Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia, lakini nimpe hongera sana na pongezi nyingi sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nyingi ambazo anazifanya Makete, lakini
Mheshimiwa Waziri kaka yangu Innocent Bashungwa ni mmoja ya Mawaziri ambao sisi vijana tunajivunia sana kwa jinsi ambavyo anatusikiliza na anatupa nafasi kwenye wakati tofauti tofauti ambapo tunakuwa na matatizo, lakini pia Naibu Mawaziri wake wote wanatupa ushirikiano mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze sana Mkuu wangu wa Wilaya Ndugu Juma Sweda anafanya kazi nzuri sana, Mkurugenzi wangu Ndugu William Makufu anafanya kazi nzuri sana kule Makete, lakini na Watendaji wote wa Halmashauri wanatupa ushirikiano mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Serikali hii sisi wana Makete tunaipongeza kwa sababu kuna mambo ambayo yamefanyika kwa muda ambao Halmashauri ya Makete ilikuwepo haya mambo hayakufanyika. Mimi nimeingia nikiwa Mbunge wa Makete tulikuwa na vituo vitatu tu vya afya, ninavyozungumza leo tumejengewa vituo vitatu vingine vya afya vya shilingi bilioni 1.5. Lakini tuna kata ambazo zilikuwa hazina shule Kata ya Bulongwa, Kata ya Mlondwe na Kata ya Kigala, tayari tumeanza mkakati Serikali imetupatia fedha, tunajenga shule ya Mlondwe na bado shule mbili mradi wa zaidi shilingi bilioni 1.8; lakini tuna shughuli nyingi ambazo tunaendelea nazo kwenye ujenzi wa madarasa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Makete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niombe Wizara mtukumbuke sana Makete kwenye suala la ukarabati wa shule za msingi. Tuna shule za msingi nyingi ni kongwe kwenye nchi hii hazijakarabatiwa kwa muda mrefu, tuna shule ya Misiwa, tuna shule ya Igorwa, tuna shule ya Asunzi tuna shule nyingi ndani ya Wilaya ya Makete, tunaomba Wizara itukumbuke ili shule hizi ziweze kufanyiwa ukarabati na kujengwa. Lakini tuna vituo vya afya kwa mfano Kituo cha Afya cha Lupila, wananchi wa Makete wanasafiri zaidi ya kilometa 100 kutoka Lupila kwenda Makete Mjini, kwa ajili ya kufuata huduma za afya pale ambapo kwenye kituo cha afya imeshindikana, hawana ambulance hawa wote wanatumia bodaboda kilometa 100, tunaomba mtukumbuke ambulance kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Lupila. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nizungumze mambo mawili makubwa leo. Leo nina jambo kubwa la TARURA; kwanza niwapongeze TARURA kwa kazi ambayo wanaifanya na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri maana break yake ya kwanza baada ya kuteuliwa breki ya kwanza ilikuwa Makete kwa ajili ya shughuli ya TARURA. Mheshimiwa Waziri uliona hali ya Makete ya barabara sisi Wilaya ya Makete inaitwa Wilaya ya Kazi wananchi wetu ni wachapakazi wakubwa, lakini changamoto kubwa tuliyonayo sisi ni barabara za vijijini hazipitiki, uliona hali halisi. Nawapongeza TARURA kwa yale wanayoendelea nayo, lakini ninaushauri na hii kwa Mheshimiwa Waziri unaweza ukawa ndio game changer wa TARURA ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 TAMISEMI mliandika barua kwenda kwenye Halmashauri mkizuia, kuna Halmashauri ambazo tulikuwa tayari kukopa mitambo ya kujenga barabara kwenye Halmashauri zetu. TAMISEMI wakazuia kwamba Halmashauri zisinunue wala zisikope kwa namna ya kwamba mnataka kulinda local constructors (wakandarasi wa ndani) waliopo ndani. Lakini nikuombe Mheshimiwa Waziri kama ambavyo leo Wizara ya Maji wananunua mitambo kwa ajili ya kuchimba mabwawa, ni wajibu sasa na ni wakati sasa TARURA kwa sababu ni department na ni Wakala, ruhusuni wawe na mitambo ya ujenzi wa barabara kwenye Miji na Halmashauri ambazo tuna mazingira magumu kama Makete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mwananchi wa kutoka Lupila kwenda Makete kupita Kipengele anasubiri fedha ya maintenance ya barabara kutoka Mkoani hadi ije ikamilike masika imepita, watu wamefariki, mazao yameozea shambani. Lakini tungekuwa na mitambo ya barabara pale Makete kutoka TARURA tungeenda na mitambo yetu, tungemwaga kifusi, tungesafisha barabara. Kwa ununuzi wa fedha za Serikali mitambo hata shilingi bilioni mbili haizidi mngefanya kwa nchi nzima, mngekuwa mmeokoa mambo mengi sana na fedha ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawasihi na ninawaomba tusije tukaja na hoja ya kulinda hawa wakandarasi kwamba wakandarasi wadogo tutawazuia. Mheshimiwa Waziri wajibu wa kwanza wowote wa Serikali ni kuhudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la watu wa private sector hilo ni hatua nyingine ninyi nendeni mkajenge barabara hawa nao watapata nafasi zao. Kwa sababu, mmejenga vituo vya afya msingejenga tungetegemea hospitali binafsi tungefika leo hapa? Tunaomba TARURA wawezeshwe… (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napenda tu kumpa taarifa Mheshimiwa Sanga anaongelea hoja ambayo ni valid sana, ukizingatia barabara hizi ambazo ziko chini ya Halmashauri au TARURA ni takriban asilimia 85 na tunajua kabisa kwamba upande wa maji kule tuna DDCA. Kwa hiyo, ni mbadala sasa hivi kuweza kuhakikisha kwamba wale ambao wanajiweza kununua mitambo wanunue mitambo. Kwa sababu kama DDCA ipo na haizuii contractor hawa ambao ni local kwa nini mzuie kwa upande wa Halmashauri. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sanga taarifa hiyo.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipokea taarifa hiyo na ninaomba Mheshimiwa Waziri ataandika historia kwenye Taifa hili, ni mmoja kati ya vijana ambao tunawategemea ni kuruhusu jambo kama hili lifanyike kwenye nchi yetu. Halmashauri zenye uwezo wa kuwa na excavator, kuwa na ma- roller, kuwa na ma-tiper ziruhusiwe. Wataalam watakudanganya tu hapa kukupiga bumbuwazi ili watengeneze chain na watu ambao ni constructors ambazo ni private sector.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninakuomba simamia msimamo huo kama Mheshimiwa Aweso anavyokwenda kuchimba mabwawa, anza kujenga barabara vijijini na tutakuja kukushukuru.

