Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza hoja aliyoongea Mheshimiwa Lusinde ni ya msingi. Ni kweli mtaani hali mbaya, ni kweli jambo hili Serikali mnatakiwa mlichukulie kwa udharura wake. Mliotoka Mikoani mnajua na maeneo mengine mnajua hali siyo nzuri ya upandaji wa mafuta pamoja na bidhaa mbali mbali. Kwa hiyo, ni jambo la msingi wananchi wana hali mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wabunge, kama wawakilishi wa wananchi kuna wajibu mkubwa wa kulitafakari kwa kina suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nijielekeze ukurasa wa 44. Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema Serikali ina mpango wa kuagiza ndege zingine ili zifike 16. Ni jambo jema sana na hakuna mtu anayepinga ununuzi wa ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunazungumzia hapa, hivi tunaendaje kufufua Shirika la Ndege? Kununua ndege peke yake ni kulifufua? Hili shirika kuna mipango madhubuti ya uendeshaji wa kibiashara? Je, tumeweka mikakati ya kuhakikisha ufufuaji wake utaongeza Pato la Taifa na uchumi kwa Taifa letu? Hayo ni mambo ni mambo ya kujiuliza, lakini suala la ndege kila Mtanzania anaona umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, 2016 wakati Shirika la Ndege linafufuliwa kwa Bombadia mbili ilikuwa na mtaji hasi Shilingi Bilioni 146, leo ina mtaji hasi Shilingi Bilioni 240, ukilinganisha mtaji na madeni ya takriban Shilingi Bilioni 371 haviendani! Sasa sawa tunaleta ndege hali ya Shirika la Ndege ni mbaya na Mheshimiwa Rais pia alisema linatakiwa lifanyiwe utaratibu liweze kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaleta ndege na matokeo yake ni nini, shirika hatujalipa mtaji, hatujaliwekea mikakati ya kibiashara, tumenunua ndege hatujalipa madeni ya ndani na nje ya nchi, ndege zinakamatwa, Serikali walichofanya wakakabidhi ndege kwa wakala! Wakala ni wa Serikali haizuii ndege kukamatwa, bado ni mali ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi wakati wanakabidhi wakala wa ndege (TGFA) lengo kubwa lilikuwa moja tu ni kwamba ndege zikinunuliwa zisikamatwe na wakasahau yule ni wakala wa Serikali wala hakukuwa na mpango wa biashara, bado tu ndege zilikamatwa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongeza gharama za uendeshaji, tunaongezea mzigo ATCL bila sababu na sababu siyo kukwepa ndege zisikamatwe sababu hapa kumaliza tatizo ni kulipa madeni na kuliongezea shirika mtaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo naifananisha wakati tunasema mifuko ya hifadhi ya jamii ina hali mbaya wakaona walete sheria waiunganishe badada ya kulipa madeni kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, ndiyo kinachotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna madeni ndani na nje ya nchi hatutaki ndege zikamatwe tukapeleka kwa wakala haikuzuia ndege zinakamatwa kwa sababu yule wakala bado ni wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hapa ni kuweka mikakati dhabiti ya uendeshaji wa shirika letu tulipe madeni ndani, nje ndege zetu ziruke, tuitangaze nchi yetu na huku uchumi ukue. Sasa hii taarifa ni ya Serikali yenyewe wanasema hata Serikali ilivyohamisha umiliki kwa wakala TGFA bado haijaleta ufanisi na gharama za uendeshaji zimepanda zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano unapozungumzia matengeno ya ndege ATCL wao wenyewe wanatengeneza ndege kwa gharama kubwa kwenye kukarabati injini kwenye karakana zao. Lakini hapohapo wanalazimika kutoa tozo kulipa tozo za ukarabati kwa wakala, siyo sawa! Imeshafika zaidi ya takribani Shilingi Bilioni 99 madeni juu ya ukarabati wa ndege kwa wakala lakini wao wenyewe pia matengenezo makubwa wanayafanya kupitia karakana zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kwenda hivi, shirika haliwezi likawa na tija, lazima tujitafakari na uzuri hatujachelewa ni shirika letu wote tunapenda kuona fahari ya ndege, tukae tujipange namna bora ya kuendesha shirika letu la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nikutolee mfano kwa miezi Minne ile ya COVID-19 ilivyopamba moto, ndege hazikusafiri, lakini kwenye tozo peke yake ililipwa Shilingi Bilioni 15 ndege hazikuruka, kwenye ukarabati Shilingi Milioni 17 ndege hazikuruka miezi minne, sasa tunajiuliza kwa nini, hivi vyote tunafanya kwa ajili ya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusiokoe hizi pesa zikaenda kutekeleza miradi mingine tukapunguza hali ngumu kwa wananchi wetu. Kwa nini haya madeni hizi hasara ambazo zinatengenezwa ambazo sasa hivi zimeshafikia zaidi ya Shilingi Bilioni 130 tungeenda kumaliza ahadi ngapi zilizotolewa kwenye majibu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunaendelea kulazimisha mkataba kwa wakala ambao ndege zinajiendesha bila faidi, zinajiendesha kwa hasara ambazo hizo hasara tungeweza kupunguza tukaenda kumaliza matatizo ya maji kwenye majimbo yetu tukamkomboa kumtua mwanamke ndoo kichwani? Ni sisi tu wenyewe kupanga ni kuchagua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma pia ukurasa wa 39 wa Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema wameweza kulipa pesa za mifuko ya hifadhi ya jamii zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili kutumia hati fungani, sawa na hii ni ile ya Pre-98 sasa mimi niulize hii tu mmetumia miaka 22 ya Pre-98 hizi. Je, mtahitaji miaka mingapi mlipe madeni ya fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii pesa ya wastaafu ya kuanzia mwaka 1999 kwenda mbele mnahitaji miaka mingapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hizi hela mnakuwa kama mnazichukuwa tu hamlipi kwa riba, lini mlikopa kwenye mabenki mkalipa bila riba? tukisema hizi pesa za wastaafu wetu mnazitumia ndivyo sivyo, ndiyo maana wanakaa zaidi ya miezi sita zaidi ya mwaka hawajalipwa viinua mgongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tu wakati napitia simu yangu nikapata meseji, wastaafu wazee wangu kwenye Maktaba Kuu ya Taifa hawajalipwa na pesa zingine ile ni Maktaba ya Serikali Mwajiri hajapeleka michango wamepunjwa kwenye kiinua mgongo chao, kwa nini tunafanya haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana pesa za wastaafu zisichukuliwe poa! siyo sawa hawa wametumikia nchi yao kwa jasho na damu, mmekaa na hela za watu miaka 22, leo hapa Waziri akasema tunalipa kwa hati fungani hizo nyingine mtatumia miaka mingapi mliochukuwa kwenda kuwekeza kwenye viwanda na bado havijalipa vinatengeneza hasara. Mmechukuwa mkaenda kuwekeza kwenye majengo ambayo hayafanyi kazi hayajalipa, mtatumia miaka mingapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je watumishi wa Taifa hili waelewe nini wanayoipenda nchi yao, hawavumilii hawana wa kuwasemea ndiyo sisi tunakuja kuwasemea na bado wanafanya kazi kwa sababu wanajua kufanya kazi kuilinda nchi yao ni jukumu la kila Mtanzania, tuwatie motisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi hatujawaongeze mishahara hatujawapandishia madaraja na bado pesa zao za hatma ya uzeeni hatujui zinafanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)