Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia na mimi nisimame ili kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Wabunge wenzangu waliompongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi njema, kazi iliyotukuka pamoja na Serikali yake yote kwa ujumla, hakika Mwenyezi Mungu anaiona kazi iliyo njema ataendelea kuibariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hususani ukurasa wa 28 ambao unaongolea kilimo. Baada ya kuchagua eneo hilo, nimepitia eneo hilo ninakuta Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu wametaja mazao ya mafuta ikiwepo alizeti pamoja na michikichi, lakini kwa bahati mbaya sana nilitarajia na zao la soya lingekuwa miongoni mwa mazao ambayo Serikali inatambua na kujua kwamba tunatakiwa kupata mafuta kutoka katika zao hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikafanya study nikapitia taasisi moja inayoitwa the International Institute of Tropical Agriculture kutaka kujua zao hili la soya likoje. Nimegundua yafuatayo; katika Afrika nchi ambayo inazalisha zao hili kwa wingi ni Nigeria, kama ambavyo Mheshimiwa Anna Kilango Malecela aligundua kwamba Nigeria pia wanazalisha zao la Tangawizi kwa wingi, hali kadhalika kwenye soya wapo. Lakini study inaonesha kwamba baada ya Nigeria wanakuja Afrika ya Kusini wanafuata Zambia pamoja na Malawi, Tanzania hatumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze kazi njema sana ambayo imefanywa na balozi wetu aliyepo nchini China Mheshimiwa Balozi Kairuki kwa kusaini mkataba kati ya Tanzania na China kuweza kuuza zao hili ambalo ni zao jema sana kwa uchumi wa taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikafanya utafiti nini faida inayotokana na zao hili. Yafuatayo nimeyabaini; katika zao hili unaambiwa kwamba asilimia 36 ya protini inapatikana kutoka katika zao la soya lakini asilimia 30 tunapata carbohydrate lakini pia wanasema excellent amount of dietary fiber vitamin and mineral. Pia ina- consist twenty percent ya oil, kwa maana ya mafuta ya kula na hivyo wana-recommend kwamba ni kati ya mazao ambayo yanatakiwa yapigiwe mfano kwa nguvu zote sisi Waafrika kuhakikisha kwamba tunalima ili tuondokane na tatizo kubwa la mafuta. (Mafuta)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi, zao hili wanasema baada ya kukamua mafuta ile keki yake ambayo inabaki ni chakula kizuri sana kwa ajili ya mifugo, na ninaamini katika mpango mzima wa Serikali wa kuanza kufuga kisasa tutatumia zao hili katika kufuga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini soya bean is the only available crop that provides inexpensive and high-quality source of protein comparable to meet poultry and eggs; lakini kama haitoshi wanasema garama yake ni ndogo ukilinganisha na mazao ya nyama pamoja na mayai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba ukilima soya ina uwezo wa kunyonya nitrogen kutoka hewani na kurutubisha ardhi. Kwa hiyo, kwa ajili ya matumizi sahihi ya ardhi yetu ambayo imechoka ni vizuri sasa kama Serikali tukahakikisha kwamba tuna encourage kilimo hiki kwani pale ambapo tunahitaji mbolea za viwandani tukishalima soya hatutakuwa na haja ya kutumia mbolea za viwandani ambazo sisi sote ni mashuhuda jinsi ambavyo mbolea hii imekuwa ikipatikana kwa bei kubwa na wakati mwingine hata upatikanaji wake unakuwa si wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo na kwa utafiti ambao nimefanya na kwa kulima mimi mwenyewe niitake Serikali, this is high time ya kuhakikisha kwamba mikoa ile ambayo inahangaika na kilimo cha mazao ya jamii ya mikunde ikiwepo Manyara ambao wamekuwa wakilima mbaazi wanakosa kwa kupeleka, ni wakati muafaka sasa twende kulima soya. Kama haitoshi, wakoloni walitaka reli iende Nachingwea kwa sababu ilionekana ndiyo sehemu ambayo soya inakubali mawazo mazuri haya it's high time kama Serikali tuhakikishe kwamba tunalima kilimo hiki kwa sababu soko la uhakika lipo lisilotiliwa mashaka hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu miongoni mwa mikoa maskini ni pamoja na Mkoa wa Rukwa, ni matumaini yangu makubwa kwamba Serikali itaielekeza nguvu yake kubwa katika kilimo cha soya ili wananchi ambao wamekuwa wakilima mahindi kwa kiasi kikubwa lakini wanaendelea kuwa kwenye lindi la umaskini wanatoka kwenye umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya uwepo wa protein, ni jambo la kusikitisha sana ukiambiwa kwamba akina mama na watoto ambao wanakufa kwa sababu ya kukosekana na virutubisho ikiwemo protein wanapatikana katika Mkoa wa Rukwa. Naamini, haya matatizo ambayo yanapatikana ndani ya Mkoa wa Rukwa na kwingine katika Tanzania hali ipo hivyo hivyo. Ni matumaini yangu makubwa sana kwamba Serikali itaenda kufanyia kazi kubwa ili tuhakikishe zao hili linaenda kufanya mapinduzi katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikielekea kuhitimisha naomba niulize Serikari maswali yafuatayo na wanijibu. La kwanza, kwa nini Mkoa wa Rukwa pamoja na kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula ikiwepo mahindi lakini imekuwa ni mkoa maskini kuliko mikoa yote Tanzania? Swali la pili, kwanini vifo vya mama na mtoto ndani ya Mkoa wa Rukwa vimekuwa vingi ukilinganisha na mikoa mingine? Swali la tatu, kwa nini katika mradi wa Agro- connect ambao unaitaja Mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Songwe na Katavi imeruka Mkoa wa Rukwa? Swali la nne, kwa nini mpango wa kuunganisha Mkoa wa Rukwa na grid ya taifa, ilikuwa ikisemwa zamani, sasa hivi hatujui mpango huu umeishia wapi? Swali la tano, kwa nini Mkoa wa Rukwa umekuwa ukifanya vibaya katika ufaulu wa watoto wanaomaliza darasa la saba kwenda kidato cha kwanza? Kwa nini Mkoa wa Rukwa umekuwa na upugufu mkubwa sana wa watumishi ukilinganisha na mikoa yote Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja naomba Serikali inijie na majibu ya maswali yangu yote. (Makofi)