Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Mheshimiwa Spika,nakushukuru sana ili niweze kuhitimisha hoja niliyoitoa asubuhi ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu taarifa ya kipindi cha Mwaka mzima ambao umepita.

Mheshimiwa Spika, pili naomba kuwashukuru Mawaziri tayari hoja nyingi wameshazijibu na hasa naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba Tume ya Mipango amekubali iweze kuanzishwa, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Wabunge wengi wamechangia ambao Wabunge 17 wameweza kuchangia hoja yetu ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji lakini kwa sababu ya muda sio lazima niwataje majina kwa sababu mmewaona.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja kubwa ambazo zimeweza kuongelewa ikiwepo TAFICO kuwa bajeti ziweze kutolewa kwenye Taasisi mbalimbali ikiwemo TAFICO pamoja na taasisi mbalimbali za Wizara yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji ziweze kutolewa fedha.

Mheshimiwa Spika, hoja kutoka kwenye Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri Bashe ameweza kuitolea ufafanuzi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameweza kuitolea ufafanuzi. Lakini hata hivyo bado Kamati tunasisitiza kuwa mtiririko wa fedha uweze kutolewa kwa wakati. Kwa hiyo, Serikali iweze kufuatilia kwa sababu huwa wananchi wanataka kuona mambo yanatendeka kwa hiyo mtiririko ukifuatiwa pamoja na certificate na nini naamini vitaweza kutolewa na ushauri utaweza kutolewa. Bado Kamati inasisitiza hivyo na muuliza swali ambaye ambaye walikuwa wanataka ufahamu bado tunasisitiza hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei nao nashukuru kwa sababu tayari umeshafafanuliwa na Waheshimiwa Mawaziri, lakini tunashauri kuwa Serikali iweze kuungalia vizuri sana kusudi wananchi waweze kupata unafuu kwenye huu mfumuko wa bei ambao unaendelea.

Mheshimiwa Spika, suala la mbolea tayari na lenyewe limefafanuliwa na Mheshimiwa Waziri husika Mheshimiwa Hussein Bashe lakini matatizo bado yapo kwa sababu usambazaji bado ni muhimu nao uweze kuangaliwa kwa sababu ili uweze kupata mazao bora ya Kilimo ambayo Wananchi wamehamasika kweli kulima, lazima uweze kutumia pembejeo bora ikiwepo mbolea pamoja na mbegu. Kwa hiyo, Kamati ilivyoshauri pamoja na Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru. Jambo hili Serikali mlitilie maanani kama Mheshimiwa Waziri ulivyosema kuanzia Mwezi wa Nane kwa safari ijayo mbolea itakuwa imepatikana, naomba ichukuliwe hatua kama ulivyosema.

