Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukuwe fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwepo hai hadi wakati huu, lakini jambo la pili niishukuru sana Wizara ikiongozwa na Waziri Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Manaibu Waziri na watumishi wote katika wizara hiyo kwa ushirikiano ambao wanaendelea kunipa mimi pamoja na wananchi wa Kilolo katika kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais pia kwa jinsi ambavyo Kilolo imeanza na inaendelea kukumbukwa sasa kwa mambo mengi tofauti sana katika historia ya Jimbo la Kilolo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo madarasa ya sekondari 73 yamejengwe, shilingi milioni 800 Hospitali ya Wilaya karibu inakamilika kwa mara ya kwanza tangu uhuru tulikuwa na kituo kimoja cha afya, tunajenga vituo vya afya vinne kwa mpigo Ruaha Mbuyuni, Ilula, Nyarumbu pamoja na Ng’ulule vituo vinajengwa, lakini pia tunayo sekondari Kata ya Kimara haikuwa nayo inajengwa pamoja na mambo mengi nikiorodhesha nitamaliza muda wangu kwa kushukuru tu, lakini sasa naomba niende kwenye mambo mengine.Tunashukuru sana kwa ushirikiano ambao tunaendelea kuupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya kwanza nitakayoizungumzia inahusu mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo; zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo inatengemea mazao ya misitu, mazao ya misitu tunayozungumza maana yake ni pamoja na nguzo, mbao na mazao mengine yanayofanana na hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nieleze ili Wizara ya TAMISEMI ijue athari zitakazotokana na maamuzi ya Wizara au idara nyingine za Serikali kuamua kununua nguzo nje ya nchi hii, tutakapoacha kununua nguzo kutoka kwenye Kiwanda cha New Forest kilichopo Wilaya ya Kilolo maana yake ni kwamba tujiandae kupunguza mapato ya Kilolo kutoka shilingi bilioni 4.5 sasa hizi kwenda shilingi bilioni mbili na point na kwa hiyo Serikali ijiandae kuleta fedha kuja kuweka hiyo nakisi hatutakuwa na hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kwa hiyo nataka Waziri anapoongea na Mawaziri wengine pamoja na Serikali inapozungumza ilijue hilo, athari za huo uamuzi ni nini kwenye mapato ya Serikali, ninaomba hili lieleweke vizuri ili nitakapokuja hapa kuomba fedha zaidi kutokana na kupunguza mapato baada ya hayo maamuzi ya kununua nguzo nje Serikali ikumbuke kwamba mimi nilisema na hii iwekwe kwenye rekodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ni kuhusu miradi ya kimkakati; Mheshimiwa Waziri bahati nzuri ulikuwa Wizara ya Viwanda na Biashara na ulitembelea Kilolo na bahati nzuri ulitembelea mashamba ya chai, nataka nikuambie mradi wa kimkakati uliletwa mwaka 2018 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo kujenga kiwanda kile cha chai hata jibu hadi leo halijawaji kupatikana kwamba ni mbovu, una nini, hatujapata jibu na kiwanda hakijajengwa na bahati nzuri na Waziri wa Kilimo yuko hapa anajua tunavyoangaika kutafuta fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mmejenga masoko sawa, mmejenga stand huko sawa mngetuambia basi sisi Kilolo tumekosea nini kwenye kuandika ili tuweze kupewa fedha tuweze kujenga kile kiwanda cha chai ambacho kinaajiri watu 2,000 na sisi kwetu watu 2,000 ni wengi, ambacho kitaongeza uzalishaji kwenye chai na tutaongeza mapato ya Halmashauri kwa sababu yale mashamba yanamilikiwa kwa asilimia 40 na Halmashauri, kwa asilimia 10 na Msajili wa Hazina ambayo ni Serikali tena hiyo Hazina inayotoa hela hayo mashamba yanamilikiwa kwa asilimia 50 na wananchi kule hayamilikiwa na taasisi binafsi, inashindikanaje kutoa fedha kwa ajili ya ule mradi wa kimkakati pale?