Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia katika Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, nampongeza pia Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mjadala mkubwa kuhusu kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali ambao pia Mheshimiwa Waziri Mkuu amejielekeza kwenye ukurasa wa 16. Ningependa kwanza niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri, Waziri wa Fedha na Waziri wa Viwanda na Biashara na Uwekezaji kwa taarifa waliyotoa jana, ufafanuzi mzuri na nishauri taarifa ile tungepewa Wabunge wote lakini pia ingewasilishwa kwenye mamlaka mbalimbali za Kiserikali. Kwa sababu imeanisha hatua mbalimbali za muda mfupi, muda mrefu na muda wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matumaini ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametupa namna gani ya kulekea bajeti ya 2022/2023 Serikali itafanya nini katika kushusha bei za bidhaa mbalimbali. Kwenye bidhaa ya mafuta ninaomba nitoe ushauri kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliona jitihada za Mheshimiwa Rais Mwezi wa Oktoba, tarehe 05 alifuta zile tozo za taasisi na kiasi cha Shilingi Bilioni 102 ziliondolewa lakini unafuu haukupatikana. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali kwa mwenendo waliyoonesha kwenye bei hii ya mafuta kabla ya UVIKO, wakati wa UVIKO na baada ya vita hii inaonesha bei inaendelea kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itakapokuja kwenye Bajeti Kuu iangalie utaratibu wa kutoa subsidy kwenye bidhaa hii ya mafuta, kama zilivyofanya nchi za jirani Afrika Mashariki. Ifanye tathmini na tafiti, tambua hatulingani kwa hali zetu za kiuchumi lakini pengine inaweza ikaendelea kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pamoja na hatua zingine ambazo zitachukuliwa, ninakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha maoni mbalimbali ya wadau wa sekta binafsi uyatilie maanani ili kusaidia kupungua kwa bei hizi kwa sababu kweli hali ni tete katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili pia utajielekeza, jana kuna maoni yalitolewa hapa kwamba Taifa letu hili halina maono na Marais wetu kila mmoja akiingia anafanya kwa kadri anavyoona yeye inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwamba Taifa letu hili maono yake yanatokana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 na dira hii iliandaliwa mwaka 2000 na utekelezaji wa Dira hii wa Maendeleo ya Taifa ulipangiwa mkakati wa miaka 15, kila baada ya miaka mitano unaandaliwa mpango wa Maendeleo ya Kitaifa ambapo kwa Ilani zetu za Chama cha Mapinduzi, chama ambacho kiko madarakani inatohoa Ilani zake kupitia mipango mbalimbali kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo moja ya kipaumbele kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ilikuwa ni kuwepo kwa jamii inayoelimika. Kwa hiyo nataka nitoe mfano hapa, kwa kipindi cha Rais Marehemu Benjamin Mkapa aliboresha elimu, kwa elimu ya msingi na sekondari kupitia MEM na MES. Kipindi cha Rais wa Awamu ya Nne ujenzi wa shule za sekondari kila Kata ni maono, kipindi cha Rais wa Awamu ya Tano kutoa elimu bure ni maono, kipindi cha Rais wa Awamu ya Sita kuwezesha kupatikana kwa madarasa zaidi ya 15,000 na miundombinu mbalimbali, ujenzi wa Maabara nayo ni maono ambayo yameanza kutolewa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba haitoshi ujenzi wa SGR wazo au mikakati ilianza tangu Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne, Awamu ya Tano utekelezaji wake ulianza na Awamu ya Sita hii Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan anaendelea kutekeleza nayo ni maono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, wazo lilianza tangu wakati wa Mwalimu Nyerere, hata Awamu ya Nne pia ilikuja na mkakati ndiyo maana mwaka 2012 Rubada iliingia mkataba na Kampuni ya ODRICH ya Brazil, hatimae Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Hayati Daktari John Pombe Magufuli mradi huu ulitekelezwa na sasa hizi chini ya Uongozi wa Rais Samia mradi huu unaendelea kutekelezwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiangalia ujenzi wa miundombinu mingine, kwa mfano mwendokasi Dar es Salaam ni utekelezaji wa Awamu mbalimbali. Kwa hiyo, kuliaminisha Taifa kwamba hatukuwa na mpango wowote au hatuna maono mimi nadhani siyo sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umefika wakati pengine kama Taifa kutazama sasa kama ushauri ulivyotolewa maono ya baada ya miaka 50 na miaka 100. Tunavyolinganisha lazima tuangalie uchumi wa nchi zetu na tuwatie moyo Viongozi wetu walioongoza nchi hii, kwamba kila mmoja ameongoza amefanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye sekta ya afya pia tulikuwa na maono ya ujenzi wa Zahanati kila Kijiji, maono ya ujenzi wa Vituo vya Afya kila Kata. Tumeona utekelezaji wake, tumeona enzi ya Awamu ya Nne uboreshaji wa Hospitali ya Muhimbili, ujenzi wa Hospitali ya Mloganzira, uanzishaji wa Kitengo cha Moyo, Awamu ya Tano imejenga zaidi ya vituo vya Afya 300, ujenzi wa Hospitali mpya za Wilaya, Awamu ya Sita nayo imejenga vituo 233 kwa muda mfupi, imejenga Hospitali za Wilaya 28 mpya, inamalizia Hospitali za Wilaya 66. Kwa hiyo Serikali zote kwa kuwa zimeongozwa na Chama Cha Mapinduzi na Ilani hii ya mwaka 2025 imejielekeza ukurasa wa Nane itazisimamia Serikali zake sasa kuandaa dira nyingine ya Taifa kuelekea 2050. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naomba ieleweke nchi yetu ina maono, Marais mbalimbali wametekeleza wajibu wao na tunavyoendelea. Inawezekana sasa kwa mazingira ya dunia inavyokwenda kuja na Dira nyingine ya Taifa kuelekea 2050 au kuelekeza 2100 lakini Awamu zote hizi tumeona. Licha ya changamoto zilizopo zifanyiwe kazi lakini Serikali inapoendelea kutekeleza ilani hii sasa ya 2025 tunaomba ijielekeze kupunguza mfumko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza sana Wizara ya Kilimo naamini nayo itatoa input nyingi katika kuwezesha bei ya bidhaa inapungua. Tumeona maono ya Mheshimiwa Rais ya kuanzisha Mfuko wa Mazao pia ahadi ya kutoa subsidy kwenye masuala ya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali mimi ninatoka Mkoa wa Pwani kwa namna ambavyo tumepata viuatilifu vya zao la korosho. Naomba kuunga mkono hoja, naipongeza Serikali iendelee kutekeleza ilani yetu kama ilivyokuwa katika Serikali zilizopita. Ahsante sana. (Makofi)