Mheshimiwa Spika,kwa upande wa malisho, ni kweli Wafugaji wanapata shida wanahama hama kwa sababu ya kutafuta malisho. Kwa hiyo, tunashauri kuwa Serikali iweze kutoa elimu kuhusu malisho na mbegu za malisho ziweze kupatikana madukani kama mambo mengine yanavyopatikana kusudi wananchi hasa wafugaji waweze kupanda malisho na kulinda malisho na hali ya Wafugaji iweze kubadilika.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa sana lingine lililo ongelewa ni mabadiliko ya tabia ya nchi. Mabadiliko ya Tabia ya Nchi kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema, naomba lichukuliwe hatua kwenye uvunaji wa maji, kwenye kulinda vyanzo vya maji. Kwa upande wa Mifugo Serikali iweze kulitilia maanani na kutoa tahadhari ni nini kitatokea kama mambo hayo kusudi kulinda athari ambazo zinaweza kutokea kwa sababu ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine lililotokea ni kuajiri Wafanyakazi wa Sekta hizi tunazo ziwasilisha hasa kwenye taasisi. Ili ufanye kazi vizuri na matokeo ya kazi yaonekane ni lazima ikama ya wafanyakazi iweze kuonekana. Kwa hiyo, vibali viwe vinatolewa viendane na bajeti kusudi wafanyakazi wanaotakiwa waweze kuajiriwa ili kuweza kutoa matokeo mazuri kwenye taasisi na Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu NARCO au Ranch zimeongelewa. Naomba sana kama Wabunge walivyosema isiwepo mabadiliko ya kusema kubadilisha Ranch kupeleka kwenye mambo mengine kama ya kilimo. Kama ni Ranch imepangwa kwa Mifugo iangaliwe jinsi ya kuboresha kusudi tuweze kupata mifugo ya kutosha kwenye Ranch zetu. Vitalu na vyenyewe viweze kutolewa hasa kwa wananchi waliokaribu na hivyo ili waweze kupata vitalu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kilimo cha umwagiliaji sio tegemezi cha mvua na chenyewe kimeongelewa pamoja na scheme ndogondogo ziweze kufanyika Scheme kubwa. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri ameweza kufafanua kuwa Fedha za umwagiliaji zipo na ninaamini kuwa Scheme nyingi zimeanzishwa ziweze kuangaliwa kwa umakini kusudi tuweze kuona kuwa Kilimo cha Umwagiliaji kinafanya kazi na hata kwenye Vituo vya mbegu tuweze kuzalisha mbegu kwa wingi kusudi tuweze kujitegemea. Kwani mpaka sasa hivi kama Wabunge walivyosema na Kamati imeona hivyo hivyo kuwa ni asilimia zaidi ya 60 mpaka sasa hivi ambayo Tanzania hatujitegemei tunapata hizi mbegu kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine lililoongelewa sana ni Uvuvi haramu, naomba Wizara husika iliangalie ili kukomesha Uvuvi haramu.Tukiendelea na Uvuvi haramu hatuwezi kupata Samaki na sisi Samaki ni lishe, Samaki ni kitoweo na Samaki ni fedha. Kwa hiyo, hilo nalo kama Wabunge walivyosema Wizara inayohusika naomba litilie maanani pamoja na matumizi ya Timba na Makokoro na Taa za Solar nazo zimeongelewa kwa wingi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine lililosemwa ni mbegu. Je tunaweza tukapata mbegu za mazao mwaka ujao? Mheshimiwa Waziri amelifafanua sina tatizo ya kulisemea kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine lililoongelewa kwa wingi ni pongezi. Tumetoa pongezi, Kamati imetoa, Waheshimiwa Wabunge wametoa pongezi kwa DAWASA pamoja na Wizara ya Maji jinsi walivyokabiliana na tatizo la maji kule Dar Es Salaam. Kwa hiyo, nazidi kuwapongeza kuwa pongezi hizi zifike na muendelee kufanya hivyohivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine lililoongelewa ni Sekta ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi vituo atamizi kwa ajira ya vijana. Mheshimiwa Waziri ameweza kufafanua kuwa vipo vituo ambavyo vijana wanabidi waweze kuajiriwa na wenyewe Wizara ya Kilimo watume applications kusudi waweze kuajiriwa.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni mazao ya bustani nayo yameongelewa, lakini haya mazao ya bustani yanaendana na usafirishaji ambao bado ni tatizo kwa hiyo, tumeshauri na Wabunge wameshauri kuwa Bandari na Viwanja vya Ndege viweze kuwa na green belt maana yake ni nini viwepo vitu vya kupoozea mazao kama haya ya bustani pamoja na uchakataji ambao utakuwa hapo karibu karibu na miundombinu ya usafirishaji iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, naamini na Serikali imelichukua na ninashauri kuwa Serikali imeji-commit hapa hapa Wizara zote tatu zimesema kuwa ushauri wa Kamati wameuchukua na wataufanyia kazi. Jambo muhimu sana ni kulinda vyanzo vya maji ambavyo tayari Wabunge wamesema sana na Kamati imesema kusudi kutokana na matatizo ya ukosefu wa maji na kuharibu na mambo ya mabadiliko ya tabia ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mtiririko wa fedha tayari nimeshaongelea, tafadhari tunaomba sana hazina pamoja na Wizara mkiwaambia watu kuwa fedha zipo hawaelewi kwa hiyo, tunaomba mkazo uweze kuangaliwa kusudi hatua inayokwenda na hatua inayofuatiwa iweze kufuatiwa kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, Utambuzi wa Mifugo; lilisitishwa jambo hili la utambuzi wa mifugo lakini limejitokeza humu Bungeni na kwenye Kamati kuwa ili tuweze kujua mifugo ni kiasi gani na idadi gani na mifugo hii ni ya nani, jambo la heleni liweze kuangaliwa tena kusudi tuweze kutambua mifugo tuliyonayo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naweza kugusia ni kuhusu Ushirikiano wa Kiwizara hasa kwenye mambo mnayofanya kwa pamoja. Tumeongelea kuhusu ujenzi wa Mabwawa nalo limechukuliwa naamini Mheshimiwa Waziri Ndaki ametolea ufafanuzi kuwa walishakaa na tunaomba litendeke sio kila Wizara inajifanyia kuona uhai kusudi tuweze kuwa na uhai.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni Sera ambalo na lenyewe limefafanuliwa hapa. Sera ya ushirika Mheshimiwa Simbachawene amelifafanua vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ulilotaka kujua ni udumavu wa Samaki wa Mtera na uzuri wake kuwa na sisi tunaokula Samaki hao, tunaweza kuwa wadumavu? Kama umeshapitia stage ya udumavu ni kitu kingine lakini kama kuna chemicals nayo ni kitu kingine kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri amesema atalifanyia kazi na tayari amesha wa-assign watu wa TAFICO kulifanyia kazi na utafiti. Tunaomba sana lifanyiwe utafiti haraka sana.

Mheshimiwa Spika, mambo hayo mengi ndio yaliyojitokeza na ninashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuchangia vizuri hoja yetu ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Kwa hiyo, nawashukuru sana na wengi wameunga mikono, nasema ahsante, nahitimisha hoja hii nikisema kuwa natoa hoja na ninaomba Bunge zima liweze kuunga hoja hii kusudi iweze kupita. Ahsante sana nawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naafiki.