maagizo kwamba ardhi itolewe kwa miaka 99, lakini nashangaa watu kwenye Mikoa yetu wanatuambia kwamba ardhi ni miaka 33 na wanaendelea kutoa Hati za miaka 33. Nilijua kwamba agizo la Rais ni Sheria pia, kwa hiyo, naomba tuambiwe kuwa kwa nini hii ya Hati Miliki za miaka 33 bado zinatolewa wakati imeshatangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja mara nyingine. Ahsante sana. (Makofi)