Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Hotuba ya Waziri wa TAMISEMI na nianze kwanza kwa kupongeza wananchi wote wa Tanzania kwa namna ambavyo kwa kweli wanaiunga mkono Serikali pale ambapo Serikali inapeleka fedha wao wanaongezea. Tumeona ambavyo Serikali inapeleka shilingi milioni 12 kujenga madarasa wao wanaweka nguvu kazi na michango yao, nawashukuru sana. Lakini niwashukuru watumishi wote wa umma ambao ndiyo wanaosimamia fedha ambazo tunapitisha hapa, nasema ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niwapongeze wasaidizi wa Waziri nikianza na Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu kwa kazi kubwa wanayoifanya, tunawashukuru sana. Lakini majemedari hawa watatu, Naibu Mawaziri wawili na Waziri wao, sisi watu wa Hai tumewapa majina; ndugu yangu Festo kule wanamuita mzee wa nkwansira na anajua kwa nini wanamuita nkwansira na ndugu yangu Silinde hapo wanamuita mzee wa makeresho anajua kwa nini wanamuita hivyo, Waziri nitakupa jina lako nikimaliza kuchangia hotuba yangu wanakuitaje kule Hai. (Makofi)

Kwa kweli kwa ujumla tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea vijana hawa wenzetu wachapakazi ambao kwa kweli wanabeba sura nzuri ya Tanzania, kazi zinakwenda kwa viwango vya hali ya juu. Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niombe pia nimshukuru sana Waziri. Ninakushukuru Waziri na watu wa Narumu watu wa Hai kwa ujumla wanasema ahsante sana. Tulikuwa na barabara yetu ya kuanzia Mferejini kwenda Makoa kilometa 18 imeanza kujengwa kwa maandalizi ya kupokea lami, wewe umeniahidi unaenda kumaliza fedha zile ili lami ikamilike ya barabara ile, tunakushukuru sana. Lakini tunakushukuru umetuahidi barabara ile ya Bomango’ombe kwenda TPC kilometa 25 na yenyewe itajengwa kwa kiwango cha lami. Tunasema ahsante sana Mheshimiwa Waziri na sisi tunakuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijikite kwenye hotuba ya Waziri na nianze na eneo ambalo tumelijadili sana, mimi ni mjumbe wa Kamati ya USEMI. Eneo la asilimia 10 fedha ambazo zinatokana na mapato ya Halmashauri; fedha hizi zinakopeshwa makundi matatu, kundi la vijana, kundi la walemavu na kundi la wakinamama. Lakini wakati tunapitia taarifa hii kumekuwa na changamoto, fedha hizi zina matatizo makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninasimama hapa kumshauri Waziri, na Waziri wewe umeshiriki kwenye Kamati umeona kilicholetwa pale. Fedha hizi zinatumika visivyo, fedha hizi taarifa zake haziko sahihi. Sasa ninaomba sasa hivi ukitazama kuanzia Januari mpaka leo kuna shilingi bilioni 35 ambazo zimekwishakopeshwa. Kwa hiyo, utaona ni fedha nyingi sana, lakini Mikoa imeleta taarifa ambazo zina mapungufu mengi sana ambazo hazioneshi marejesho kiasi gani yamerejeshwa, fedha kiasi gani zimerejeshwa na vikundi. Sasa ninachoshauri hapa; moja, ninaomba tulete sheria ile hapa ifanyiwe mabadiliko. Tufanye mabadiliko kwanza kuongeza kundi la wanaume, maana wakina baba wamesahaulika kwenye hili, nimeshashauri tena Bunge lililopita, lakini narudia tena na kwenye kamati tumesema tuongeze wigo mpana ili na wanaume nao waweze kukopesheka na wanufaike na hizi pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri kanuni zako ziongeze makali ili kuwe na akaunti maalum ya kupokea fedha hizi, lakini na akaunti maalum ya kupokea fedha za marejesho ili mwisho wa siku tuweze kuona kwenye 10 percent tumekata kiasi gani, zile za marejesho ziko wapi tujumlishe za marejesho, tujumlishe zile asilimia 10 lakini tutoe fedha zao za usimamizi. Hizi zinazobaki tuone zinakopeshwa kwa kiwango gani. Lakini pia kama ambavyo tulishauri kwenye Kamati, naendelea kusisitiza ni muhimu sana tuwe na mfumo wa ku-capture mambo haya. Fedha hizi zitolewe kwa mfumo wa TEHAMA ambavyo Wizara inaweza kuona, level la Mkoa inaweza kuona na level ya Halmashauri na kwenye level zote hizo kuwe na watu ambao wana-approval ili kuondoa watu kukopa mara mbili, lakini kuweza kuwabana wale wanaokopeshwa waweze kurejesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba pia nizungumze kuhusu Tume ya Utumishi wa Walimu; Tume hii inafanya kazi nzuri, lakini Tume hii haijawa kamilifu. Walimu nchi hii wana mabosi wengi mno. Sasa nilikuwa naomba hapa Waziri tuone namna sahihi ya kuifanya Tume hii iwe bora, tuiongezee nguvu ili kama tukiamua ndiyo Tume ya kusimamia walimu ifanye hivyo kuliko mwalimu anasimamiwa na TAMISEMI, kila mtu ni kiranja wa mwalimu. Sasa mwisho wa siku tunajikuta hawa Walimu tunawapa mzigo mzito ambao wanashindwa kuisimamia kazi yao ya kitaaluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana sana kaeni chini muone namna ya kutuletea tufanye mabadiliko, walimu wawe centralized somewhere wasimamiwe na chombo kimoja ambacho kwa mawazo yangu Tume ya Utumishi wa Walimu ingefaa kuwa chombo sahihi cha kusimamia walimu Tanzania na kuwaacha walimu kutokusimamiwa na watu wengi kama ilivyo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba nishauri jambo linguine, tunaenda kupitisha hapa bajeti na kwenye bajeti hii vifungu vya usimamizi vimeongezeka sana na kupelekea matumizi ya miradi kushuka zaidi ya asilimia 14 jambo ambalo ni zuri na ofisi ya ma-DC zimepata fedha za kutosha.