Mheshimiwa NaibU Spika, barabara vijijini ndio sera ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anasema tuwezeshe barabara vijijini zipitike. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri una nafasi ya kuyafanya haya mambo ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ninataka kuzungumza ni kwenye asilimia 10 kwenye 10 percent ambazo zilianzishwa na sheria yetu hapa nchini kwa makusudi mazuri sana ya kuona tunasaidia vijana, akina mama na watu wenye ulemavu. Hii sheria ilianzishwa kwa ajili ya kusaidia watu hawa ambao ni vijana wenzetu, lakini 10 percent ambayo tumekuwa tukitenga kwa ajili ya vijana wa Taifa hili, kwa ajili ya akina mama wa Taifa hili imegeuka ni 10 percent ya watu ambao wana uwezo na sio vijana wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza kwa data ukisoma kwenye hotuba ya Waziri kwenye moja kati ya maelekezo toka tuanze kukopesha 10 percent mwaka 2017/2018 hadi 2021 nchi hii tumekopesha zaidi ya shilingi bilioni 300 kwa asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini toka tumeanza kukopesha tuna zaidi ya shilingi bilioni 222 ziko kwenye mikono ya wanyang’anyi na ninataka nikupe mfano Mheshimiwa Waziri; mfano ni Mkoa wa Tabora toka mwaka 2018 hadi 2021 wamekopesha shilingi bilioni 5.7, lakini fedha zilizorudi hadi leo ni shilingi bilioni mbili tu fedha zingine zote ziko mifukoni kwa watu. Ukienda Mkoa wa Pwani mwaka 2018 hadi 2021 wamekopesha shilingi bilioni 11 lakini hadi leo wamerudisha shilingi bilioni nne tu fedha zingine zimepotea. Ukienda Mkoa wa Mwanza wamekopesha shilingi bilioni 8.9, wamefanikiwa kurudisha shilingi bilioni 3.9 tu fedha zingine zote zimepotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Mkoa wa Dar es Salaam wamekopesha bilioni 52.3 wamefanikiwa kurudisha bilioni 14 tu fedha nyingine zote zimepotea; ukienda Mkoa wa Mbeya anakotoka Spika wa Bunge wamekopesha bilioni 12 toka mwaka 2018 hadi leo wamerudisha bilioni saba tu fedha nyingine zote zimepotea; achana na Simiyu wamekopesha bilioni nne imerudi bilioni moja, achana na Geita wamekopesha bilioni sita zimerudi bilioni tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zipo kwenye mikono ya wanasiasa, zipo kwenye mikono ya watumishi wa Serikali ambao wanatengeneza vikundi vya vijana, wanawa-lob, wakifika pale wanakopeshwa fedha zinaingia mifukoni mwao, vijana hawafaidiki chochote. Kwa hiyo… (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, anachokiongea ni very valid na kuna muongozo wa 10% ambao uliandaliwa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, mpaka tunavyozungumza bado haujapelekwa kwenye Halmashauri kwa ajili yak u-guide na muongozo huo ungekuwa suluhisho kwenye matatizo ambayo anazungumza mzungumzaji anayechangia sasa hivi, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sanga, Taarifa, unaipokea?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea. Mheshimiwa Naibu Spika, nini nataka kuzungumza, Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, anaweza kuzifuatilia fedha hizi zaidi ya bilioni 222 zilizoko mikononi kwa wahuni. Kwa nini nasema ziko kwenye mikono ya wahuni?

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda ukafuate Halmsahauri ya Temeke ufuatilie fedha ziko kwa nani…

(Hapa kipaza sauti kilizimwa)

NAIBU SPIKA: Tayari, muda wako umekwisha.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, bado sijamaliza, bado dakika moja. Naomba dakika moja tu.

NAIBU SPIKA: Aah, sekunde tatu, sekunde tatu maliza.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri fedha hizi shilingi bilioni 222 zilikuwa zina uwezo wa kutafutwa na zikaenda kutatua matatizo ya barabara, kuweza kununua mashine za kufyatulia tofali mkawapa vijana, mkaenda mkanunua mitambo mingine ambayo imeandikwa kwenye project ikasaidia vijana. Tafuta bilioni 222 ziko wapi zisaidie nchi yetu kwa sababu ni fedha ambazo ziko kwa viongozi wa taasisi, zipo kwa wanasiasa… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante, umeeleweka, ahsante sana.