Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Lakini kabla sijachangia na mimi naomba kushiriki kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri sana ambayo amenza kuifanya tangu alipoingia madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa Mpwapwa, kama unavyojua Mpwapwa ina majimbo mawili, tumepata madarasa mengi, madarasa takriban 103. Madarasa 20 ya shule za msingi na madarasa 83 shule za sekondari, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea, kwa hiyo tunamshukuru sana. Lakini pia kwa ujumla wetu kwenye haya majimbo mawili, ya Kibakwe na Mpwapwa, tumepata vituo vya afya vitatu, shule za sekondari zinazojengwa na nguvu ya Serikali ni tatu, na pia barabara zote za vijijini zimefunguka. Napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kufanya kazi hii nzuri. Naamini majimbo yote yamenufaika na fedha hii ambayo Mama Mheshimiwa Rais wetu ametoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimshukru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ajili ya uongozi wake mzuri sana hapa Bungeni. Mtu mnyenyekevu, ambaye ameongoza Bunge hili kwa kipindi kirefu akisimamia mambo ya Serikali katika Bunge hili, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa nianze kuchangia mambo matatu. Kwanza naomba nizungumzie habari ya barabara. Sera ya Serikali ni kuunganisha miji yote ya mikoa na wilaya kwa barabara za lami, lakini bahati mbaya sana katika Jimbo letu la Mpwapwa na Kibakwe sisi barabara haijaunganishwa kwa lami. Tuna kipande kinachotoka njia panda ya Kongwa kuelekea Mpwapwa Mjini, lakini pia kutoka Mpwapwa Mjini mpaka Chipogolo. Barabara hiyo ni kati ya ahadi za Mheshimiwa Rais Marehemu Magufuli, aliahidi kwamba ingejengwa katika kiwango la lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mpwapwa ni mji mkongwe lakini umedumaa sana kimaendeleo kwasababu ya tatizo la barabara hii. Hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuthubutu kuja kuwekeza Mpwapwa kwasababu ya barabara mbaya. Na kutokuwa na wawekezaji wa kutosha katika mji wa Mpwapwa kiuchumi hatuwezi kukua. Kama mnavyojua uwekezaji ndio unazalisha ajira nyingi sana kwa vijana wetu, kwa hiyo suala la ajira kwa vijana wa Mpwapwa, kama ile barabara haitawekwa lami, itabaki kuwa historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana barabara hii Serikali mwaka huu wa fedha 2022/2023 basi tukumbuke, kutokee muujiza tupate barabara ya lami. Waheshimiwa Wabunge walionitangulia wote wamepiga kelele; tangu uhuru kipande hiki hakijawekwa lami, ni kama kilometa 40. Kwahiyo wananchi wa Mpwapwa wanaendelea kuteseka na hali ngumu ya uchumi kwasababu hawana interaction na watu. Ukiwa hauna barabara watu hawawezi kufika kwako.hata katika maisha ya kawaida nyumbani kwako kama hakuna njia safi ya watu kupita kuja kukusalimia hawatafika, kwa hiyo hautakuwa na interaction na watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo ningependa kuzungumza ni madaraja. Pale Mpwapwa tuna madaraja matatu ambayo yana umuhimu mkubwa sana, yote yanaunganisha majimbo yote mawili. Kuna daraja la Godegode, daraja la Gulwe na Daraja moja la TANESCO, lipo mjini. Mheshimiwa Waziri Simbachawene anashindwa kwenda kule kwenye Jimbo lake kwasababu madaraja yote yamevunjika. Ukipita njia hii ya Godegode daraja limevunjika, ukipita njia hii ya Gulwe daraja limevunjika. Sasa utasikia watu wanamtafuta hawamuoni, lakini atapita wapi? Kwa hiyo ninaomba sana madaraja haya pia yaangaliwe kwa karibu sana (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine nizungumzie sekta ya kilimo. Wengi tumezungumza; katika Wilaya ya Mpwapwa wilaya nzima ina maeneo mengi mazuri sana kwa ajili ya Kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano Kata za Chunyu, Mlembule, Lumuma, Mbuga pamoja na Nduga ni maeneo ambayo yana maji; lakini shida tunayoipata kule hata kilimo kile kinachofanywa na wakulima wetu pale hakina tija kwasababu hakuna miundombinu. Mimi ningeshauri Serikali; kwamba tukitaka ku-emphasize kilimo lazima tuangalie sana kilimo cha umwagiliaji, kilimo ambacho hakitegemei mvua za msimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka huu mvua hapa Dodoma haijamalizia, kwa hiyo mazao mengi yanakauka sasa. Lakini tungekuwa tunamwagilia maana yake tungekuwa na uhakika wa chakula. Kwa hiyo ninaomba sana Serikali iwatengenezee hawa watu miundombinu barabara zimefunguka lakini wakipata Kilimo wakalima kwa mfano kule tulilima vitunguu sana, vitunguu vile vinaweza kusafirishwa kutoka kwenye maeneo yao kwenda kwenye masoko, kwenda Dar es salaam ama kuja Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sasa hivi wanalima kidogo sana. Tumesema ajira kubwa katika nchi hii inapatokana kutokana na kilimo, asilimia 65 ya ajira inapatikana kutokana na kilimo, lakini je, ni asilimia ngapi ya hizi ajira? Hawa watu walioajiriwa na kilimo ni asilimia ngapi wanapata tija halisi inayotakiwa na Kilimo? Utakuta asilimia kubwa ni watu wanaolima kilimo cha kujikimu tu, hawapati mazao yanayotakiwa kwasababu ya ukweli kwamba miundombinu ya umwagiliaji haipo; na mimi ningependa sana Wizara ya Kilimo ijikite sana kwenye miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la mazingira pale Mpwapwa Mjini. Mji wa Mpwapwa umepitiwa na korongo kubwa sana. Lile korongo limeleta athari nyingi kwa miaka mingi sasa. Maisha ya watu yamepotea na nyumba zimechukuliwa. Hata mwaka huu nilimletea picha za athari zilizotokea Mheshimiwa Waziri wa Mazingira. Tunaomba sana Serikali iangalie namna ya kutatua hilo tatizo la mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naona kengele ya pili imegongwa naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)