Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi pia na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami niungane na wenzangu waliotangulia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea kwenye Majimbo yetu, miradi ya barabara inaendelea vizuri, miradi ya maji na ujenzi wa vyumba vya madarasa ambao umepita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara ambayo aliifanya Mkoa wa Kagera tarehe 29 mwezi uliopita, ziara ambayo imetoa ufumbuzi wa kilio cha muda mrefu cha wakulima wa kahawa katika Mkoa wa Kagera, kutuondolea tozo 42 kati ya tozo 47 ambazo zilikuwa zinatunyonya na kututesa sasa tumebaki na tozo tano ambazo zimeleta unafuu wa kuweza kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nitaongelea sehemu kama tatu. Sehemu ya kwanza ni mfumuko wa bei, sehemu ya pili itakuwa ni issue ya ajira na kama nitapata muda kidogo nitaongelea habari ya TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi kwenye habari ya mfumuko wa bei nimekuwa najiuliza kitu kikubwa kimoja ambacho nimekuwa nacho. Kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba hili Taifa wakati wa janga la Corona limeipiga dunia Taifa hili tulisimama na Mungu kama tulivyosema na mambo yetu yalienda vizuri hatukuwa na lockdown, hatukuwa na nini na kila kitu kiliendelea kwenda sawa, hatukuona changamoto yoyote ile katika shughuli zetu za kiuchumi, lakini sasa baada ya hili janga kuwa limetukumba wenzetu walipokuwa wamejifungia baada ya kurejea kwenye shughuli za kawaida kunakuwa na uhaba sasa, supply and demand inaongezeka kwamba vitu vingi vinahitajika kwa wakati mmoja kwa wakati huo huo kwa hiyo, wafanyabiashara wanachukua advantage ya kupandisha baadhi ya bei ili waweze kujinufaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haianzii hapa tu inaanzia duniani huko imeshuka mpaka sasa imekuja imetukumbuka. Kitu kimoja ambacho nimekuwa najiuliza, kwa hali ya nchi sasa leo hapa tunaposimama huko nje ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengine wameshatangulia kusema hali ya wananchi ni mbaya mno, vitu vimepanda bei sana kupita kiasi. Statement ya nyanya kupanda bei, vitunguu kupanda bei, tukaanza kusema ni vita ya Ukraine mimi hiki kitu sikubaliani nacho! Nadhani tunakosa control kwenye nchi, kama Taifa ni lazima ifikie stage tujue jinsi ya kufanya control ya bei kwenye nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na Taifa ambalo watu wanajiamulia kupanga bei wanavyojua wao kwa kisingizio cha vitu vingine hakuna mtu anayeenda kuuliza, halafu tunakuja kuishauri Serikali kwamba tutafute hela ya kukopa na ku-inject kule, uta-inject mara ngapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye pesa ya UVIKO, Mama ameleta hapa 1.3 trilioni lakini matokeo yake mabati yalipanda bei, cement ilipanda bei, vitu vingi vilipanda bei, lakini baada ya vitu vile kupanda bei hakuna mtu ambaye amerudi nyuma akawaambia wale watu washushe bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Biharamulo bati linaenda Shilingi 38,000 la gauge 28, limeshafikia Shilingi 38,000 lakini kabla ya ujenzi ule mabati yalikuwa yapo chini ya Shilingi 35,000. Sasa unaweza ukaona kwamba tabia ya wafanyabiashara wa nchi hii kila wanapopata fursa ya kupandisha bei hata yale mambo yakimalizika bei huwa hazirudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la kwanza lazima kama Taifa tusimame tujue jinsi ya kujikwamua kutoka hapa, tusikubali ongezeko la bei kwenye kitu chochote kile, hiyo ndiyo itakayoweza kusaidia wananchi, kwa sababu tutakapokuja na wazo la kukopa na ku-inject pesa mzunguko unakopa anaelipa ni nani? Ni Watanzania walewale hakuna unafuu ambao unao wasababishia, kwa sababu watalipa kwenye kodi hakuna mfanyakazi ameongezewa mshahara, tunajua tarehe 01 Mwezi wa Tano kilio cha wafanyakazi Mama anatakiwa ajibu, sasa Mama atajibu mambo mangapi? Anatakiwa aongeze mshahara huku tukiwa tunalia na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idea ambayo mimi ninayo, maoni yangu mimi ni lazima…

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi, aah! Mheshimiwa Mtemvu.

