Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi kuniruhusu nichangie hii hoja yetu ya Taarifa ya Mwaka ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na Wizara ya Maji. Kamati yangu ilitembelea miradi mbalimbali inayofanywa na Wizara ya Maji, lakini pia Kamati yangu ilitembelea miradi mikubwa ya DAWASA huko Kimbiji, Dar es Salaam; mradi wa maji kule Mlandizi, lakini pia tulitembelea miradi mingine kule Mwanza, Butimba na kule Musoma, Kiabakari ya Bugingo na Butiama.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa miradi mikubwa hii iliyolenga kauli ya mama Samia Suluhu Hassan ya kumtoa mama ndoo kichwani. Na Serikali imetoa hela nyingi sana na miradi hii inakwenda vizuri. Mpaka tulipokuwa tumetembelea miradi hii ya maji ilikua imepata asilimia 70 hela za ndani na asilimia 81 hela za nje. Serikali imetekeleza miradi hii mikubwa ya Mwanza na Musoma.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ule mradi wa miji 28 katika nchi nzima kama ambavyo tumeisikia huko nyuma, lakini tumeona kwamba miradi hii imekwenda na upanuzi wa mradi ule wa Ziwa Victoria. Katika Jimbo langu kwa mfano, nitapata vijiji 58 na kwa kweli mradi unakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, tulipata tatizo dogo, mkandarasi mmoja hayupo site licha ya kupewa site miezi minne iliyopita, hapo ndipo ninaomba nipate maelezo kwa nini. Lakini miradi mingine jimboni kwangu inakwenda vizuri na ninaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu mifugo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Kamati yangu ilitembelea miradi kadhaa na miradi hiyo, kwanza niipongeze Serikali kwa kuanza mradi ule mkubwa wa bandari ya uvuvi kule Lindi. Lakini tuliona bandari ile badala ya kuwa bandari peke yake ambako meli zitakuwa zinashushiwa samaki, Serikali ifanye mpango wa kubuni industrial park pale ili samaki watakaoletwa na meli zile za uvuvi wachakatwe palepale na kutoa mazao ya samaki badala ya kuwasafirisha samaki waende wapi. Kwa sababu Bandari ya Dar es Salaam haina eneo la kuweka samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala hilo tumeona kwamba Serikali haikuwa na uwazi viwanda gani vitakuwa pale. Na tungependa meli zote zipeleke samaki pale watoke pale kama mazao ya samaki.

Mheshimiwa Spika, liko suala la mpango mzima wa kutumia fursa ya uchumi wa blue. Sisi tulikuwa tumejipanga huko nyuma – bajeti ya mwaka jana – kununua meli za uvuvi na kufufua ile Kampuni yetu ya TAFICO. Lakini hela inayopelekwa kule tumeona ni ndogo sana, haiwezi kulifufua Shirika la TAFICO likarudi kama lilivyokuwa zamani. Kamati yangu inaishauri Serikali iweke hela za kutosha kuifufua TAFICO ili tuweze kufaidi fursa hizi za uvuvi na uchumi wa blue.

Mheshimiwa Spika, liko pia suala la kufufua, nimesema kwa kifupi TAFICO, lakini tulipotembelea pale TAFICO hali haikuwa nzuri sana, niseme tu ukweli. Na hata juzi nilijitembeza mwenyewe pale, bado hali iko vilevile. Kwa hiyo ninaomba Serikali yetu iupe nguvu mradi huu wa kufufua TAFICO, utakuwa na faida kubwa sana kuliko hali ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie sasa suala la kilimo. Kilimo mwaka huu kwenye bajeti hii na Serikali ya Awamu ya Sita inahitaji kuchezewa ngoma tukafurahia. Kilimo, Waziri, Mheshimiwa Hussein Bashe, amevaa viatu vya kilimo, na kama anavyotaka mama Samia Suluhu Hassan, wanafanya mambo makubwa mapya, wana maingizo mapya kwa mfano kilimo cha block farms, kilimo kile cha mashamba makubwa ambayo yataajiri vijana wengi sana. Lakini pia Wizara hii imejikitika katika kupatisha mbegu wakulima na kuongeza bajeti mpaka tukapata ruzuku ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri Serikali ijenge viwanda vyake vya mbolea ili kuondoa matatizo ya utegemezi wa mbolea kutoka nje ambayo kwanza inachelewa kuja na inakosana na vipindi au ratiba ya kilimo. Kwa kuwa na viwanda hapa kwetu tutakuwa na faida kubwa sana. Tumeshuhudia kiwanda kimoja kimejengwa hapa lakini hakitoshelezi kupeleka mbolea nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana mama Samia Suluhu Hassan kwa kuona lengo la kilimo kwa maono mapya, kwa matoleo mapya, na matokeo yake kilimo kimekuwa cha kibiashara na kimevutia vijana wengi kwenda kuchangia kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo mipango mizuri kabisa ya kupata mbegu kutoka kwenye Shirika letu la ASA, lakini pia tafiti mbalimbali zinaendelea katika mashirika yetu. Tatizo ni hela kuchelewa kwenda au kutokwenda kabisa. Tunashauri Serikali ipeleke hela hizo ambazo sisi tumeziomba kwa ajili ya kuleta mafanikio ya kilimo cha kisasa na kuleta uwezekano wa kuongeza tija zaidi na zaidi kwa kuwa na mbolea itakayopatikana hapa kwetu.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kuchangia hayo; ahsante sana. (Makofi)