Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia katika taarifa hizi mbili za Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wa Ta'ala, kwa kutujalia uzima, afya njema na kuweza kusimama hapa mbele yako leo na kuweza kuchangia taarifa hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja ninapenda kuanza katika Taarifa hii ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa kuomba twende tukaongeze azimio moja la kuzitaka taasisi watekeleze takwa la kisheria la kuanzisha desks za climate change (mabadiliko ya tabianchi) katika kila Wizara. Kwa sababu kuna azimio ambalo la utekelezaji wa mpango kabambe kwa kutoa elimu zaidi, lakini nafikiria itakuwa na tija zaidi tukiliacha hili azimio lakini pia tukaongeza na azimio lingine la kuzitaka taasisi zote zitekeleze hili azimio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo; kwa sababu taasisi zote hapa zimekuwa zikiripoti matatizo ya mabadiliko ya tabianchi kama ni changamoto ambayo inatatiza utekelezaji wa bajeti, utekelezaji wa miradi ya maendeleo, utekelezaji wa shughuli zote za huduma za kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kutekeleza vizuri takwa hili la kisheria ambalo limewekwa katika sheria na sera yetu ya mazingira basi ni vyema tukazitaka sasa kwa sababu hizi sekta zimekwisha kushajihishwa, zimeshapewa elimu lakini sidhani kama kuna angalau desk officer au focal person mmoja katika taasisi zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, Rais, Mheshimiwa Samia, ame-commit hekta milioni 54 katika Mkutano wa Glasgow na Mkutano wa juzi wa Sharm El Sheikh kule Misri, kwamba tunazitenga kwa ajili ya carbonsink Tanzania. Hili ni azimio na vilevile ni commitment ambayo tumeifanya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna huu mpango kabambe, hali kadhalika kuna matakwa mengi ya Kitaifa na kimataifa ambayo tunataka tutekeleze na kuisaidia Tanzania kuweza kuepukana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, ninaomba hili takwa la kisheria tukaliongeza hapa, na tukaliongeza hili azimio katika maazimio ambayo wenzetu wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira wamekuja nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitakwenda moja kwa moja katika sekta ya maliasili na utalii. Mwenzangu amezungumzia kuhusu TANAPA. Na ni kweli, kwamba TANAPA wana jukumu kubwa sana na kama alivyozungumza kwamba tulikuwa tuna hifadhi 16 na hivi sasa zimeongezeka na kuwa 22.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa na hifadhi 16 tulikuwa tuna eneo kama kilometa za mraba 54,000 tu, lakini hivi sasa tuna kilometa za mraba 104,000 wakati eneo la uhifadhi limeongezeka na hizi hifadhi zimeongezeka lakini bado bajeti imebakia ileile tuliokuwa tukiitumia wakati tuna hifadhi 16. Kwa hiyo, ninaomba tu kwamba wenzetu wa Wizara ya Fedha waliangalie hili na ninafikiri sasa ni wakati mwafaka hili azimio la kusaidia, pamoja na bajeti ambayo tunakuwa tunawapa lakini angalau ku-retain, ile retention ya asilimia angalau 20 zibakie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna majukumu ambayo wakati mwingine inakua ni vigumu hizi taasisi zetu kuyatekeleza kama vile majanga ya moto, majanga ya maradhi n.k. kwa kutegemea fedha za bajeti. Mpaka uombe Wizara ya Fedha zije inakuwa ni ngumu. Kwa hiyo, ninaomba tu kwamba tubakishe angalau asilimia 20 za fedha katika ile retention au makusanyo yao wakaweza kutumia kwa masuala mbalimbali, hasa yale ambayo yanakuwa hayana mpangilio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni Hifadhi ya Ngorongoro; tuwapongeze sana wenzetu wa Maliasili, wanafanya kazi nzuri. Lakini pamoja na hayo, Waswahili wana usemi kwamba mchuzi wa mbwa uliwe ukiwa wa moto. Sasa na sisi hili jambo tulifanyie harakati kidogo kwa sababu kama tukichelewa mpaka 2025 inawezekana tukajikuta kuna ugumu kuweza kulitekeleza hili suala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wana bajeti ya karibu bilioni 200 na kidogo ambazo wakizipata hizi wataweza kutekeleza kuhamisha wananchi kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera kwa ukamilifu. Kwa hiyo, ninaomba tu kwamba tujitahidi kuwapatia hizi fedha, na hata ikiwezekana kwa sababu makusanyo ya Ngorongoro kwa mwaka mmoja yanafika milioni 150. Sasa kama tukijitahidi tukiachilia labda fedha zisiende Treasury kwa miaka miwili basi hatutakuwa na haja ya kuchangisha fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niongelee kuhusu Jeshi Usu; Jeshi Usu linafanya kazi kubwa sana. Na hivi karibuni tumekuwa tukisikia kuna vifo vingi vimekuwa vikitokea vya askari wetu hawa wa Jeshi la Uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaomba tu kwamba tujitahidi inavyowezekana kwamba mafao yao hivi sasa yarekebishwe kwa sababu sasa hivi Jeshi la Uhifadhi kutoka TANAPA wana skimu yao, Jeshi la Uhifadhi na WMA wana skimu yao na Jeshi la Uhifadhi la TFS nao wana skimu yao. Kwa hiyo ninaomba tu tukarekebisha utaratibu huu haraka inavyowezekna ili ikiwezekana wawe na utaratibu kama vile wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania, nao watambulike na mafao yawe mazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)