Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu na wataalam wake wote na mawaziri wote na viongozi wote ambao wako katika Wizara hii ambayo imekuwa ikiendelea kufanya kazi pamoja na Waziri Mkuu. Na niseme tu tunafarijika na namna wanavyokuwa wakiendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kutoa hoja ambayo nimedhamiria sana kuna mambo ambayo nilitamani niyabainishe, ambayo ningetamani Ofisi hii ya Waziri Mkuu waweze kuona na kuyapa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu masuala ya utekelezaji wa miradi. Kumekuwa na uibuaji wa miradi mingi ambayo imekuwa ikiendelea kutelezeka, lakini mingi unakuta miradi imedolola na imekaa muda mrefu bila kumalizika. Nitatoa mfano wa mradi mmoja ambao tulipitia, Mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbalali ambao ulianza tangu 2011 na mpaka leo haujaisha. Nilitamani Ofisi ya Waziri Mkuu wawe na mkakati wa kuwa na timeframe kwa kila mradi unaoanzishwa, kwamba ndani ya muda fulani mradi huu unakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu kingine ambacho nimekiona na ningetamani kukichangia hapa ni katika masuala ya ardhi. Kumekuwa na tabia ya watu kubadilisha matumizi ya ardhi bila utaratibu, na unakuta Serikali inapoteza mapato mengi katika maeneo haya. Unakuta mtu aliomba kibali cha kupata eneo kama makazi badaye anakwenda kufanya biashara na wakati huo huo yeye anakuwa anaingiza pesa nyingi Serikali aipati chochote. Kwa hiyo, nilitamani pia Ofisi ya Waziri Mkuu iliangalie hili pia na kufanyia mkakati maalumu, badala ya kuendelea kutenga maeneo na kupima mapya kila siku na kugawa kuwe na uhakiki wa maeneo yalishatolewa na sisi kama taifa tuweze kunufaika kwa ubadilishaji wa maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu maeneo mengi ya miji yamechangamka lakini ukienda kuhakiki unaweza ukakuta either pale mjini hawana hati na yale maeneo hayajapimwa; lakini unakuta wao wanaendelea kufaidika na Serikali haipati kitu chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nilitamani kuongelea ni suala la TAZARA. Tunafahamu upo ukakasi katika suala la TAZARA, lakini tufahamu kabisa TAZARA ni uchumi wa Nyanda za Juu Kusini. Watusaidie hiyo sheria ambayo haifanyiwi marekebisho kwa kushirikiana na wenzetu wa upande wa Zambia walichukuwe kwa haraka. Katika hotuba hii sijaona kitu chochote kinachozungumziwa kuhusu TAZARA. TAZARA ni muhimu, TAZARA bado iko vizuri, lakini inachakaa na miundombinu inachakaa kwa sababu tu hakuna uangalizi mzuri kutokana na hiyo sheria wanayosema ina ukakasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nirudi kwenye hoja halisi ambayo nilitamani kuizungumzia leo. Tunafahamu kabisa nchini hapa kuna janga la madawa ya kulevya. Tunapoongelea madawa ya kulevya mimi awali nilikuwa naona ni kitu cha kawaida sana; lakini kuna siku wabobezi wenyewe wa masuala ya madawa ya kulevya walinifafanulia, na hivyo niliona ipo haja kama taifa kuingia kwenye mapambano dhabiti ya kuahakikisha madawa ya kulevya kwetu inakuwa ni kitu cha kusimuliwa, kwamba yasiwepo kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea madawa ya kulevya unaongelea kuhusu nguvu kazi ya taifa ambapo vijana wengi wanaharibika na wanakuwa hawawezi kufanya kazi yoyote ya kulijenga taifa kwa kujipatia kipato chao wenyewe. Lakini pia tunaliongelea maadili ya taifa. Tunafahamu vijana wengi wanaotumia madawa ya kulevya ni watu ambao hawajali lolote na maadiliyao yanakuwa mabovu, wanakuwa vibaka, wengine ndiyo wanajiuza wengine unakuta ndio hao wanaoingia kwenye vitendo vya ushoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa upande wa Serikali tunakuwa tunapoteza pesa nyingi kwa kununua hizi dawa, na taifa linapoteza fedha kwa biashara hii haramu. Sasa, kiuchumi hili linasababisha tunaendelea kushuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema nini; tunajua kabisa program mbalimbali za dawa za kulevya zimekuwa zikiendelea chini ya Kamishna Jenerali wetu Kusaya na wataalamu wake. Hata hivyo, bado ziko changamoto za msingi ambazo kama taifa tunatakiwa tuwape support Ofisi ya Mamlaka Dawa za Kulevya ili iweze kufanya kazi vizuri. Tunafahamu kabisa pesa inayotolewa ni ndogo, lakini pia kuna kitu ambacho kimesahaulika. Wanabainika watu wa dawa za kulevya lakini hakuna linkage na TAMISEMI ambao ndiyo iliyo karibu sana na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninataka kusema nini, kuna kundi la watu wa ustawi wa jamii ambao ndio wanao-deal na watu wote wenye changamoto za kijamii ikiwa ni pamoja na hawa wa dawa za kulevya. Kule chini hatuna watu ambao wanasimamia. Yaani katika TAMISEMI ukienda kufuata structure ile huwezi ukamkuta mtu ambaye yuko maalum kwa ajili ya kusimamia masuala ya kulevya katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii sasa inavyokuwa hapa unaona kwamba, mamlaka inapambana kwa namna yake lakini TAMISEMI yenye watu haina habari na hiki kitu. Kwa hiyo niseme tu mimi kwamba, ofisi hii ya mamlaka itengenezewe utaratibu wa kuwa linked na TAMISEMI ili waweze kuwahudumia na kuwabaini hawa watu kwa wepesi kuanzia kwenye ngazi za vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kutoa hizo pesa kwa ajili ya upambanaji wa uingizaji na matumizi na kupunguza madhara ya dawa za kulevya kuna kitu ambacho kimesahaulika. Kwamba, tukumbuke wale watu wanaotumia dawa za kulevya jamii imeshawatenga; ni watu wasiokubalika katika jamii. tunafanya nini kama Serikali kuwaaminisha hawa watu tumewatibu katika vituo vyetu vya matibabu ya dawa za kulevya ili waweze kurudi kwenye jamii na kupokelewa na kuweza kushiriki katika shughuli za maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme, kwamba ipo haja kupitia Ofisi ya Kamishna kutenga fungu maalum la fedha ambalo litasaidia katika kuwajengea uwezo au kuwapa mitaji hawa vijana. Na itengenezeke sera ambayo itaonesha kwamba hawa vijana, sasa baada ya kuacha madawa ya kulevya waingine katika utendaji kazi, hata wakawa wanarudishwa mmoja mmoja kwenye ofisi, kwa wale ambao wamesoma. Hii itasaidia kuepukana na changamoto hii. La sivyo tutakuwa tunawatibu lakini wanaendelea kurudi kwenye matumizi ya dawa kwa sababu watakuwa wanakosa support ya kijamii, kiserikali katika kuacha kabisa haya masuala ya dawa za kulevya. Tutakuwa tunafanya kazi ya kuwatibu, wanarudia, kitu ambacho siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.