Naomba kushauri hapa ofisi za Maafisa Tarafa ambapo ni kiungo kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa hao Maafisa Tarafa wamekuwa watu wa kuishi kwa hisani kitu ambacho siyo sawa, sasa ofisi za ma-DAS zimepewa fedha. Mimi niombe wapewe special vote ya kwao. Kwa sababu ofisi ya Afisa Tarafa inajitegemea wapewe sub-vote yakwao ili kwamba kama wanahitaji matumizi yao fedha ziende kule kuliko ilivyo sasa hivi pesa zinapelekwa ofisi ya DC halafu inakuwa ni utashi wa DAS kuwapa au kutokuwapa. Kwa hiyo, niombe sana hawa watu wanatusaidia kwenye usimamizi wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niombe tutazame tena, wenzangu hapa wamezungumza kuhusu posho za Madiwani. Mimi niseme kwa Madiwani tumefanya vizuri, lakini tuone namna ya kuwaongezea na Wenyeviti wa Mitaa. Tufike mahali pia tutazame hata Watendaji walioko kule, tunafahamu wanapata mishahara yao, lakini hebu tuwatazame namna ya kuwapatia mafunzo ili na wao waweze kufanya kazi kwa wakati. Wakati mwingine tunapeleka tu, tunashindilia maagizo kule kwa Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata lakini hatuwapi taaluma ya nini kinatakiwa kufanyika kwa wakati ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninaomba nizungumze kuhusu miradi ya kimkakati; hii miradi ya kimkakati wenzangu hapa wameeleza masoko maeneo mengi hayakufanya vizuri, kwa sababu walioibua mikakati ile hawakutufikisha mwisho.

Mimi niseme Mheshimiwa Waziri pale Hai tuna soko la Kwa Sadala tayari tumeshakuletea ramani hapo. Mimi niombe hebu tukajifunze pale Hai kwa kujenga hilo soko. Lile soko letu lina kitu cha tofauti, mle ndani tumeweka sorting industry, mle ndani tumeweka viwanda vya kufungashia, mle ndani tumeweka viwanda vya kuongeza thamani mazao. Lakini pia tumeweka sehemu ya wakinamama kuwaacha watoto wao wapumzike pale kama day care center, na soko liko mjini pale Kwa Sadala. Soko ambalo ukitazama linapokea karibu kata zote na nchi nyingi zinakuja kununua pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe huu mradi Mheshimiwa Waziri tafadhari sana mtusaidie na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Rais mwenyewe ameahidi pale mara mbili soko hili la Kwa Sadala, tafadhalini sana mtusaidie lijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme jambo moja jana nilikuwa kwenye msiba kwenye Kata Uroki pale Uswaa. Mheshimiwa Waziri kila aliyekuja kunipa mkono pole Mheshimiwa Mbunge alikuwa ananiambia tuna barabara yetu; barabara ya Uswaa – Kwa Sadala; Uswaa - Bwani kuna mahali ambapo pale Uroki pa kupandia juu hapapitiki kabisa na ile barabara ndiyo tunategemea ipitishe ndizi zile Kwa Sadala, ipitishe ndizi zije Dar es Salaam, zije kwetu hapa Dodoma. (Makofi)

Niombe sana, inawezekana nimekuomba maombi mengi ya lami na wewe umeniahidi lakini hii basi hata changarawe, angalia fungu chochote unachoweza kupata hata kwa kipande kile kidogo cha pale kwenye bonde la kushuka Uroki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)