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninalo lile andiko kama limepotea au liko mahali niko tayari kukuletea twende mguu kwa mguu Hazina tupate zile fedha kile kiwanda kipate kujengwa na mitambo inunuliwe na zile hela sio nyingi ni kama tu shilingi bilioni tatu ambazo kule mmetoa shilingi bilioni 60 majengo makubwa tunashindwaje kutoa fedha kidogo hivi kwa ajili ya kiwanda cha chai kilichokaa miaka 30 hakijengwi na hela zipo kila siku tusomee miradi ya mkakati ya mijini na sisi tunataka hizo fedha kwa ajili ya mradi wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya jambo hili naomba pia nizungumzie kuhusu vifaatiba; ninashukuru sana kwamba umejengwa vituo vya afya vizuri pale Ruaha Mbuyuni mmetupa na hata shilingi milioni 300 juzi tumalizie maana kile kilianza kujenga mwaka wa fedha uliopita na pia pale Ilula tunacho na ninyi mnajua haya ni maeneo ya barabara kuu, sasa hivi karibuni kulitokea ajali pale Ruaha Mbuyuni watu walipelekwa pale nadhani ni kama watu tisa au kumi ambao walihitaji huduma kwanza, madaktari hakuna, lakini vifaatiba havipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maeneo kama haya tumeambiwa kuna ajira zinakuja maeneo ya barabarani, maeneo yenye Vituo vya Afya ambavyo vinahitaji attention kubwa kwanza madaktari wapelekwe, lakini pili tutafute uharaka wa kupeleka vifaatiba kwa sababu pale sikutakiwa peke yangu nisimame, Wabunge wote humu mnapita Ilula, Wabunge wengi humu mnapita Ruaha Mbuyuni mnapoenda kwenye sehemu zenu huko, hili ni suala la sisi wote na wananchi wote wanaopita mle kwa sababu hatuwezi kujua ya kesho, ninaomba sana vifaatiba kwenye hivi vituo vya afya viwili ambavyo vimekamilika, ninawashukuru sana vifaatiba vipewe kipaumbele kwa sababu ya unyeti na umuhimu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo ningependa kulizungumzia nalo ni suala zima la TARURA pamoja na fedha na jinsi zinavyotolewa, mambo mawili; jambo la kwanza ni suala zima la magari ambalo limeshazungumzwa na vifaa, tulipokuwa kwenye Kamati mimi ni mwamakamati wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, tulipokuwa kwenye kamati tuliona kwamba kweli fedha za magari zimetolewa, lakini mamlaka zinazonunua hazijanunua zaidi ya magari 100 na fedha zimeshalipwa, haya magari yangeweza kugawa kwenye hizi Halmashauri yangetosha, kupunguza angalau hiyo kero.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tuiombe Serikali kwa sababu ni hiyohiyo tujue kikwazo kinachozuia magari haya kununuliwa na kugawiwa kwa hawa hiyo mamlaka ingekuwa ni taasisi binafsi imepewa fedha za magari zaidi ya 100 hainunui mwaka mzima, hicho ni kiashiria kinaweza kupeleka hadi kwenye karibu na uhujumu, sasa ni Serikali hatuwezi kuita hivyo. tunafanyaje kuhusu watendaji au mahali popote panapokwamisha ununuaji wa haya magari? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili TARURA ina sema kwamba wanasajili barabara, sasa barabara inayosajiliwa ni kwamba imetengenezwa yako maeneo kama kule kwangu kwa mfano pale kutoka Idete ili ushuke kule Mngeta ni pori, pana mchoro wa barabara, lakini ni msitu, kila tukienda pale wanasema tengenezeni ili tusajili, atengeneze nani na ile ni hela nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni lazima itobolewe ile barabara kama ingelikuwa ni ndogo kwa hela ndogo lakini barabara kubwa kama ile lazima itengewe fedha ili itoboke na ile ni barabara muhimu kiuchumi, ndio tungeweza kusafirisha mbao kwa treni kwenda Dar es Salaam, lakini hatuwezi kuitoboa kwa mikono, walijaribu pale walienda wananchi walishindwa ni sehemu ambayo ni lazima Serikali iwekeze. Ninaomba TARURA kwa dharula itenge fedha kwa ajili ya kutoboa barabara ile ili iweze kufanikiwa na kufanya kazi. Nakuomba sana kupitia kwako namuomba sana Waziri aingalie barabara kama hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na barabara nyingine ambazo ni muhimu kiuchumi nataka kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge mkila njegele, viazi na hizo mbogamboga nyingine zote kwa asilimia kubwa zinatoka Kilolo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara kama ya kutoka Kitoo kwenda Masisiwe, barabara kama ya kutoka Ihimbo kupitia Itimbo kuja kutokea Kitelewasi ambako ndo mahindi mengi mnakula haya ya njiani, barabara ya kutoka Nyanza kwenda Mtandika vitunguu karibu vyote vinatoka huko hizi barabara zinahitaji ile milioni mia tano tu na ndio maana wakati ule nikakuambia mimi nikipata shilingi bilioni 1.5 inapunguza sana hizi kero. Lakini si kwa ajili yangu tu ni kwa ajili ya Watanzania wote wanaoatarajia mazao kutoka kule lakini pia kwa ajili ya kuongeza mapato ambayo yanaweza kutusaidia.(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)