T A A R I F A

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampa taarifa mzungumzaji kwamba asishangae bidhaa nyingine kupanda bei ilihali ni eneo moja tu analoliona yeye malighafi ya mafuta kupanda bei. Malighafi ya mafuta inasababisha multiplayer effect katika maeneo yote. Hoja kubwa hapo ni kuendelea kumuomba sana Waziri Mkuu anayeisimamia Serikali kuendelea kusimamia matumizi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi sasa wanalia huko barabarani wanalia kwenye vyombo vya mitandao kwamba matumizi ni makubwa sana yanayoendelea kwa Viongozi wetu wa Serikali.

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Chiwelesa, Injinia, unapokea taarifa?

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea na huko ndiko nilikokuwa naelekea kwenye solution, kwa sababu kazi yangu ni kuongea tatizo halafu baadae tuende kwenye kutafuta ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, idea ambayo ninayo ni moja, hii ni ripoti ya BOT kwenye issue ya Treasury Bond, tulipokuwa tunapewa ripoti hapa kipindi kilichopita tulipewa ripoti, tulikuwa tunaanza kuuza bond mwezi huu nadhani kesho zilikuwa zinauzwa. Kesho tulikuwa tunauza bond ya 20 years kwa asilimia 15.4, BOT wameshusha leo ipo asilimia 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 27 tulikuwa tunauza bond ya seven years kwa asilimia 9.48 leo wameshusha imeenda asilimia 10 na nyingine asilimia 10 leo wameshusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kimoja ambacho ninacho, unilindie muda wangu. Kitu kimoja ambacho ninacho ni kwamba ni lazima sasa kama Serikali imejitafakari upande wa BOT tumeanza kushusha hizi hisa na interest ambazo zipo ni lazima turudi nyuma tukae na mabenki, unajua unapotaka wafanyabiashara washushe bei, mfanyabiashara yupo tayari ku-adjust kwenye faida yake, lakini wafanyabiashara wengi wamechukua working capital kutoka kwenye mabenki na wakati wote wa CORONA mabenki yaliendelea kutoza interest ileile na wafanyabiashara wameendelea kufanya biashara katika interest zilezile zinatoka kwenye mabenki.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Msongozi, taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. ninampa taarifa mchangiaji anayechangia sasa, kwenye suala ambalo analifanya la kuishauri Serikali juu ya masuala ya uchumi. Mheshimiwa Mbunge anachokiongea ni sahihi kabisa na hata Bunge lililopita tumemsikia Mheshimiwa Mbunge akitekeleza majukumu yake alipokuwa anashauri namna ambavyo wenzetu wa Egypt wanachimba chima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa Ezra.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilindie muda wangu. Nilichokuwa nasema ni kwamba, hatuwezi kuwa na Taifa ambalo kila mmoja anajipangia vitu anavyovitaka. Tukumbuke tumetoka katika athari ya uchumi sasa wakati ule wa lockdown, vitu vingi sana vilisimama lakini katika Taifa letu mambo yalienda vizuri. Kwa hiyo ushauri wangu kwa upande wa Serikali, Serikali irudi nyuma, kwanza iongee na Commercial Banks zishushe riba kwa ajili ya wafanyabiashara ambao wamekopa mikopo ya kibiashara. Benki zikishashusha riba turudi sasa kwa wafanyabiasha tukawaambie kwamba, kwa sababu Serikali imewa-favor kwenye upande wa biashara iweze kushusha riba hali kadhalika wafanyabishara watengeneze faida ndogo lakini ile faida ndogo iweze kushusha bei ya bidhaa vinginevyo hali itakuwa mbaya na uchumi wetu unaenda kuathirika kwa sehemu kubwa.

MWENYEKITI: Ahsante sana, kengele yako ya pili imepigwa Mheshimiwa Ezra.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina dakika 10 hapa nilizihesabu sidhani kama zimetimia au umenichanganya na wa dakika tano?